WAZAZI, WASICHANA AMBAO HAWAJARIPOTI KIDATO CHA KWANZA WAKAMATWA
>>Ni katika msako unaoendeshwa Kata ya Matongo- Nyamongo kuwakamata ambao hawajaripoti shule
>>Polisi wawapelela kituoni
>> Wengine ni wajawazito , waliosuka nywele wanyolewa
Na Dinna Maningo, Tarime
WASICHANA wapatao 14 kutoka katika vijijini vya Kata ya Matongo- Nyamongo, wilaya ya Tarime mkoa wa Mara waliofaulu kuanza kidato cha kwanza mwaka 2025 lakini hawajaripoti shuleni wakiwa na wazazi wao wamekamatwa na kupelekwa kituo cha polisi Nyamongo.
DIMA ONLINE Machi, 06, 2025 ikiwa katika ofisi ya Kata ya Matongo majira ya saa tano asubuhi , imeshuhudia kuona wazazi jinsi ya kike na kiume wakiingizwa kwenye gari la Polisi na kisha polisi kuondoka nao.
DIMA ONLINE ikiwa katika ofisi hiyo imeshuhudia wasichana wapatao 14 wakiwa wameketi chini wakihojiwa na Mratibu elimu Kata hiyo, Mtendaji wa kijiji cha mjini kati na mtendaji wa Kata ya Matongo sababu za kutoripoti shule huku baadhi ya wazazi wengine wa wanafunzi hao wakiwa wameketi wakiwatazamana watoto wao.
Kati ya wasichana hao , wasichana wawili ni wajawazito huku wasichana wengine vichwani mwao wakiwa wamesuka nywele ukiwemo mtindo wa rasta.
Wanafunzi waliosuka nywele waliweza kunyolewa nywele zao na afisa elimu Kata ya Matongo, Alex Kayobo kutokana na kwamaba ni kosa kwa wanafunzi kusuka nywele.
Afisa elimu Kata ya Matongo- Nyamongo Alex Kayobo akiwanyoa nywele wanafunzi waliofaulu na kutoripoti shuleni ambao wamesuka nywele.
Mwandishi wa chombo hiki cha habari amezungumza na baadhi ya wazazi ambapo mzazi mmoja amesema kwamba anaishi na mjukuu wake na alikosa fedha za maandalizi ya mwanafunzi .
" Mimi ni mjane , huyo mtoto ni mjukuu wa binti yangu , nimemlea akiwa mdogo baba yake alifariki. Nilikosa fedha za kununua makauntabuku na mahitaji mengine maana shule iliandika mahitaji mengi kwenye fomu nikakosa uwezo wa kununua" amesema.
Licha ya baadhi ya wazazi kudai ugumu wa maisha umesababisha washindwe kumudu gharama za mahitaji ya shule lakini kwa muonekana wa mavazi yao waliyokuwa wameyavaa inaonesha si watu wa kuweza kushindwa kumudu gharama za mahitaji ya shule zikiwemo sare na madaftari.
Wasichana wengine wakati wanahojiwa wameonekana kutohitaji kuendelea na masomo , hivyo huwenda wengine wakawa tayari kuendelea na masomo na wengine huwenda wakakwamia njiani na kutohitimu shule.
Afisa elimu Kata ya Matongo- Nyamongo Alex Kayobo akiwanyoa nywele wanafunzi waliofaulu na kutoripoti shuleni ambao wamesuka nywele
Hata hivyo, baada ya dakika kadhaa kupita gari la Polisi lilirejea ofisini hapo na kuwapakia wasichana hao na wazazi wao ndani ya gari la Polisi na kisha kuondoka nao kwenda kituo cha Polisi huku wakiongozana na afisa elimu Kata.
Bhoke Marwa mkazi wa Kijiji cha Nyangoto ameupongeza uongozi wa kata kwa kufanya masako huo kwa kile alichoeleza kwamba wazazi ni sehemu ya kuchangia watoto kutokwenda shuleni.
" Hivi mzazi unawezaje kusema kwamba mwanao umemwambia aende shuleni amekataa? mtoto umzae mwenyewe alafu akuendeshe! huu ni uzembe kabisa wa wazazi.
" Ni mzazi gani ambaye mwanae amekataa kwenda shule akaenda kuripoti katika mamalaka za serikali?mtoto anakataa shule na wewe unakubali maana yake nyote mmekubalina" amesema Bhoke.
Joseph Mwita mkazi wa Kijiji cha Matongo amesema" Serikali imefanya la maana kuwakamata wazazi maana hawa wazazi wanachangia watoto kutokwenda shule kwasababu ya kutaka mahari na kusaidiwa kazi za nyumbani.
" Mtoto mwenye nia na masomo hata kama uwezo wake ni mdogo darasani hawezi kuchukua masomo , bado atasoma na atahitimu shule lakini sio mtoto ukatae masomo kwamba masomo ya Sekondari ni magumu.
" Tunaomba serikali iendelee kuwasaka iwakamate na iwachukulue hatua kali maana mtoto akisoma hasa wa kike unamsaidia kutojiingiza kwenye ndoa za umri mdogo ,akikaa nyumbani bila kwenda shule anashawishika kuolewa" amesema Joseph.
Wiki chache zilizopita mkuu wa wilaya ya Tarime Meja , Edward Gowele akiwa anazunguza na wananchi Nyamongo alihimiza wazazi kuwapeleka wanafunzi shule na kwamba wazazi ambao watoto wao hawajaripoti shule watawajibishwa.
Pia Machi, 05, 2025 , mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi aliwaagiza wakuu wa wilaya zote kuhakikisha wanawatafuta wanafunzi ambao hawajaripoti shule.
RC Mtambi alitoa agizo hilo wakati akifungua kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) kilichofanyika kwenye ukumbi wa uwekezaji ofisi ya mkoa wa Mara.
RC Mtambi alisema kwamba wanafunzi walioripoti kidato cha kwanza hadi sasa wamefika asilimia 82.3 huku akiwataka wakuu wa wilaya zote kuongeza kasi ya ufuatiliaji na kuhakikisha wanafafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2025 wanaripoti shule.
" Uandikishaji wa shule za awali ulifikia asilimia 99.61, huku uandikishaji shule za msingi ukivuka lengo na kufikia asilimia 107. Wanafunzi walioripoti hadi sasa kidato cha kwanza ni asilimia 82.3 hapa hatufanyi vizuri.
" Nawaagiza wakuu wa wilaya zote kuongeza kasi ya ufuatiliaji. Endesheni operesheni maalum kuwatafuta wanafunzi hao. Zipo taarifa kwamba kuna baadhi wameanza kujishughulisha na shughuli za nyumbani na wengine wameenda nchi jirani, na kuna taarifa wengine wameolewa na wengine wazazi wameamua kuwaacha nyumbani ili kufanya shughuli" amesema Meja Evans.
RC huyo alisema kwamba mzazi anayemkosesha mtoto haki ya elimu hawatamuacha watashughulika nae.
Post a Comment