HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI: NYWILA NIMEFUNGULIA

WOTE ninawaambia, simu naifungulia,

Vyote nilivyozibia, nati zote naachia,

Nywila nilijifichia, kwake namfunulia,

Tuliapa kwake Mola, sisi ni mwili mmoja.

Mwenzi ataangalia, yale ninaangalia,

Na kusikilizia, wewe utayonambia,

Simu kwake ni huria, nyote nawatangazia,

Tuliapa kwake Mola, sisi ni mwili mmoja.

Mlio akisikia, mtu ananipigia,

Ninapomsikizia, sauti naachilia,

Siri kunisimulia, usije ukarudia,

Tuliapa kwake Mola, sisi ni mwili mmoja.

Na yake akiachia, mimi sitamwingilia,

Kama atajisikia, pia nitafurahia,

Ni nini chakufichia, wamoja kutuzibia?

Tuliapa kwake Mola, sisi ni mwili mmoja.

Hadi hapa nafikia, sana nimefikiria,

Simu inaniwangia, ndoa kunichafulia,

Mtu akinipigia, mawazo yanamjia,

Tuliapa kwake Mola, sisi ni mwili mmoja.

Unayenikubalia, niliyojiamulia,

Nawe sasa fikiria, mtihani kuingia,

Mwisho wake nakwambia, nyote mtafurahia,

Tuliapa kwake Mola sisi ni mwili mmoja.

Kama mwili wamwachia, chochote aufanyia,

Chakula akupikia, chochote akutilia,

Simu nini wafichia, akose kuangalia,

Tuliapa kwake Mola, sisi ni mwili mmoja.

Vitu tunavibania, kwamba twavithaminia,

Sumu vinatutilia, ndugu zanguni sikia,

Wenzi watufikiria, kinyume twavitumia,

Tuliapa kwake Mola, sisi ni mwili mmoja.

Nini unachofichia, asiweze angalia,

Kisogo wageuzia, asije akasikia,

Kama kipo nakwambia, nyumba wajivurugia,

Tuliapa kwake Mola, sisi ni mwili mmoja.

Washikaji nawambia, nywila nimefungulia,

Vitu vya kunitumia, msije nivurugia,

Ya maana kusikia, hayo nitafurahia,

Tuliapa kwake Mola, sisi ni mwili mmoja.

Mwenzangu wanisikia, makufuli naachia,

Utakayoyasikia, ndiyo yanayoingia,

Picha ukiangalia, ndizo wananitumia,

Tuliapa kwake Mola, sisi ni mwili mmoja.

Simufifi kinijia, zote ataangalia,

Meseji kinitumia, wala hazitasalia,

Ndugu sijeniwangia, mchanga kunitilia,

Tuliapa kwake Mola, sisi ni mwili mmoja.

Ndoa naiheshimia, ili izidi salia,

Tuzidi kufurahia, kutoka na kuingia,

Simu isije ingia, kati kutuvurugia,

Tuliapa kwake Mola, sisi ni mwili mmoja.

Mtunzi wa shairi Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments