HEADER AD

HEADER AD

WAKO JUU YA SHERIA



Wako juu ya sheria,

Wewe chini ya sheria,

Nao ukishindania,

Elewa utaumia,

Endapo wanakujia,

Pembeni ukapishia,

Amani itabakia,

Hata kama waumia.


Wako juu ya sheria,

Wanazijua sheria,

Ila kufuatilia,

Wewe wanakuachia,

Wanavunja angalia,

Vunja wakukamatia,

Mpini washikilia,

Acha kuwafwatilia.


Wako juu ya sheria,

Wewe wakushikilia,

Wao wanajipitia,

Foleni waisagia,

Mbele wanatangulia,

Sheria wajivunjia,

Nani utamuambia?

Wewe fanya kuridhia.


Wako juu ya sheria,

Wewe chini ya sheria,

Waweza kusingizia,

Kile hujajifanyia,

Kibano kukupatia,

Ubaki wajililia,

Huna kwa kukimbilia,

Mpini washikilia.


Uko chini ya sheria,

Yote unafwatilia,

Ukipitiwa sikia,

Kama mwewe wakujia,

Utu mbali watupia,

Hata kiwaangukia,

Utailipa fidia,

Ubaki unajutia.


Wako juu ya sheria,

Hata wakikupitia,

Ukichukua sheria,

Yaweza kukulalia,

Kesi ya nyani sikia,

Tumbili asikizia,

Haki hutaipatia,

Utabaki unalia.


Wako juu ya sheria,

Wewe chini ya sheria,

Baya wanakufanyia,

Nawe wawashitakia,

Waweza kugeuzia,

Kibao kukubania,

Hata ukiwabishia,

Haki hutaisikia.


Lini nami tafikia,

Niwe juu ya sheria,

Walo juu ya sheria,

Niweze watapikia,

Vile wanatufanyia,

Haifai Tanzania,

Bora wakajirudia,

Haki kusisitizia.


Walo juu ya sheria,

Wabaya ni masalia,

Wanazijua sheria,

Chini wanazifukia,

Onyo nawatamkia,

Moto wawachemkia,

Na wasipoangalia,

Kazi haitasalia.


Walo juu ya sheria,

Wema wengi Tanzania,

Wachache walosalia,

Doa kubwa wawatia,

Tena vile wasikia,

Ubaya wajivumia,

Leo nawaachilia,

Ni msamaha sikia.


Wako juu ya sheria,

Sisi chini ya sheria,

Wema twawafagilia,

Torati washikilia,

Haki wanaitumia,

Chuki kuidhibitia,

Hao hasa twatambia,

Kwa amani Tanzania.


Ni msumeno sheria,

Hilo walishikilia,

Milungula kiwajia,

Kudaka hutasikia,

Hata ukiwavizia,

Baya hutajipatia,

Hao ninawaambia,

Mungu atawalipia.


Wako juu ya sheria,

Chini wanaangalia,

Waweze tutatulia,

Yale yanatuzidia,

Hukumu wakikazia,

Mwisho mwema twafikia,

Lakini wakiachia,

Ni hasara Tanzania.


Kote kuliko sheria,

Utii twafagilia,

Shuruti kutotumia,

Hiyo bora yasalia,

Kwa wote sawa sheria,

Siwepo wa kusalia,

Uwe juu ya sheria,

Au chini ya sheria.


Ni haki mtawalia,

Ambayo tunalilia,

Nyumbani kazini pia,

Sheria kushikilia,

Na barabarani pia,

Haki ipate timia,

Sote tutafurahia,

Bila jisikitikia.


Wako juu ya sheria,

Tuko chini ya sheria,

Ajira twawapatia,

Si ya kutunyanyasia,

Jueni mnasalia,

Posho tunawalipia,

Nyendo zenu angalia,

Mkitaka kusalia.


Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments