WANAFUNZI 267, WALIMU WAPATA ELIMU YA MSAADA WA KISHERIA
>>Ni katika kampeni ya mama Samia ya msaada wa kisheria inayoendelea kutolewa wilayani Kibaha
Na Gustaphu Haule, Pwani
WANAFUNZI 267 na walimu 10 wa Shule ya Sekondari Milalazi iliyopo Kata ya Gwata katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani wamenufaika na kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia iliyofika shuleni hapo kupitia timu ya wataalam wa kampeni hiyo.
Kampeni hiyo imeendelea kufanyika katika Kata mbalimbali za Halmashauri hiyo ambapo Machi 3, wataalam wa Kampeni hiyo walitembelea Shule ya Sekondari Milalazi kwa ajili ya kukutana na wanafunzi wa Shule hiyo pamoja na walimu wao.
Timu hiyo ikiwa shuleni hapo chini ya Mratibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Egidy Mkolwe wanafunzi hao walipata wasaa wa kuelimishwa mambo mbalimbali ikiwemo haki na Wajibu,ukatili dhidi ya watoto, ukatili wa Kingono, ukatili wa kisaikolojia pamoja na ukatili wa kiuchumi.
Mratibu wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Egidy Mkolwe akitoa elimu ya msaada wa kisheria kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Milalazi iliyopo Kata ya Gwata ,timu ya wataalam wa Kampeni hiyo walitembelea Shuleni hapo Machi 3,2025
Mada hizo zilifundishwa na mratibu Egidy Mkolwe ambaye pia ni Wakili wa Serikali anayefanyakazi katika ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambapo katika mada hizo aliwasisitiza wanafunzi hao kujiepusha na viashiria vya kingono vinavyofanywa na baadhi ya Jamii.
Mkolwe amesema watu baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiwarubuni wanafunzi kwa kuwapa vizawadi,rifti za bodaboda ili kusudi mwisho wa siku wafanye nao mapenzi jambo ambalo Wakili hiyo alilipinga na hivyo kuwataka wanafunzi hao kukaa mbali na watu wenye tabia hizo
Amesema kuwa madhara ya mwanafunzi kuingia katika mapenzi ni makubwa kwani wanaweza kupata magonjwa ikiwemo ugonjwa wa Upungufu wa Kinga Mwilini (Ukimwi) na magonjwa mengine ya zinaa na hivyo kukatisha ndoto zao za maisha.
"Ni marufuku mwanafunzi chini ya umri wa miaka 18 kufanya mapenzi na ukiona kuna mtu anakufanyia ishara mbaya za kutaka kukushawishi kwa kitu chochote mtu huyo ni mbaya na unapaswa kumkimbia haraka na ikiwezekana fikisha taarifa katika mamlaka ili hatua zichukuliwe,'' amesema Mkolwe .
Mkolwe ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amebaini changamoto zinazowakumba wanafunzi hao ndio maana akaamua kuwatumia wataalam hao ili waende mashuleni,na hata katika jamii kutoa elimu ya msaada wa kisheria ili kuwakomboa Wananchi wake.
Kutokana na hali hiyo Mkolwe amependekeza kuwa elimu ya sheria hiwe sehemu ya masomo yanayofundishwa katika Shule zote Nchini ili kusudi kila mwanafunzi aweze kuelewa mapema na hivyo kupata fursa ya kujilinda na kuweza kutimiza ndoto zao.
Mwakilishi wa wanafunzi wa shule hiyo ambaye pia ni dada mkuu Rehema Shaban wa kidato cha tatu amesema kuwa elimu hiyo imewasaidia kujua haki za mtoto na masuala ya ukatili wa kijinsia huku akitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia.
Wanafunzi wa shule ya Sekondari Milalazi wakimsikiliza kwa makini Mratibu wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Egidy Mkolwe katika mkutano uliofanyika Machi 3, Shuleni hapo.
"Sisi tunamshukuru Rais Samia kwa kutuletea wataalam hawa wa Sheria maana wametufundisha mambo mengi ambayo tulikuwa hatuyajui lakini kwasasa tumejua haki za mtoto na namna ya kujilinda sisi wenyewe katika viashiria mbalimbali vibaya,"amesema Shaban .
Nae Mkuu wa Shule hiyo Josephu Meli, amesema kuwa,amepokea kwa furaha program hiyo ya Mama Samia kwani inawasaidia wanafunzi na jamii kiujumla kuelewa mambo mbalimbali ya kisheria.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Milalazi iliyopo Kata ya Gwata katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Josephu Meli akizungumza katika mkutano wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia uliofanyika shuleni hapo Machi 3 chini ya Mratibu wa kampeni hiyo Egidy Mkolwe.
Post a Comment