TAASISI YA BEGA KWA BEGA YAFANYA BONANZA KUHAMASISHA WANANCHI KUSHIRIKI UZINDUZI MBIO ZA MWENGE
Na Gustaphu Haule, Pwani
TAASISI ya Bega kwa Bega Tanzania kupitia Mkoa wa Pwani imefanya bonanza la siku moja sambamba na mbio za polepole (Jogging)kwa ajili ya kuhamasisha wananchi kushiriki uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa utakaofanyika katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha April 2,2025.
Katika uzinduzi huo,Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango anatarajia kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo ambapo Taasisi ya Bega kwa Bega Tanzania kwa kutambua umuhimu wa Mwenge wa Uhuru hapa nchini imeamua kubeba jukumu la kuhamasisha jamii kujitokeza katika uzinduzi huo kwa kufanya bonanza la michezo mbalimbali.
Bonanza hilo limefanyika April 1,2025 katika viwanja vya Bwawani vilivyopo Mailimoja Kibaha mjini ambapo miongoni mwa michezo iliyofanyika ni kukimbiza Kuku, Kuvuta kamba, mchezo wa kukimbia na gunia, ngoma za asili pamoja na mchezo wa mpira wa miguu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Kibaha , Mratibu wa Taifa wa Taasisi ya Bega kwa bega Tanzania Ruth Mateleka amesema kazi wanazofanya katika Taasisi yao ni pamoja na kuisemea miradi iliyotekelezwa na Serikali chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Mateleka amesema kuwa kutokana na umuhimu wa mbio za Mwenge wa Uhuru hapa nchini waliona kuna kila sababu ya kuhakikisha wanajitoa katika kuongeza hamasa kwa wananchi ili waweze kujitokeza kuungana na Makamu wa Rais katika shughuli nzima ya uzinduzi huo.
Mratibu wa Taasisi ya Bega kwa Bega Taifa Ruth Mateleka akizindua bonanza la michezo mbalimbali katika viwanja vya Bwawani Kibaha Mjini ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha Wananchi kujitokeza katika uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kesho April 2,2025.
Amesema Taasisi hiyo tayari imefika katika mikoa 12 hapa nchini na malengo yake ni kuhakikisha inafikia katika mikoa yote 31 iliyopo Tanzania Bara na Zanzibar ambapo kazi kuwa ni kuendelea kuizisemea kazi za kimaendeleo zilizofanywa na Serikali kupitia Rais Samia.
Ameongeza kuwa bonanza lililofanyika Mkoa wa Pwani limejumuisha washiriki kutoka mikoa mbalimbali wakiwemo kutoka mikoa ya Kigoma, Kilimanjaro,Morogoro,Pwani na Dar es Salaam.
Mratibu wa Bega kwa Bega mkoa wa Pwani Zuhura Sekelela amesema pamoja na michezo mbalimbali kufanyika lakini pia wameendesha zoezi la kuchangia damu kwa hiari na kufanikiwa kupata chumba 19 ambazo zitapelekwa hospitali kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wenye mahitaji.
"Bonanza letu limelenga kuhamasisha wananchi kushiriki uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa utakaofanyika kesho katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha Mkoani Pwani na sisi tupo tayari kushiriki ," amesema Zuhura
Zuhura amesema kwa mkoa wa Pwani wamekuwa wakitangaza kazi zilizofanywa na Serikali ambapo pia wamekuwa wakifanya usafi wa mazingira sambamba na kupanda miti kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa huo ikiwemo shule na hospitali," amesema.
Balozi wa Bega kwa Bega mkoa wa Pwani ambaye pia ni daktari kutoka hospitali ya Rufaa mkoa wa Pwani Happiness Ruta, ameishukuru taasisi hiyo kwa kuendesha zoezi la uchangiaji damu kwakuwa mahitaji ya damu kwa wagonjwa ni makubwa.
Viongozi wa Taasisi ya Bega kwa Bega na Tanzania wakiendesha bonanza Kibaha Mkoani Pwani leo April 1,2025
Ruta,ameiomba taasisi hiyo kuendelea kuhamasisha jamii juu ya suala la uchangiaji damu kwa hiari kwani kufanya hivyo itasaidia kuokoa vifo vya wagonjwa vinavyotokana na ukosefu wa damu.
Nae Mchungaji wa Kanisa la Reedemed Gospel Church (RGC) lililopo Kibaha picha ya Ndege Levalent Mwasulama amesema amejiunga na taasisi hiyo baada ya kuona shughuli wanazofanya ikiwemo kutangaza miradi ya maendeleo.
Mchungaji wa Kanisa la RGC la Kibaha Picha ya Ndege Levalent Mwasulama wa kwanza kushoto akiwa pamoja na viongozi wa Bega kwa Bega Taifa na mkoa wa Pwani.
Hata hivyo , Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa tayari mpaka sasa maandalizi yamekamilika kwa asilimia 100 ambapo amewaomba Wananchi wajitokeze kwa wingi katika uzinduzi huo.
Mratibu wa Bega kwa Bega Taifa Ruth Mateleka akizindua bonanza la michezo mbalimbali lililofanyika April 1,2025 kwa ajili ya kuhamasisha Wananchi kujitokeza katika uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kesho April 2.
Post a Comment