HEADER AD

HEADER AD

PROFESA MKENDA AWATAKA WABUNIFU KUWA INJINI YA UCHUMI WA TAIFA

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI wa Elimu , Sayansi, na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amewahimiza wabunifu nchini kuamka na kuwa sehemu ya msingi ya mabadiliko ya kiuchumi ya Taifa .

Lengo ni kuendeleza ajenda ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza uchumi kupitia ubunifu na maendeleo ya viwanda.


Ametoa kauli hiyo katika hafla ya uzinduzi wa ushirikiano kati ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Benki ya CRDB unaolenga kutoa mikopo nafuu kwa wabunifu ili kuwawezesha kubadilisha mawazo yao kuwa biashara zenye tija iliyofanyika tarehe 17 Aprili 2025 katika ukumbi wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Akiongea katika hafla ya utiaji saini, Profesa Mkenda amesisitiza kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo mahsusi kuhakikisha vijana wabunifu nchini wanawezeshwa kwa vitendo, si tu kwa maneno, ili kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za kiuchumi na kijamii. 

Amesema kuwa kwa kufuata dira hiyo ya Rais, Serikali iko tayari kushirikiana na sekta binafsi na taasisi za umma kuondoa vikwazo vinavyokwamisha mawazo bunifu kufikia hatua ya kibiashara.

“Wabunifu ndio injini ya uchumi wa kisasa. Nchi zilizoendelea zilitumia ubunifu kama nguzo ya maendeleo yao, na Tanzania hatuwezi kuwa tofauti. Maelekezo ya Rais ni kuhakikisha vijana hawa wanawezeshwa kwa kila njia, kifedha, kitaalamu, na kimazingira, ili taifa linufaike na vipaji vyao,” amesema Profesa Mkenda.

Aidha, ametumia fursa hiyo kuipongeza Benki ya CRDB kwa kuona fursa ya kuwekeza kwa wabunifu wa Kitanzania, jambo alilolieleza kuwa ni mfano bora wa taasisi binafsi kushiriki katika maendeleo jumuishi ya taifa.


 “Nawapongeza CRDB kwa kuchukua hatua hii ya kihistoria. Mmekubali kuwa sehemu ya mabadiliko na mmeshika mkono wa vijana ambao mara nyingi wamekuwa wakihangaika kutafuta mtaji wa kuanzisha au kukuza ubunifu wao,” ameongeza.

Pia amewataka wadau wengine zikiwemo taasisi za fedha, sekta binafsi, mashirika ya kimataifa, na watunga sera kuiga mfano wa CRDB kwa kuwekeza kwa wabunifu, hususan vijana, na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha ubunifu na maarifa afrika mashariki.

Amesisitiza kuwa nchi itakapowekeza kwa wabunifu wake, itakuwa na uhakika wa kupunguza ukosefu wa ajira, kukuza viwanda vya ndani, na kuleta mageuzi ya kiuchumi yanayochochewa na maarifa ya ndani.

Katika hafla hiyo, Profesa Mkenda hakusita kugusia umuhimu wa kuendeleza masomo ya akili-undi (Artificial Intelligence – AI) na teknolojia zingine za kisasa mashuleni na vyuoni, akieleza kuwa huo ndio mwelekeo wa dunia na Tanzania haiwezi kubaki nyuma.

 “Masomo ya akili-undi na teknolojia za kisasa lazima yawe sehemu ya mitaala yetu. Tunahitaji kuandaa kizazi chenye uwezo wa kushindana kimataifa kwa maarifa, sio kwa nguvu za misuli,” amwsisitiza.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia  (COSTECH) Dkt. Amos Nungu, ameeleza kuwa zaidi ya wabunifu 400 kutoka mikoa mbalimbali nchini wamefikiwa kupitia programu za uwezeshaji, wengi wao wakiwa vijana waliopata mafunzo, ushauri, na sasa wako katika mchakato wa kupata mikopo nafuu kupitia CRDB.

Amesema mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Rais Samia za kuhakikisha teknolojia, ubunifu, na maarifa vinatumika kama nyenzo za kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation,Tully Esther Mwambapa, amesisitiza kuwa benki yake imedhamiria kuwekeza katika mabadiliko ya kweli kwa kusaidia wabunifu wenye miradi yenye mwelekeo wa kibiashara. 


Amesema kuwa ushirikiano na COSTECH ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo wa kuunga mkono maendeleo jumuishi na kukuza uchumi unaoongozwa na bunifu za na kiteknolojia.

Kauli ya Profesa Mkenda ni mwitikio chanya wa serikali katika kuhakikisha kuwa Tanzania haibaki nyuma katika mapinduzi ya kiuchumi yanayoongozwa na ubunifu.

Kwa sasa, wabunifu wana nafasi ya kipekee kuwa sehemu ya mabadiliko ya taifa, wakihimizwa kutumia fursa zilizopo, huku jamii nzima ikihamasishwa kuwaunga mkono kwa dhati ili wajenge Tanzania ya kisasa katika kuhakikisha kuwa Tanzania haibaki nyuma katika mapinduzi ya kiuchumi yanayoongozwa na ubunifu.

No comments