CCM SIMIYU YAKERWA KUSUASUA UJENZI WA VETA BUSEGA
Na Samwel Mwanga, Simiyu
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Simiyu kimeeleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa Chuo cha ufundi Stadi (VETA) kinachojengwa katika wilaya ya Busega kwa gharama ya Tsh Bilioni 1.48 kwa awamu ya kwanza.
Hayo yameelezwa na Katibu wa CCM mkoa huo, Eva Ndegeleka Aprili , 8, 2025 akiwa ameongozana na wajumbe wa kamati ya siasa ya chama hicho ya mkoa wa Simiyu kukagua ujenzi wa chuo hicho amesema kuwa ujenzi unasuasua.
Amesema ujenzi wa chuo hicho ni muhimu kwa ajili ya vijana ambao watajifunza utaalamu na ujuzi mbalimbali ili waweze kujikimu kwa ajili ya maisha yao.
“Serikali imetoa fedha kupitia wizara ya elimu, sayansi na teknolojia,lakini maendeleo ya ujenzi wa chuo hiki unasuasua, hali ambayo inatia mashaka juu ya usimamizi na utekelezaji wake,”amesema.
Amemtaka mkuu wa mkoa huo,Kenani Kihongosi kushirikiana na chama hicho ili waweze kuwasiliana na wizara hiyo kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi huo ifikapo mwezi juni mwaka huu.
Naye mkuu wa mkoa huo ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo, amesema kuwa ni muhimu kwa wahusika kuongeza kasi ili kuhakikisha kuwa ujenzi huo unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa mafunzo kwa vijana wa wilaya hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenan Kihongosi (mwenye kofia rangi nyekundu) akisoma taarifa ya ujenzi wa Chuo cha VETA wilaya ya Busega.
Amesema kuwa ujenzi huo una changamoto kubwa katika utekelezaji wake, licha ya ofisi ya mkuu wa wilaya ya Busega pamoja na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwakumbusha kwa maandishi juu ya utekelezaji wake na umuhimu wa mradi huo lakini bado kuna shida kidogo.
"Wizara wanapoleta hii miradi, wajue kuna viongozi kama mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa halmashauri kwenye eneo husika wanaopaswa kujua utekelezaji wake ili waguswe zaidi na miradi hii, kwa sababu, hapa leo tunaulizana gharama ya jengo, hakuna anayejua zaidi ya wizara.
''Hii ni changamoto, kama fedha zimeletwa zaidi ya Tsh Milioni 429 lakini bado majengo hayajakamilika, wizara ya elimu wana wajibu wa kufanya, hapa, sisi kama mkoa hatujaridhika na huu mradi." Amesema.
Amesema kuwa changamoto zote zilizojitokeza ikiwemo nondo kuoza, zinaweza kusababisha majengo kubomoka na kuitaka wizara hiyo kuhakikisha wanasaidia ujenzi wa chuo hicho unakamilika kwa wakati kwani tayari serikali imeshatoa fedha.
Afisa Uthibiti Ubora wa shule wilaya ya Busega, William Thomas akitoa taarifa ya ujenzi huo amesema kuwa lengo la mradi huo ni kupata wataalamu watakaosaidia nchi baada ya kuhitimu mafunzo ya vyuo, kuwajengea ujuzi na uwezo wa kujiajiri vijana pamoja kupunguza tatizo la ajira hapa nchini.
Afisa uthibiti ubora wa Shule wilaya ya Busega,William Thomas(kulia) akisoma taarifa ya ujenzi wa chuo cha VETA wilayani humo kwa wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM mkoa wa Simiyu.
Amesema kuwa ujenzi wa chuo hicho ukikamilika utakuwa na majengo 18 ambapo awamu ya kwanza itahusisha majengo tisa na awamu ya pili majengo tisa na hadi sasa Tsh Milioni 429 zimeshatolewa.
"Jengo la utawala limefikia asilima 50, madarasa yako asilima 50, kuna changamoto ya ukosefu wa nondo kwa ajili ya kufunga lenta, nguzo za kunyanyua majengo ya karakana na mbao hazijaletwa ili kuendelea na upauaji wa majengo sita" amesema Mtibiti ubora.
Post a Comment