SERIKALI YAVITAKA VYAMA VYA MSINGI KUDHIBITI UBORA WA KAHAWA
Na Alodia Dominick, Bukoba
SERIKALI mkoani Kagera imevitaka vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) mkoani humo kudhibiti ubora wa kahawa kuanzia shambani hadi sokoni, kudhibiti magendo ya zao hilo ili mkulima aweze kupata bei nzuri.
Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya Bukoba Erasto Sima wakati akifungua mkutano mkuu wa chama kikuu cha ushirika cha mkoa wa Kagera KCU 1990 ltd kama mgeni rasmi.
Sima amesisitiza kudhibiti ubora wa zao la kahawa ikiwa bado shambani hadi sokoni na kuzitaka AMCOS kusimamia ubora huo na kuwahamasisha wakulima mkoani Kagera kuvuna kahawa iliyokomaa na kuianika kwa ubora ili mkulima aweze kupata bei nzuri sokoni.
Amesema kuna baadhi ya wakulima wanavuna kahawa mbichi kwa kigezo cha kupata fedha na wengine wanaanika kahawa chini kwenye udongo na kuikausha kahawa katika viwango ambavyo siyo vizuri na kuwa jambo hilo halikubaliki.
"Kahawa inapovunwa ikiwa mbichi inanyauka lakini pia inakosa ubora, swala hili linarudisha nyuma jitihada za serikali za kumkomboa mkulima, nawasihi viongozi wa AMCOS kusimamia jambo hili na mkulima atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria" amesema Sima .
Amesema richa ya wakulima kuvuna kahawa mbichi pia wapo watu wasio wema ambao wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kwenda kwenye mashamba ya wakulima na kuvuna kahawa mbichi, ambapo wakuu wa wilaya wamekuwa wakikumbana na kesi za mara kwa mara za wizi wa kahawa mbichi mashambani.
Amewasihi kuvuna kahawa iliyoiva na kuianika kwa njia bora na kwamba mkoa wa Kagera unapakana na nchi jirani zaidi ya tatu jambo linalosawishi watu kujiingiza kwenye magendo ya kahawa na kusababisha serikali kukosa mapato na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Wakati huo huo mwasibu mkuu wa KCU 1990 ltd Tatianus Kamoi akisoma taarifa ya mapato na matumizi amesema kuwa, kwa msimu 2025/2026 wamekadilia kukusanya kilo milioni 8.5 kahawa ya maganda na kahawa safi ya organic milioni 2.
Amesema kwa mwaka 2024/2025 walikisia kukusanya kilo za kahawa ya maganda kilo milioni 10 kahawa iliyopelekwa mnadani ni kilo milioni 4.9 na kahawa safi organic walikisia kukusanya kilo milioni 2.5 na zikakusanywa kilo milioni 1.3.
Mwenyekiti wa KCU 1990 ltd Ressy Mashulano amesema kuwa, ushirika huo msimu 2024/2025 ulikopa benki ya maendeleo ya wakulima TADB Tsh Bilioni 10.4 na hadi machi mwaka huu.
Amesema ushirika huo ulikuwa umemaliza kulipa mkopo na riba kiasi cha Tsh. Bilioni 11 na kuwa msimu 2025/2026 wanatarajia kukopa sh. bilioni 27, bilioni 20 zitatumika kununua kahawa na Tsh. Bilioni 7 ujenzi wa hotel mpya ya Lake.
Post a Comment