HEADER AD

HEADER AD

MPASUKO WA WALIMU WAITESA SHULE YA SEKONDARI MAGOTO TARIME


>>Walimu wagawanyika makundi

>> Wazazi wamekuwa wakichanga fedha kulipa walimu wa sayansi lakini hakuna walimu

>> Mapato na matumizi miradi ya shule hayajulikani

>> Tuhuma zaelekezwa kwa mkuu wa shule

Na Dinna Maningo, Tarime

HALI si shwari katika shule ya sekondari Magoto iliyopo kata ya Nyakonga, wilaya ya Tarime mkoani Mara, kufuatia kuwepo kwa makundi ya walimu ndani ya shule na kusababisha mpasuko jambo ambalo linaweza kushusha taaluma ya shule.

Shule ya sekondari Magoto ni ya bweni kwa kidato cha tano na sita, na kutwa kwa kidato cha kwanza hadi kidato cha nne, iliyopo halmashauri ya wilaya ya Tarime.  

        Moja ya jengo shule ya sekondari Magoto, wilayani Tarime

Januari , 13, 2025 mkuu wa wilaya ya Tarime , Edward Gowele akiwa katika ziara yake Kijiji cha Magoto, alizungumza na wananchi ambapo alielezwa kero mbalimbali zikiwemo za shule ya sekondari Magoto.

Machi, 25, mwaka huu , mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime ambaye pia ni Diwani wa Kata hiyo, Simion Kiles akiwa katika ziara ya kutembelea miradi alifanya kikao na Kamati ya siasa chama Mapinduzi (CCM) kata ya Nyakonga.

Kikao hicho kiliwakutanisha pia viongozi wa serikali za vijiji , bodi ya shule, walimu ambapo hoja mbalimbali ziliibuliwa zikiwemo changamoto shule ya sekondari Magoto.

Walimu wagawanyika makundi

Tuhuma nyingi zinaelekezwa kwa mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Magoto , Christopher Kinene Mosabi kwa kushindwa kuwaunganisha walimu ili kuwa kitu kimoja badala yake amekuwa akiwaga.

Inaelezwa kuwa walimu kwa walimu wamegawanyika makundi ambapo kuna kundi la upande wa mkuu wa shule na kundi lisilo upande wa mkuu wa shule. Inaelezwa kuwa walimu walioko upande wa mkuu wa shule wanapendelewa kwenye utoaji wa motisha. Huku walimu wasio upande wa mkuu wa shule wanaofanya kazi kwa juhudi mkuu wa shule hatambui juhudi hizo hata kuwapongeza kwa maneno.

Habari zinasema kwamba mkuu wa shule amekuwa akiwagawa walimu na wanafunzi hasa wa A-level . Walimu wanapotoa adhabu kwa wanafunzi,  miongoni mwao huishia kukimbilia ofisi ya mkuu wa shule na adhabu nyingi kutenguliwa na kama sio kutenguliwa basi adhabu kubadirishwa na mkuu.

Inaelezwa kwamba hali hiyo inachangiwa na ubinafsi wa kimaslahi wa fedha kutoka kwa wanafunzi kwani wanapopewa adhabu na walimu, mkuu wa shule hutengua adhabu na wengine kuwapa adhabu kubwa ili tu wazazi wampatie fedha ili watoto wao waendelee na masomo.

Pesa walimu wa sayansi zapigwa

Inaelezwa kuwa , wazazi wamekuwa wakichanga fedha kwa ajili ya kuwalipa walimu wa kujitolea wa masomo ya sayansi lakini shule hiyo haina walimu wa sayansi pamoja na changamoto kadha wa kadha zinazohitaji utatuzi ili kunusuru shule hiyo pamoja na walimu.

Habari zinasema kwamba kutokana na uhaba wa walimu wa sayansi wazazi kupitia kikao cha wazazi walikubaliana  kila mzazi mwenye mwanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne kutoa Tsh. 20,000 kila mwaka kwa ajili ya kulipa walimu wanne wa kujitolea kufundisha masomo ya sayansi.

Inaelezwa kwamba walimu hao wa sayansi waliokuwa wanalipwa kwa fedha za wazazi walifundisha kwa miezi kadhaa na kisha kuondoka ambapo mwalimu aliyekuwa amesalia nae ameondoka mwezi uliopita.

"Kuna mwalimu tangu aondoke mwaka umeishia, na mwingine akaondoka mwaka jana , aliyekuwepo nae ameondoka mwezi uliopita ,2025, baadhi yao wameacha kwasababu ya malipo kidogo.

" Michango ya walimu wa sayansi ni Tsh. 20,000 kwa mihula miwili kwa maana ya mwaka mmoja kwa kila mwanafunzi wa kidato cha kwanza hadi kidato cha sita. Wanafunzi wanaochanga ni 449×20,000 ni sawa na 8,980,000. Mwalimu wa sayansi ni mmoja na analipwa 150,000 kwa miezi 10 ya kazi.

" Miezi 10 × 150,000 = 1,500,000.
Kinachobaki ni 7,480,000.
Sasa tuseme kuna wanafunzi 150 hawajamalizia 10,000 ya mhula wa pili nikijua kwa mhula wa kwanza kila mwanafunzi hubanwa atoe hiyo 10,000. Hii pesa nyingine inaenda wapi na inafanya kazi zipi " anasema chanzo kimoja .

" Wazazi waliajiri walimu wa sayansi 4 na wazazi wakawa wanatoa 20,000 kwa mihula miwili lakini baada ya mwaka mmoja walimu hao waliondoka kuendelea na masomo akabaki mmoja ambaye analipwa 150,000 kila mwezi " anasema.

Anaongeza " Nikianzia mwaka jana ambapo ndo nina kumbukumbu nzuri, wanafunzi walikua zaidi ya 500 walikuwa wanalipa 20,000 kwa mwaka kila mmoja. Wakati huo mwalimu huyo wa kujitolea analipwa laki moja na elfu hamsini kila mwezi kwa miezi 10. Pesa inayobaki inafanya nini wakati huo watoto wamekua wanapigwa na kufukuzwa kufata pesa hizo?. 

Kati ya wanafunzi 440 wanachanga kwa mwaka 8,800,000 na ukitoa 1,500,000 ambayo Mwalimu aliekuwa amebaki toka mwaka juzi inabaki 7,300,000. Basi tuseme kuna wazazi 200 hawachangi na ufanye hesabu ya wazazi 200 wanaochanga unapata 4,000,000 na ukitoa 1,500,000 anayolipwa mwalimu huyo kwa mwaka inabaki 2,500,000. Hizo pesa zinafanya kazi gani au zinaenda wapi? kinauliza chanzo hicho.

Mapato, matumizi ya miradi hayajulikani

Inaelezwa kwamba, miradi ya shule kama vile mashine ya kusaga unga, mashamba, duka, saluni ya kunyoa nywele, miti ya shule imekuwa ikiendeshwa bila walimu, bodi ya shule kujua mapato na matumizi yake, hakuna ushirikishwaji wa walimu katika miradi hiyo.

               Mradi wa mashine ya kusaga unga shule ya sekondari Magoto

" Mashine ya kusaga walimu hawajui mtaji wa uendeshaji wa mashine hiyo kuanzia kwenye mtaji wa kununua  umeme, kiasi gani kimetumika kwenye huo mtaji, kilichobaki na faida iliyopatikana na matumizi yake.

"Shule ina mradi wa mashamba ya shule ya kilimo cha mazao ya mahindi na viazi ambayo yanakodishwa kwa watu. Cha ajabu tunakuja kusomewa taarifa ya mapato na matumizi ya mashamba hayo wakati haijulikani matumizi halisi ya mradi huo"  anasema mwalimu mmoja.

"Hatushirikishwi juu ya hatua zote za kabla ya kulima ili tutoe ushauri au mawazo panapowezekana na kujua mtaji uliotumika na hatua zote, wanakodisha kwa watu wengine walimu wanakosa pakulima mazao.

" Shamba la ndizi sijawahi sikia juu ya ndizi zinazouzwa ni kiasi gani na mapato yake kwenye taarifa tunazoandikiwa,  huku nikiona ndizi zinakatwa na kuuzwa sana lakini fedha haijulikani zinaenda wapi na zinafanya kazi gani" anasema.

Inaelezwa kwamba wanafunzi wanaokaa Hosteli wanalipa kwa mwaka Tsh. 600,000 lakini bodi ya shule ,walimu hawajui pesa inayoingia wala matumizi yake huku wanafunzi wa hosteli wakitumia sehemu kubwa ya chakula cha wanafunzi wa bweni wa kidato cha tano na sita wanaolishwa na serikali.

" Je, pesa ambazo wanafunzi wanaokaa hosteli zinaenda wapi na kufanya nini kama sio mradi wa mkuu maana kwa mwaka wanalipa 600,000 kila mwanafunzi anayekaa hosteli, Walimu hawajui hostel ipo kwa utaratibu upi hasa ada ya kukaa hostel, matumizi yake na faida yake " Chanzo cha habari kinasema.

Madhaifu ya utawala

Habari zinasema kwamba mkuu huyo wa shule amekuwa na utawala wa uonevu kwa kuminya uhuru wa walimu kuongea na kutoa mawazo yao na amekuwa akitumia maneno ya vitisho kwa walimu wanapokua na hoja za kushauri au kupinga jambo fulani.

Inaelezwa kuwa mkuu huyo wa shule amekuwa akijitwika mwenyewe majukumu yote ya shule huku idara ama vitengo kwenye shule hiyo vikishindwa kufanya majukumu yao .

Amekuwa asiyeshirikisha walimu na hivyo idara na vitengo vyote vya shule kukosa uhuru wa kusimamia majukumu yao na kuingiliwa na kusimamiwa na kufanywa na mkuu huyo jambo ambalo linawakatisha tamaa baadhi ya walimu kwenye idara zao na hivyo kupuuza mambo mengi yanayokuwa yanaharibika na kutotoa ushirikiano.

Pia wanafunzi kutoka mikoa ya mbali wakati mwingine wamekua wakikaa zaidi ya siku mbili hadi tatu shuleni wakimsubilia mkuu wa shule atoke mjini anakoishi aje awape vyeti vya kuhitimu elimu ya sekondari jambo ambalo linatajwa kuwa lipo kimaslahi pale wanafunzi wanapokuwa wanadaiwa wamlipe madeni hayo ili aweke fedha mfukoni mwake.

Inaelezwa kwamba ,ugawaji wa vyeti mwalimu yoyote anaweza fanya kazi hiyo ilimradi taarifa za mwanafunzi husika zipo ambazo zinakua kwenye daftari la madeni na la kusaini anapochukua cheti. 

Habari zinasema kwamba wanafunzi wamekuwa wakiteseka katika upewaji wa vyeti na wakati mwingine mkuu huyo akilazimishwa kufika shuleni kuwapa vyeti huwa anawaomba hela ya mafuta ya pikipiki yake hasa kwa wale wanaokutwa hawana madeni.

Ubaguzi kushusha taaluma

Ubaguzi wa walimu umepelekea kushuka kwa taaluma kwamba mkuu wa shule ameshindwa kusimamia na kubuni mbinu nzuri za kuweza kusaidia katika kuimalisha taaluma kwa wanafunzi.

Hali hiyo inapelekea wanafunzi hao kumzoea na kumuona mtu wa kawaida sana na kuishi maisha ya kizembe na kutokuchukulia uzito mkubwa katika kupambana na taaluma hali iliyosababisha kushuka kwa taaluma katika mtihani wa Mock kidato cha sita 2024 kwa kupata hadi daraja la Sufuri.

" Mfano, kidato cha sita wamekuwa wanapata hata divisheni 3 na 4 licha ya kwamba wanasoma taasusi za masomo ya sanaa. Mtihani wa moko wa kanda ya ziwa mwaka huu kuna daraja la sufuri. Na matokeo hayo ni kwasababu ya juhudi binafsi za walimu pamoja na kupelekwa pelekwa kama watumwa wasiokua na uhuru wa mawazo, kuzungumza, kutishiwa kuhamishwa, kutoshirikishwa mbinu ya ufanisi wa kitaaluma n.k." Chanzo kimoja kinasema.

Miti ya shule kuuzwa

Habari zinasema kwamba shule hiyo ina mzabuni anayepeleka kuni kwa ajili ya matumizi ya shule lakini miti ya shule imekuwa ikikatwa kwa ajili ya kuni na hata kuchanwa mbao na kuuzwa huku fedha kutojulikana zinakwenda wapi na kufanya kazi gani.

" Miti inakatwa sana tena kwa kipindi kirefu sana kwa ajili ya kuni huku tunajua kuna uzabuni wa kusuply kuni na wanafunzi ndio wanasomba hizo kuni kwa kutumwa na mkuu wa shule na wakati huo tunaamini kuwa bodi ya shule haina taarifa wala walimu kuwa na taarifa ya ukataji hovyo wa miti ya shule.

Inaelezwa kwamba mkuu huyo wa shule amekuwa akikata miti ya shule kwa kushirikiana mwenyekiti wa bodi ya shule, Amon Wambura na Marwa  Wambura maarufu Marwa Meneja ambaye ni ndugu wa Mwenyekiti wa bodi, kupasua mbao ambazo huuzwa kwa watu mbalimbali bila uongozi wa shule kushirikishwa . 

Idara ya Elimu kutotunza siri

Hata hivyo, idara ya elimu halmashauri ya wilaya ya Tarime na Kata ya Nyakonga zinatuhumiwa kwa kutoa siri za walimu wanaofika ofisi ya elimu kumlalamika mkuu wa shule na baadhi ya walimu, kwani wanapowalalamikia wahusika hushangaa taarifa hizo zinawafikia na hivyo kuwatambia.

" Idara ya elimu ngazi ya halmashauri kwa ujumla wamechangia sehemu kubwa kulea matatizo kwenye vituo vya kazi huku ikishindwa kulinda siri za walimu badala yake wanapopokea malalamiko ya watoa taarifa huzirudisha kwa wahusika" anasema mwalimu .

Wazazi, walimu wanaiomba serikali kuwaelimisha mifumo gani inayotumika kuwapa walimu cheo cha mkuu wa shule kwani baadhi ya wakuu wa shule wamekuwa wakichangia kuongeza matatizo shuleni.

Pia wananchi, wazazi wanaiomba serikali kuwahamisha baadhi ya walimu wakiwemo waliokaa miaka mingi shuleni kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kuondoa dosari nyingi katika shule hiyo.

Kuwepo kwa malalamiko na tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwa mkuu wa shule na baadhi ya walimu, bodi ya shule na Idara ya elimu, DIMA Online ikafunga safari mwendo wa km 25 kutoka Tarime mjini hadi Kijiji cha Magoto ili kufahamu ukweli wa mambo.

Mwandishi wa chombo hiki cha habari alipofika ofisi ya mkuu wa shule hakupata ushirikiano kwa mkuu huyo.  Alisema hawezi kuzungumza na ili azungumze mpaka mkurugenzi wa halmashauri ambaye ni mwajiri wake ampe barua ya maandishi ili kuzungumza na Mwandishi wa habari.

DIMA Online ikawatafuta viongozi wa bodi ya shule , mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha Magoto , wananchi , wazazi, wanafunzi na kuweza kuzungumza nao.

Mwandishi wa DIMA Online akafunga safari hadi ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, kufahamu nini anachokijua juu ya tuhuma zinazoelekezwa kwa mkuu wa shule. Je nini walichokisema ? , endelea kufuatilia DIMA Online itakujuza  .

........... Itaendelea






No comments