WAKILI MAKANYA : KAZI YA MABARAZA YA ARDHI NI KUSULUHISHA NA SIO KUTOA HUKUMU
Na Gustaphu Haule, Pwani
WAKILI wa Serikali wa Halmashauri ya Wilaya Kibaha iliyopo mkoani Pwani Yasmin Makanya amewataka wananchi wa Kijiji wa Lukenge Kata ya Magindu kulitumia baraza la ardhi la Kata kama sehemu ya usuluhishi na hupatanishi.
Makanya amesema kuwa mabaraza ya ardhi ya Kata hayana mamlaka ya kisheria ya kutoa hukumu juu ya migogoro ya ardhi na kwamba baraza lolote linalofanya hivyo ni kosa kisheria.
Makanya ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho katika mkutano maalum wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia inayoendelea kufanyika katika Vitongoji, Vijiji na Kata za Halmashauri hiyo.
Wakili wa Serikali wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Yasmin Makanya akitoa elimu ya Sheria kwa Wananchi wa Kijiji cha Lukenge Kata ya Magindu leo Machi 2,ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia iliyoanza kufanyika Februari 25 hadi Machi 5,2025
Amesema awali mabaraza hayo yalikuwa na mamlaka ya kusikiliza na kutoa hukumu dhidi ya migogoro ya ardhi lakini Disemba 2021 yalifanyika mabadiliko na kwamba kwa sasa hayatakiwa tena kutoa hukumu ya migogoro ya ardhi.
Amesema hapo awali ilibainika kuwa mabaraza hayo yalikuwa yanatoa hukumu ya upendeleo na hivyo kusababisha kuzuka kwa malalamiko kiasi ambacho kilipelekea kuwepo kwa migogoro isiyomalizika na hivyo kujenga chuki baina ya Wananchi na wajumbe wa mabaraza hayo.
"Kuanza sasa nendeni kamati ya ardhi ya Kijiji au baraza la Kata kwa kusuluhishwa na sio kwa ajili ya hukumu kwani mabaraza hayo hayana mamlaka tena ya kutoa hukumu ya migogoro ya ardhi na kama kuna baraza linafanya hivyo basi ni kosa na wajumbe wake wanatakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria,"amesema Makanya.
Amesema kuwa yeyote ambaye atapata hukumu atoe taarifa kwa mkurugenzi na mkurugenzi ataitisha baraza hilo na kufuta hukumu hiyo na kisha kesi hiyo kuanza kusikilizwa tena kwa mujibu wa Sheria kwakuwa Rais Samia anataka kuona Wananchi wake wanatendewa haki.
Wananchi wa Kijiji cha Lukenge Kata ya Magindu wakiwa kwenye mkutano wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia uliofanyika leo Machi 2 Kijijini humo
Pamoja na mambo mengine Makanya katika mkutano huo mbali na kutoa elimu ya sheria katika masuala ya ardhi pia aliwaelekeza wanakijiji hao juu ya masuala ya wosia,taraka , ndoa na miradi.
Awali kabla ya Makanya na timu ya wataalam wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama kuingia katika Kijiji cha Lukenge walipita kutoa elimu hiyo katika makanisa mbalimbali likiwemo kanisa Katoliki la Kigango cha Magindu,
Akiwa kanisani humo, Makanya amewaeleza waumini hao kuwa wamefika kanisani humo kwa ajili ya kutoa ujumbe wa msaada wa kisheria kazi ambayo wanaifanya kwa niaba ya Rais wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Afisa ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Neema Yohannes akifafanua jambo katika mkutano na Wananchi wa Kijiji cha Lukenge Kata Magindu ikiwa ni sehemu ya kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia.
"Ndugu waumini wa kanisa hili la Kigango cha Magindu,sisi tumekuja hapa tukiwa timu ya wataalam wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ambapo kazi yetu kubwa ni kuwaelimisha kuhusiana na mambo mbalimbali ikiwemo masuala ya migogoro ardhi na namna ya kutatua,ndoa,miradhi,wosia,taraka na hata ukatili,"amesema Makanya.
Katekista wa Kanisa hilo Altho Mbiro,amemshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwatuma wataalam hao kwa ajili ya kuelimisha jamii na wananchi kiujumla kwakuwa wapo Wananchi wanapoteza haki zao kwakuwa hawana uelewa wa kisheria.
Mbiro amesema ujio wao Kijijini hapo inakuwa msaada kwa Wananchi kwani wanapata pa kuanzia kwani wapo watu ambao wanatumia ubabe kunyang'anya Mali za Wananchi jambo ambalo ni kinyume na mipango ya mwenyezi Mungu.
,"Binafsi niseme mama Samia kafanya mambo mengi mazuri kwa kipindi kifupi cha uongozi wake ,yaani hili jambo la kuwaleta wataalam wa sheria hakika amejitahidi sana na inatakiwa mambo kama haya muhimu yawe yanakuja mara kwa mara Kwa ajili ya kuwasaidia Wananchi ,"amesema Mbiro.
Nae Ramadhani Ally wa Kijiji cha Lukenge, amemshukuru Rais Samia kwa kuanzisha kampeni huku akiomba Halmashauri ya Wilaya Kibaha kufanya uchunguzi na utafiti juu ya migogoro ya wakulima na wafugaji na kisha kuja na suluhisho la migogoro hiyo.
Post a Comment