HEADER AD

HEADER AD

TANROADS YAMALIZA MGOGORO WA WANANCHI WALIOPITIWA NA MRADI WA UJENZI WA BARABARA

>>Ni waliokuwa wanadai fidia mkoani Pwani

>>TANROADS yapokea Bilioni 6.6 


Na Gustaphu Haule ,Pwani

MGOGORO wa madai ya fidia kwa Wananchi wanaopitiwa mradi wa ujenzi wa barabara ya TAMCO-Mapinga kwa kiwango cha lami kwasasa umemalizika baada ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Pwani kupokea jumla ya Tsh. Bilioni 6.6.

Meneja wa TANROADS mkoa wa Pwani Baraka Mwambage ,ametoa taarifa hiyo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa robo tatu ya mwaka 2024/ 2025 katika kikao cha bodi ya barabara kilichofanyika Machi 4 mjini Kibaha.

   Meneja wa TANROADS mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage akiwasilisha mada ya utekelezaji wa shughuli zake katika kikao cha Bodi ya Barabara ya MKoa wa Pwani kilichofanyika Machi 4 Mjini Kibaha.

Barabara hiyo inayounganisha Halmashauri ya Mji Kibaha na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo  kwasasa ulipwaji wa fidia hizo upo hatua za mwisho na kwamba wananchi wanaendelea kulipwa.

Amesema katika ulipaji huo kuna changamoto ya vitambulisho na vitu vingine vidogovidogo lakini hata hivyo haijazuia utekelezaji wake kwakuwa zoezi hilo linaendelea vizuri.

Amesema kwasasa hakuna mgogoro tena katika eneo la ujenzi wa barabara kwani tangu Machi 3 mwaka huu tayari wamemkabidhi mkandarasi Kilomita zote 12 zilizobaki na sasa ni yeye na kazi.

Mwambage amesema kuwa mradi wa TAMCO- Mapinga ni moja ya miradi ya kimkakati ya mkoa wa Pwani ambapo kukamilika kwake utakuwa na umuhimu mkubwa kwakuwa utaunganisha mkoa wa Pwani na hivyo kufungua fursa za kiuchumi kwa Wananchi.

Kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara ya mwendo wa haraka(Express Way) kutoka Kibaha -Chalinze-Morogoro amesema mradi huo upo katika hatua za manunuzi na kwamba hivi sasa wanafanya majadiliano ya mwisho kati ya Serikali na mwekezaji.

" Kuhusu barabara ya Makofia -Mlandizi -Maneromango Mwambage, mpaka sasa wanaendelea kukamilisha taarifa za ulipwaji fidia na mara zitakapokamilika zitatolewa taarifa" amesema Meneja.

Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) mkoa wa Pwani Leopold Runji, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya robo tatu ya Mwaka 2024/2025 ameutaja mradi wa Tactic kuwa mradi huo utakwenda kuubadilisha Mji wa Kibaha.

     Meneja Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Mhandisi Leopold Runji akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya robo tatu ya Mwaka wa fedha 2024/2025 katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Pwani kilichofanyika Machi 4 Mjini Kibaha.

Runji amesema kuwa kupitia mradi huo Kibaha mjini imefanikiwa kupata barabara zaidi ya Kilomita 17 ambazo zitajengwa kwa awamu mbili tofauti.

Amesema awamu ya kwanza itajengwa barabara ya Tughe mpaka kuunganisha Ikulu ndogo anapoishi Mkuu wa mkoa wa Pwani yenye Kilomita 3.7 na tayari wametangaza huku awamu ya pili zitajengwa Kilomita 13 katika maeneo ya Kata ya Mailimoja na Kata ya Tangini.

Wakichangia mada katika kikao hicho baadhi ya wajumbe akiwemo mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti, amekiomba kikao hicho kuangalia namna ya kujenga barabara za lami katika Wilaya hiyo kwani mpaka sasa inakilomita Saba pekee huku zikiwa na mashimo mengi.

       Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti akichangia mada katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Pwani kilichofanyika Machi 4 Mjini Kibaha.

Magoti pamoja na changamoto hizo amempongeza Meneja wa TANROADS mkoa wa Pwani pamoja na Meneja wa TARURA mkoa wa Pwani kwa juhudi na kazi kubwa wanazozifanya katika kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote.

Nae Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Michael Mwakamo,amempongeza Meneja wa TANROADS mkoa wa Pwani pamoja na Meneja wa TARURA kwakuwa barabara nyingi utekelezaji wake umeanza huku akiomba kuhakikisha wanazifanyiakazi barabara zenye kipaumbele kwa wananchi wakizingatia kuwa mwaka huu wa uchaguzi.

Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, ametaka kufanya tathmini wa yale walioyaahidi kufanya na kujua mangapi yamefanyika na kisha kuyapa kipaumbele kulingana na wakati uliopo.

       Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Pwani kilichofanyika Machi 4 Mjini Kibaha.

Hatahivyo, Kunenge amewataka wajumbe kutafuta ufumbuzi wa changamoto na sio kulalamika huku akisema lazima wajifunze kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye hana muda wa kupumzika hivyo lazima watendaji wafanyekazi zaidi yake.


No comments