HEADER AD

HEADER AD

KIJIJI CHA GENKURU KILIVYO JIPANGA KUTUMIA BILIONI 1.6 ZILIZOTOLEWA NA BARRICK NORTH MARA KUTEKELEZA MIRADI


>> Fedha hizo ni asilimia moja itokanayo na uzalishaji wa dhahabu kwenye klemu cha Kijiji cha Genkuru namba 38810 kilichochukuliwa na mgodi wa Barrick North Mara.

Na Dinna Maningo , Tarime

KIJIJI cha Genkuru kina wakazi wapatao 5,664, kilichopo kata ya Gorong'a wilaya ya Tarime mkoani Mara , kinajihusisha na shughuli za kilimo, mifugo na uchimbaji wa madini.

KIJIJI cha Genkuru ni miongoni mwa vijiji vitano vilivyokuwa na leseni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu maarufu (Klemu), kijiji kilikuwa na klemu namba 38810. Vijiji hivyo ni Kijiji cha Genkuru, Kewanja, Nyangoto, Kerende na Nyamwaga ambavyo mgodi wa North Mara katika shughuli zake za uchimbaji ilichukua vlemu hivyo.

Mgodi na vijiji vilivyokuwa vinamiliki mashimo ya dhahabu viliingia makubalinao, ambapo mgodi hutoa fedha kila mwaka asilimia moja ya uzalishaji zinazotolewa kila baada ya robo mwaka kutokana na uzalishaji na kuvipatia vijiji hivyo kwa ajili ya kuendeleza vijiji katika kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo.

Katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 Mgodi wa Barrick North Mara umetoa asilimia moja Tsh. Bilioni 1.6 katika Kijiji cha Genkuru zinatolewa kwa awamu.

Awamu ya kwanza kijiji kilipokea Tsh. Milioni mbili ambapo fedha hizo zimeendelea kuongezeka kutokana na uzalishaji kwani katika robo ya mwisho mwezi Machi, 2025, Kijiji kimepokea Tsh. Milioni 746.

Uongozi wa serikali ya Kijiji cha Genkuru umejipanga kutumia fedha hizo Bilioni 1.6 ambazo bado hazijatumika zipo kwenye akaunti ya Kijiji hicho ili kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Miradi itakayotekelezwa kwa fedha hizo ni miradi katika sekta ya elimu, afya, miundombinu ya barabara, ujenzi wa soko na ununuzi wa mashine ya usingizi kwa ajili ya upasuaji.

Akizungumza na Waandishi wa habari mkoa wa Mara Aprili, 11, 2025 walipotembelea kituo cha afya Genkuru, Mtendaji wa Kijiji hicho Waitara Kemo anabainisha miradi 15 itakayotekelezwa katika Kijiji hicho.

" Tumepokea jumla Tsh. Bilioni 1.6 , fedha hizi tayari ziko kwenye akaunti ambazo ni asilimia moja ya Kijiji cha Genkuru. Zimetolewa na mgodi wa Barrick North Mara kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na zinatolewa kwa kila robo kulingana na uzalishaji.

Ujenzi wa barabara

Fedha za asilimia moja zitaweza kuondoa changamoto za barabara katika Kijiji hicho kama inavyoelezwa na mtendaji wa Kijiji.

" Kati ya fedha hizo zitatumika kujenga barabara ya Makabano hadi kwa Mwita Mosongo yenye urefu wa km4. Barabara ya Keirondo hadi Mekoma km 2,Barabara ya shule ya msingi Genkuru hadi kuruya senta km 4.

"Barabara ya Mekoma hadi  Nyansisine km 4 , barabara ya kutoka Bwirege Sec. hadi Komalera km 1.2 na ujenzi wa karavati la kuingia S/m Keirondo " anasema Mtendaji Waitara.

                     Elimu

Mradi mwingine utakaojengwa kwa fedha ya asilimia moja ya kijiji ni ujenzi wa jengo la utawala shule ya msingi Keirondo, ujenzi wa jengo la nyumba ya mwalimu 2/1 shule ya mpya Kuruya.

" Tutanunua mashine ya kuchapa (printing machine) katika shule ya msingi Genkuru , ukarabati wa nyumba 7 za walimu shule ya msingi Genkuru na ukarabati wa bweni la wavulana shule sekondari Bwirege " anasema Waitara.

                        Afya

Katika sekta ya afya nayo haijaachwa nyuma, sehemu ya fedha hizo za Kijiji itajengwa nyumba ya mtumishi 2/1 kituo cha afya Genkuru, ununuzi wa mashine ya usingizi kwaajili ya upasuaji katika kituo cha afya Genkuru.

" Ununuzi wa mashine ya Adubini  (Microscope machine) kituo cha afya Genkuru pamoja na ununuzi wa eneo kwa ajili ya ujenzi wa soko hivyo jumla ya fedha zitakazogharimu miradi hiyo ni Tsh. Bilioni 1. 531. 

Bilioni 1.6 hazijaanza kutumika

Fedha hizo licha ya kutolewa na mgodi na kuwekwa kwenye akaunti ya kijiji bado zinaendelea kusota kwenye akaunti bila kufanya kazi licha ya kuwepo changamoto katika Kijiji hicho zinazohitaji utatuzi kwa wakati.

Mtendaji huyo wa Kijiji cha Genkuru Waitara Kemo, anaeleza sababu ya fedha hizo kuendelea kukaa kwenye akaunti " Fedha bado ziko kwenye akaunti ya kijiji hazijaanza kutumika kwasababu hazikuwa na vifungu vya matumizi ila Mkurugenzi wa halmashauri ameshalishughulikia na fedha zitaanza kufanya kazi" anasema Waitara.

  Kituo cha afya kinavyosaidia

Mbali na fedha hizo asilimia moja ya kijiji zilizotolewa na mgodi kujenga miradi ya maendeleo katika mwaka wa fedha 2024/2025, mwaka 2018 mgodi ulitoa asilimia moja katika Kijiji hicho kujenga miradi ya maendeleo.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Genkuru mwaka 2014- 2023 na kuondolewa na Chama cha Mapinduzi, John Mkira anasema mwaka 2018 mgodi wa North Mara ulitoa fedha asilimia moja ya kijiji zilizotumika kujenga majengo mapya saba katika Zahanati ya Genkuru yaliyogharimu Tsh Milioni 700.

     Sehemu ya jengo la kituo cha afya Genkuru

" Ujenzi ulianza mwaka 2019  yakajengwa majengo saba ujenzi uliofikia asilimia 90 , kisha mgodi ukaleta Tsh. Milioni 151 za uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR) zikajenga  jengo la mama na mtoto na korido katika kituo hicho cha afya pamoja na Tsh. Milioni 150 za ujenzi shule ya msingi Keirondo" amesema John Mkira.

Anasema mwaka 2020 majengo yalikamilika na Zahanati hiyo ikapandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya.

 
Kituo hicho cha afya sasa kimekuwa ni msaada mkubwa kwa jamii kwa kutoa huduma ya afya saa 24 zikiwemo nyakati za usiku jambo ambalo limesaidia wajawazito kutojifungulia majumbani kwani awali ilipokuwa Zahanati wananchi walipata huduma saa 12 pekee .

Kebohi Obogi Mosabi mkazi wa Kijiji cha Genkuru anaonekana kufurahi kutokana na huduma itolewayo katika kituo hicho cha afya huku akiupongeza mgodi wa Barrick kwa ujenzi wa majengo uliowezesha zahanati kupewa hadhi ya kituo cha afya.


Kebohi Obogi Mosabi akizungumza 

" Sasa hivi tuna raha sana mgonjwa hata usiku anapata matibabu hapahapa kwenye kituo chetu cha afya, tofauti na huko nyuma mgonjwa alipougua usiku tulilazimika kutembea umbali mrefu kwenda hospitali ya halmashauri ya wilaya iliyopo Nyamwaga na hospitali ya wilaya ya Tarime 

" Tunakishukuru Kijiji chetu cha Genkuru kutoa mawazo ya kukipanua kituo na kutenga fedha zitokanazo na asilimia moja kufanya maendeleo.

" Tunaushukuru mgodi wa Barrick North Mara kwa kutekeleza asilimia moja ya vijiji itakayosaidia kuleta maendeleo kijijini bila kuisahau serikali yetu ambayo imeweza kutuletea watoa huduma wa afya kwenye kituo chetu " anasema  Kebohi.

Neema Mwita mzazi aliyejifungua akiwa katika kituo hicho cha afya anashukuru kwa huduma kutolewa usiku kwamba imewezesha wajawazito kujifungulia kituo cha afya.

           Neema Mwita akizungumza 

Pia wagonjwa waliozidiwa nyakati za usiku kupata matibabu na hivyo kupunguza vifo vilivyotokana na kukosa huduma ya afya nyakati za usiku.

Chacha Ryoba  mkono mwenye mke na watoto sita anasema pamoja na kupata huduma ya afya saa 24 kituo hicho hakitoi huduma ya kuongeza wagonjwa damu pamoja na upasuaji.

            Chacha Ryoba  mkono

Anasema hali hiyo huwalazimu wagonjwa kufuata huduma hizo hospitali ya halmashauri mwendo wa zaidi ya km 8 hivyo anaiomba serikali kusogeza huduma hizo kituo cha afya Genkuru.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Genkuru Juma Elias Kegoye anasema kuwa wakati ikiwa Zahanati huduma zilitolewa masaa manane kwa siku jambo lililosababisha wajawazito kujifungulia nyumbani.

         Mwenyekiti wa Kijiji cha Genkuru Juma Elias Kegoye.

" Limejengwa jengo la OPD, Maabara ,jengo la mama na mtoto, mochari na nyumba ya mtumishi, sasa hivi vifo vimepungua vya wajawazito kujifungulia nyumbani maana sasa wanajifungulia kituo cha afya wanapata huduma " anasema Mwenyekiti.

Kauli ya kaimu mganga Mfawidhi 

Kwa mujibu wa Kaimu mganga Mfawidhi kituo cha afya Genkuru , kituo kina watoa huduma ya afya 9 kinahudumia wagonjwa takribani 30 kwa siku wanatoka Kijiji cha Genkuru na Kijiji jirani cha Msege.

          Kaimu mganga Mfawidhi kituo cha afya Genkuru

" Wajawazito kujifungulia nyumbani kumepungua ,tunaweza maliza miezi mitatu hatujapata mzazi mwenye kesi ya kujifungulia nyumbani . Changamoto iliyopo ni baadhi ya wagonjwa kuchelewa kufika kituoni kutokana na  changamoto ya miundombinu ya barabara , mvua.

"Pia kuna changamoto ya uelewa mdogo katika jamii juu ya afya ya uzazi, elimu ya lishe bora hivyo tunawaomba wananchi wadumishe ushirikiano na kuzingatia taratibu za afya " anasema. 

Anaongeza kwamba tayari Kijiji kimeshatenga fedha za ununuzi wa mashine ya usingizi katika kituo cha afya Genkuru na ununuzi wa mashine ya Adubini  (Microscope machine) kituo cha afya Genkuru.

Meneja mahusiano mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi anasema " Kwa miaka miwili tumetoa zaidi ya Tsh Bilioni 2 kama asilimia moja ya uzalishaji katika Kijiji hiki cha Genkuru na katika kituo hicho cha afya, pia limejengwa jengo la mama na mtoto na korido la kutembelea kwa fedha za CSR " amesema Francis.

      Meneja mahusiano mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi

" Ni miongoni mwa vijiji ambavyo pia vimepata fedha za CSR ambazo zimetekeleza miradi mbalimbali ikiwemo upanuzi wa kituo cha afya Genkuru kama vile jengo la mama na mtoto " anasema Francis.

  Meneja Barrick North Mara    

Mgodi wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime mbali na kutoa asilimia moja kwa vijiji vitano umekuwa ukitoa fedha za uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR) kutokana na uzalishaji wake.

Mgodi unaendelea kutekeleza mradi wa uwajibikaji wa makampuni kwa jamii katika kata 26 , vijiji 88 vya halmashauri ya wilaya ya Tarime. Miradi hiyo ya CSR ilipitishwa  na Baraza la madiwani la halmashauri hiyo.

Asilimia 40 ya fedha za uzalishaji hupatiwa Vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa Barrick North Mara na asilimia 60 Vijiji 77 vilivyopo ndani ya halmashauri hiyo ambapo gharama za utekelezaji wa miradi ni Tsh. 9,049,264,380.

Meneja mkuu wa mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko anasema " Miradi hiyo inagusa nyanja zote muhimu za maendeleo ikiwemo elimu, afya, miundombinu, uwekezaji wa kiuchumi na mazingira" anasema.

Anaongeza kuwa, uzalishaji wa mwaka 2024 mgodi umetenga Tsh 4,687,961,715 kwa ajili ya mradi kwenye jamii, ikiwemo upanuzi wa mradi wa maji wa Matongo na kufikia vijiji vingine ulianza na Kijiji cha Kewanja.

        Meneja mkuu wa mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko akizungumza.

           Majengo ya kituo cha afya Genkuru 



      Jengo lililokuwa Zahanati ya Kijiji cha Genkuru 

No comments