POLISI SIMIYU YAWAONYA SUNGUSUNGU
Na Samwel Mwanga, Simiyu
JESHI la jadi la Sungusungu limeonywa kuacha mara moja tabia ya kujichukulia sheria mkononi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya ulinzi wa jadi katika jamii.
Onyo hilo limetolewa jana jumamosi,April 5,2025 wilayani Itilima na kamanda wa polisi mkoa wa Simiyu, Kamishina Msaidiziwa Polisi,Edith Swebe alipokuwa akizungumza na vikundi vya ulinzi shirikishi katika wilaya hiyo.
Amesema kuwa ingawa jeshi hilo ni sehemu ya mifumo ya jadi ya ulinzi inayotambuliwa na jamii, hawaruhusiwi kuwachukulia hatua watu bila kufuata taratibu za kisheria.
Kamanda wa polisi mkoa wa Simiyu,Edith Swebe akizungumza na wanajeshi wa jeshi la jadi la Sungusungu katika wilaya ya Itilima.“Tunakiri mchango wa Sungusungu katika kudumisha amani vijijini, lakini tunawakumbusha kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria. Mtu akituhumiwa kwa kosa lolote, ni wajibu wenu kumfikisha kwenye vyombo vya dola, si kumpiga au kumwadhibu mtaani,” amesema.
Amesema vikundi hivyo vya ulinzi shirikishi likiwemo jeshi hilo la jadi vinatambulika kisheria hivyo viongozi wa vikundi hivyo wanatakiwa kusimamia kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu pamoja na miongozo ya nchi.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano wa Sungusungu ulioitishwa na jeshi la polisi katika wilaya ya Itilima mkoa wa Simiyu.Mkazi wa mji wa Langangabilili wilayani humo Matondo Jilala amesema ni vizuri kwa serikali kutoa mafunzo rasmi kwa wanajeshi wa jeshi hilo la jadi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na bila kuvunja haki za binadamu.
“Ili kupunguza malalamiko ya jeshi hili la jadi ni vizuri serikali ikaona umuhimu wa kuwapatia wanajeshi hao mafunzo rasmi ya muda mfupi ili watelekeze majukumu yao kwa mujibu wa sheria za nchi,naona hii itakuwa njia nzuri juu ya utendaji wao,”amesema.
Naye mkazi wa kijiji cha Lugulu wilayani humo, Jilala Maduhu amesema kuwa jeshi hilo linafanya kazi nzuri sana ya kuzuia uhalifu katika maeneo ya vijijini hivyo linapokwenda kutekeleza majukumu yake ni vizuri awepo askari polisi ili kuepuka uvunjifu wa sheria.
“Sungusungu wanafanya kazi nzuri sana katika maeneo yetu ya vijijini na hao ndiyo wameweka hali ya utulivu huwezi kusikia matukio ya wizi kwa sasa ila sasa,ili waweze kufanya majukumu yao vizuri waambatane na askari polisi,”amesema.
Mahona Jinunu ni kiongozi wa Sungusungu wilayani humo amekiri kuwepo kwa baadhi ya matukio yasiyofuata sheria, lakini amesema kuwa changamoto hizo zinasababishwa na ukosefu wa mafunzo na vifaa vya kutosha.
Jeshi la jadi la Sungusungu limekuwa likitekeleza jukumu la kulinda usalama katika maeneo mbalimbali ya vijijini, hasa maeneo yenye uhaba wa askari wa polisi, lakini limekuwa likikumbwa na malalamiko ya matumizi ya nguvu kupita kiasi.
Wananchi wa wilaya ya Itilima waliohudhuria mkutano wa Sungusungu ulioitishwa na jeshi la polisi.
Post a Comment