HEADER AD

HEADER AD

DKT MPANGO AWATAKA WAKIMBIZA MWENGE KUFICHUA VITENDO VYA UBADHILIFU

Na Gustaphu Haule, Pwani 


MAKAMU wa Rais Dkt.Philip Mpango amezindua mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa huku akiwataka wakimbiza Mwenge Kitaifa kwenda kufichua vitendo vya ubadhilifu wa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo bila uoga.

Mpango amezindua mbio za  Mwenge huo April 2, 2025 katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani hafla ambayo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kitaifa.

      Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango akizindua Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa leo April 2,2025 katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha Mkoani Pwani.

Miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu Dkt.Dotto Biteko, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete.

Akizungumza katika hafla hiyo Mpango amewaambia wakimbiza Mwenge hao kuwa Taifa limewaamini na kuwapa jukumu hilo kubwa na kuwataka wafanyekazi kwa maadili na uaminifu ikiwa pamoja na kufichua vitendo vyote vya ubadhilifu bila uoga.

Amewataka wakuu wa mikoa yote 31 pamoja na viongozi wengine waliopo katika mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wanatoa ushirikiano dhidi ya wakimbiza Mwenge Kitaifa ili waweze kuwafikia wananchi na hivyo kutoa ujumbe sahihi sambamba na kufanya shughuli za maendeleo.

     Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango,akishika Mwenge tayari kwa kukabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge leo katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha Mkoani Pwani.

Dkt.Mpango ametumia nafasi hiyo pia kusisitiza mambo makubwa mbalimbali ikiwemo kila Mtanzania mwenye sifa ahakikishe anakwenda Kujiandikisha katika daftari la Kudumu la wapiga kura ili muda ukifika wakachague viongozi wazuri na wanaowataka.

Mbali na hilo amewataka wapiga kura wajitokeze katika kampeni za wagombea pindi zitakapoanza ili wapate kuwafahamu vizuri na kujua sera zao ili wakafanye chaguo sahihi wakati wa uchaguzi.

Jambo lingine alilosisitiza Dkt.Mpango ni juu ya kuwaasa vijana kuepuka vitendo viovu vinavyoashiria kuvunja amani  pamoja na wadau wa uchaguzi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu mchakato wa uchaguzi ili huwe wa amani na Utulivu.

       Vijana wa Halaiki katika uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa uliofanyika katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha Mkoani Pwani April 2,2025

Amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dkt.Hussein Mwinyi kwa kazi kubwa wanayofanya huku akiwaomba Wananchi waendelee kuwaombea viongozi hao ili waweze kutimiza vyema malengo ya kuwatumikia Wananchi.

Katika hafla hiyo Dkt. Mpango mara baada ya kuwasha Mwenge huo aliwakabidhi Mwenge vijana sita, Raymond Josephu Mbeya) Zainabu Mbwana ( Mjini Magharibi Unguja)Elizabeth Makingi (Shinyanga) Hamada Hamada(Kaskazini Pemba)Azizi Abubakar (Pwani) na Ismail Ally ( Kaskazini Unguja)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mbio za Mwenge wa Uhuru zitapita katika Mikoa 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar ukipita katika Halmashauri 195  huku akiwapongeza vijana waliochaguliwa na kusema wamechaguliwa kwa vigezo vyote.

        Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Wananchi pamoja na viongozi mbalimbali katika hafla ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa iliyofanyika leo April 2,katika vwanja vya Shirika la Elimu Kibaha Mkoani Pwani

Majaliwa amesema wakimbiza Mwenge hao wapo makini na imara kwani wamepata mafunzo ya kutosha huku akimshukuru Rais Samia kwa kukubali mwaka huu Mwenge wa Uhuru utumike kuhamasisha amani ya Nchi.

Awali,Waziri Nchi,ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete amemshukuru Rais Samia kwa kuiamini Wizara yake na kuona kuwa inafaa kusimamia jambo hilo.

     Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa leo April 2,2025 katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha Mkoani Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, ameishukuru Serikali kwa kutoa heshima kubwa ya kuzindua Mwenge wa uhuru Kitaifa mkoani Pwani ambapo ukiwa nkoani Pwani utapita katika Halmashauri tisa na Wilaya saba na kuweka mawe ya nsingi na kuzindua jumla ya miradi 64 yenye thamani zaidi ya Trilioni 1.28.

Amesema mkoa wa Pwani ni mkoa wa Viwanda ambapo mpaka sasa una Viwanda 1,535 huku viwanda vikubwa ni 124 ambapo kati ya hivyo Viwanda  78 vimepatikana wakati Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan akiwa madarakani.

Hata hivyo, Kunenge amewaomba wawekezaji mbalimbali  kuendelea kujitokeza Mkoani Pwani kwakuwa bado Kuna fursa za  kutosha na katika uwekezaji wa viwanda,kilimo,uvuvi na hata katika maeneo mengine.

      Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge (kulia) akimkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha Mkoani Pwani  April 2,2025

No comments