WANAKIJIJI WAIOMBA SERIKALI KUTAFUTA NJIA YA KUDUMU KUONDOA CHANGAMOTO MIGOGORO YA ARDHI
Na Gustaphu Haule, Pwani
WANANCHI wa Kijiji cha MwembeNgozi ,Kimaramisare na Dutumi vilivyopo Kata ya Dutumi katika Halmashauri ya Wilaya Kibaha wameiomba Serikali kuhakikisha inatafuta njia ya kudumu ya kukomesha changamoto ya migogoro ardhi katika Vijiji vyao.
Wananchi hao wametoa kauli hiyo kwa wakati tofauti walipokuwa wakikutana na timu ya wataalam wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia iliyokuwa katika Vijiji hivyo leo Machi 1,2025.
Timu hiyo ikiwa katika Kijiji cha MwembeNgozi ilikutana na Wananchi waKijiji hicho ambapo wakati Wakili Amos Sura alipokuwa anaanza kutoa elimu hiyo walieleza kuwa changamoto ya Kijiji hicho ni migogoro ya ardhi inayotokana na wakulima na wafugaji pamoja na Wawekezaji mbalimbali.
Wakili Amos Sura akitoa elimu katika kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia katika mkutano uliofanyika leo Machi 1,2025 katika Kijiji cha MwembeNgozi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani.
Wamesema kuwa endapo watasaidiwa kupata muarobaini dhidi ya utatuzi wa migogoro ya ardhi katika Kijiji chao ni wazi kuwa wataishi kwa amani na utulivu na hivyo kupata fursa ya kufanya shughuli za kilimo na nyingine za maendeleo bila hofu.
Ramadan Kondo, Mwanakijiji wa MwembeNgozi amesema amekuwa akiishi katika Kijiji hicho tangu miaka ya 1974 na ardhi waliyonayo walipewa na Kijiji na kukabidhiwa hati za kimila lakini anashangaa kuona leo hii zinakuja taasisi mbalimbali na kusema eneo la Kijijik hicho ni lao.
"Ardhi ya Kijiji chetu imetolewa kwa mwekezaji mwaka 2017 lakini chakushangaza wanakuja watu wa Housing wanasema eneo hilo ni la kwao na wanahati ya Mwaka 1937 sasa je,kuna uwezekano wa hati kutolewa juu ya hati,?ameuliza Kondo
Nae Rehema Mvugalo,Mwanakijiji wa Dutumi amesema kuwa wamekuwa wakipata shida na suala la migogoro ya ardhi katika Kijiji chao huku akiomba Serikali kutafuta njia muafaka wa kutatua migogoro hiyo.
Rehema Mvugalo aliyesimama kushoto akipata maelezo kutoka kwa wataalam wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia leo katika Kijiji cha Dutumi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha
Mvugalo amesema kuwa changamoto hiyo inakuwa kubwa kutokana na wakulima na wafugaji kuingiliana katika maeneo yao lakini kama kutakuwa na njia mbadala ni wazi kuwa migogoro hiyo itakwisha na shughuli nyingine zinaendelea.
Mvugalo amesema kwasasa ameanza kuona mwanga kwakuwa timu ya wataalam wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia wanatoa muelekeo wa namna ya kutatua migogoro ya ardhi katika Kijiji chao.
"Kwanza lazima nimpongeze Rais Dkt.Samia kwakutukumbuka sisi wanyonge huku Vijijini lakini naomba hawa wataalam wa Sheria wawe wanakuja mara kwa mara ili kusudi matatizo yetu yaweze kutatuliwa,"amesema Mvugalo .
Mratibu wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Wakili Egidy Mkolwe,amesema kuwa amebaini changamoto ya migogoro ya ardhi Kibaha Vijijini ni kubwa hivyo lazima ifanyiwe kazi ili kunusuru wanaKijiji hao.
"Tangu kuanza kwa kampeni hii nimebaini changamoto ya migogoro ya ardhi baina ya Wananchi na Wawekezaji,wakulima na wafugaji ni kubwa hivyo sisi kama Wanasheria tutaona namna ya kuishauri Serikali namna ya kufanya ili kukabiliana na changamoto yenu",amesema Mkolwe
Mkolwe amesema kuwa madhumuni ya kampeni hiyo na kubainisha matatizo na kuyafanyiakazi na kwamba katika kipindi kifupi cha kampeni wamebaini kuwepo kwa hali hiyo na watahakikisha katika ripoti yao migogoro ya ardhi inapewa kipaumbele ili ifanyiwe kazi kikamilifu.
Mwananchi wa Kijiji cha MwembeNgozi Rashid Mbegu akizungumza katika mkutano wa Kampeni wa mama Samia
Amesema miongoni mwa mambo ambayo watashauri ni pamoja na kuhakikisha Serikali inatenga vitalu vya kufugia mifugo pamoja na wagugaji kupelekwa katika maeneo ya karibu ambayo yatakuwa na malisho ya kutosha.
Awali Wakili kutoka chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Amos Sura,amewaeleza Wananchi hao namna ya hatua za kuchukua wanapotaka kumiliki ardhi lakini pia namna ya kutatua migogoro ya ardhi katika Vijiji vyao.
Hatahivyo, pamoja na mambo mengi Sura katika mikutano yake alitoa elimu mbalimbali ikiwemo elimu kuhusu ardhi,ndoa, wosia,mirathi,taraka na utawala bora huku akisema anamshukuru mama Samia kwa namna alivyojitoa kusaidia Wananchi wake.
Post a Comment