HEADER AD

HEADER AD

KUFA NA TAI SHINGONI

ILI tusife haraka, maumivu yatushika,

Bora kufanya haraka, ya moyoni kututoka,
Kwa washauri kufika, ya kwetu kuyaanika,
Kufa na tai shingoni, twaweza kukuepuka.

Jambo gumu lakufika, kufanya kuhangaika,
Hadi moyo waumuka, na fikira zinachoka,
Kwa mtu lisipotoka, mwisho waweza pasuka,
Kufa na tai shingoni, twaweza kukuepuka.

Yaweza kufikirika, lako gumu kubebeka,
Kama vile lakufika, tangu nchi kuumbika,
Kumbe kama likisika, ni dogo la kubebeka,
Kufa na tai shingoni, twaweza kukuepuka.

Gonjwa la moyo kufika, shinikizo panda shuka,
Ni hayo umeyashika, moyo unashughulika,
Hadi pale inafika, yanashindwa vumilika,
Kufa na tai shingoni, twaweza kukuepuka.

Wanaume yasikika, wengi vifo huwashika,
Sababu yakiwafika, wabaki wasononeka,
Kwa wenza kuyaanika, aibu zinawashika,
Kufa na tai shingoni, twaweza kukuepuka.

Hili likieleweka, Kufichaficha kuchoka,
Pazuri tutapafika, shida nyingi kuondoka,
Mauti kufikafika, kwaweza sahaulika,
Kufa na tai shingoni, twaweza kukuepuka.

Wanawake twawacheka, kusema bila kuchoka,
Kumbe nyingi takataka, ambazo zinawafika,
Ndivyo zinahamishika, zisije zikawabaka,
Kufa na tai shingoni, twaweza kukuepuka.

Moyo mdogo hakika, amani yahitajika,
Mizigo ya kubebeka, kubeba yaleta shaka,
Kama haujapasuka, nyufa zaweza jengeka,
Kufa na tai shingoni, twaweza kukuepuka.

Kaka na dada amka, haya upate kushika,
Afya ni kutajirika, magonjwa kufukarika,
Yale ya kuepukika, bora yasijetushika,
Kufa na tai shingoni, twaweza kukuepuka.

Shairi limetungwa na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

No comments