HEADER AD

HEADER AD

WANANCHI KIJIJI CHA IYOGELO MASWA WADAI FIDIA UJENZI WA BWAWA

Na Samwel Mwanga, Maswa

WANANCHI katika kijiji cha Iyogelo katika Kata ya Binza wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu wameilalamikia serikali kwa kuweka mradi wa bwawa la maji katika maeneo yao bila kulipwa fidia.

Wakizungumza leo jumanne Machi 25,2025 katika kijiji hicho katika kitongoji cha Bugarama wamesema wanachohitaji ni kulipwa fidia vinginevyo watakwenda mahakamani kuzuia ujenzi huo kuendelea.

Gwita Hinda mkazi wa kijiji cha Iyogelo amesema kuwa Baba yake mzazi,Jilala Hinda ambaye kwa sasa ni marehemu alitoa eneo lake la hekari 30  kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo kwa masharti ya kulipwa fidia lakini hadi sasa hajalipwa.

      Ngwita  Hinda mkazi wa kijiji cha Iyogelo wilaya ya Maswa akilalamikia eneo lake la hekari 30 kuchukuliwa na serikali bila kulipwa fidia.

“Mzee wakati wa uhai alitoa eneo la kuchimbwa bwawa baada ya kuombwa na uongozi wa Kata ya Binza lakini kwa masharti kuwa watamlipa fidia baada ya kufanyika tathimini lakini hadi sasa hakuna fidia iliyolipwa na ujenzi umekwisha kuanza,”

“Nilipoanza kufuatilia nikiwa mtoto mkubwa wa familia nikaelezwa  kuwa eneo lilitolewa bure jambo ambalo si kweli tumeomba tupatiwe maandishi ya makubaliano hayo hadi sasa hatujafanikiwa,ila nikuhakikishie hayapo,”amesema.

Gwisu Jilala mkazi wa kijiji cha Iyogelo anasema kuwa eneo lake lenye ukubwa wa hekari 4 ambalo ni shamba alikuwa akilima mazao mbalimbali ya chakula ambayo ni mahindi na mtama limeanza kuchimbwa udongo kwa ajili ya ujenzi wa tuta.

        Gwisu Jilala mkazi wa kijiji cha Iyogelo wilaya ya Maswa akilalamikia eneo lake la hekari 4 kuchukuliwa na serikali bila kulipwa fidia.

“Mie nilifika kwenye eneo langu nikakuta mitambo ya ujenzi ikichimba udongo kwenye shamba langu nilipohoji nikaelezwa kuwa wameupenda udongo wa eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa tuta la bwawa,huu ni uvamizi,”amesema.

Naye Lwenge Malale mkazi wa kijiji hicho anasema kuwa mwezi Machi 12,2025 aliona makatapila yakichimba udongo kwenye eneo lake lenye ukubwa wa hekari 12 bila ya kuwepo kwa makubaliano yoyote.

“Binafsi napenda masuala ya maendeleo lakini hiki kinachofanyika cha kuvamia eneo langu na kuanza kuchimba bwawa,kitendo hiki hakikubaliki ni vizuri wakanilipa fidia maana hata nyumba yangu imo ndani ya mita 60 kutoka bwawa linapojengwa hapo siwezi kuishi tena,”amesema.

Mahona Mathias mkazi wa kijiji cha Iyogelo anasema kuwa eneo lake lenye ukubwa wa hekari 6 limechukuliwa kwa ujenzi wa bwawa hilo bila makubaliano ya aina yoyote.

     Mahona Mathias mkazi wa kijiji cha Iyogelo wilaya ya Maswa akilalamikia eneo lake la hekari 6 kuchukuliwa na serikali bila kulipwa fidia.

Mwenyekiti wa kitongoji wa Bugarama,Jackson Madata akizungumzia malalamiko hayo amesema kuwa ni vizuri serikali ya wilaya kwa kushirikiana na uongozi wa wizara ya maji kupitia bonde la ziwa Victoria wakutane kwa ajili ya kutatua mgogoro huo.

“Ni kweli hata mie malalamiko ya wananchi hao yamefika kwangu,hili jambo ili liweze kumalizika ni vizuri uongozi wa serikali wa wilaya pamoja na bonde la ziwa Victoria wakakutana na wahanga kwa lengo la kutatua mgogoro uliopo,”amesema.

Mkurugenzi wa Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria,Dkt Renatus Shinhu amesema kuwa kabla ya kuanza kwa ujenzi huo walihakikishiwa na uongozi wa serikali ya kijiji cha Iyogelo kuwa halina mgogoro na ndipo wakaanza ujenzi lakini ameshangaa kupata malalamiko ya wananchi kuvamiwa maeneo yao.

Amesema kuwa iwapo itabainika ya kuwa wananchi hao madai yao yana msingi itabidi wafanye tathimini ili waweze kulipa fidia.

“Sisi tunajenga mabwawa katika maeneo ambayo hayana migogoro,ni kweli nimeelezwa malalamiko ya wananchi hao ila nachokiomba s t hughuli ya ujenzi iendelee na sisi tutakutana nao kwa dharula ili uone malalamiko yao iwapo watastahili fidia tutawalipa,”amesema.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Maswa,Athuman Kalaghe amekiri kupokea malalamiko hayo na kueleza amepanga kuwakutanisha wananchi hao na serikali ya kijiji,uongozi wa bonde la ziwa Victoria pamoja na Kamati inayoshughulikia migogoro wilayani humo inayoongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo.

“Kweli nimekutana na wananchi hao wenye malalamiko na tumekubaliana ya kuwa Machi 27,2025 tutakuwa na kikao cha pamoja ili kuyapatia ufumbuzi malalamiko ya wananchi wetu,”amesema.

        Sehemu ya eneo linalochimwa bwawa katika kijiji cha Iyogelo wilaya ya Maswa ambapo wenye maeneo wanalamikia kutolipwa fidia.

 

No comments