WAFANYABIASHARA SIMIYU WALALAMIKA OFISI YA WAKALA WA VIPIMO KUGEUKA MAHABUSU
Na Samwel Mwanga, Simiyu
BAADHI ya wafanyabiashara katika mkoa wa Simiyu wameibua madai mazito dhidi ya Wakala wa Vipimo, wakisema kuwa wamekuwa wakikamatwa na kushikiliwa kwa saa kadhaa katika ofisi za wakala zilizoko eneo la Nyaumata mjini Bariadi kinyume cha taratibu za kisheria.
Madai hayo wameyatoa jana jumatatu Aprili 14, 2025 katika mkutano wa wafanyabiashara hao uliofanyika mjini Bariadi huku wakitoa tuhuma kwa wakala wa vipimo mkoa huo kuwakamata na kuwaweka mahabusu badala ya kuwapa elimu, wanapofanya ukaguzi wa vipimo mbalimbali kwenye maeneo yao ya biashara.
Wafanyabiashara hao wamekuwa wakikamatwa kutokana na baadhi ya bidhaa walizokutwa nazoa ambazo ni nondo, vyuma na saruji kutokuwa ma vipimo sahihi na hivyo kutuhumiwa kuwa wanahujumu Taifa.
Hamka Hamka ni mfanyabiashara mjini Bariadi wa vifaa vya ujenzi anasema kuwa mamlaka husika za serikali zinaviruhusu viwanda kuwauzia wao bidhaa hizo lakini zikifika kwao wanaelezwa kuwa wanahujumu taifa hilo ni jambo la kushangaza.
Mfanyabiashara wa mjini Bariadi,Hamka Hamka akitoa malalamiko yake katika kikao cha wafanyabiashara wa mkoa wa Simiyu.
"Kule viwandani wanaruhusu nondo zenye urefu wa futi 38, unamkamata mfanyabiashara kapunguza futi mbili ili azifanyie nini? inchi moja ya vyuma (pipe) inapungua theluthi tunaambiwa tunaihujumu nchi wakati bidhaa imetoka kiwandani,”
"Unajiita una mamlaka ya kuweka wafanyabiashara mahabusu, polisi imeenda wapi, mahakama imeenda wapi, ile ofisi ya wakala wa vipimo ina mahabusu huo ndiyo utaratibu ? amehoji.
Maria John ni muuzaji wa duka la vifaa vya ujenzi linalomilikiwa na baba yake mzazi, John Sabu amesema kuwa afisa wa vipimo wa mkoa huo alifanya ukaguzi kwenye duka na kukuta mifuko miwili ya saruji aliyodai imepungua uzito na kuwatoza faini ya Tsh Milioni 20 huku wakiwatishia kuwapeleka mahakamani.
Baadhi ya wafanyabiashara waliohudhuria mkutano wao na Wakala wa vipimo mkoa wa Simiyu uliofanyika mjini Bariadi.
"Walishindwa kuelewana na baba wakitishia kutupeleka mahakamani, hatukutaka maongezi yoyote na mifuko miwili ya saruji alikuwa ameichukua, alisema faini ni Tsh Milioni 20 kama mko tayari tutaongea lakini faini lazima ilipwe," amesema.
Naye Kuchonke Togoro ambaye ni mwakilishi wa kituo cha kuuza mafuta cha Nengelo kilichopo Nkololo, amesema kuwa kituo chao kilipigwa faini ya Tsh Milioni 1.5 licha ya kufanya mazungumzo na meneja wa vipimo mkoa huo lakini alimfungia ofisini kwake kwa saa tatu.
"Niliitwa ofisini kwake, baada ya kushindwa kuelewana aliniambia twende kituo cha polisi, mimi nikagoma na nikamwambia nenda ili polisi waniite, akanifungia ofisini kwake kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi aliporudi saa 6:30 mchana," amesema.
Afisa mtendaji mkuu wa wakala wa vipimo nchini, Alban Kihula, amesema kuwa masuala ya mahabusu yako Jeshi la polisi na kama kuna mfanyabiashara ana tatizo na wakala wa vipimo huwasiliana na jeshi la polisi kwa hatua zaidi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini, Alban Kihula (katikati), akimsikiliza hoja za Wafanyabiashara mjini Bariadi.
Akizungumzia madai ya wafanyabiashara hao kutozwa faini kubwa, amewataka wafanyakazi wa wakala wa vipimo mkoa huo kutumia busara kwa asilimia sabini ili kuondoa migogoro na malalamiko ya wafanyabiashara.
“Faini hizo zinatokana na bidhaa zinazokuja kukaguliwa na wakala wa vipimo kutokuwa na vipimo sahihi,ikiwemo uzito,ujazo na unene wa bidhaa husika,”amesema.
Post a Comment