HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI : JICHO LIMEPOTEA

NI changamoto pokea, msijekujitetea,

Kwa sasa mmelegea, jicho lenu lapotea,

Kule inategemea, na kusema mwachelea,

Bali mwana mpumbavu, ni mzigo wa mamaye. 

Jicho twalielezea, watoto livyozoea,

Yenu huko kupokea, kwa jicho kuwamegea,

Mambo ya kushobokea, wasiweze endelea,

Bali mwana mpumbavu, ni mzigo wa mamaye. 

Ni jicho limepotea, la mama naelezea,

Watoto kuwatolea, yaweze kuwaelea,

Kwa lengo la kukemea, na kuwaelekezea,

Bali mwana mpumbavu, ni mzigo wa mamaye. 

Wengi wanaelezea, jicho lilivyokolea,

Mama akikutolea, nawe ulivyopokea,

Kile unaendelea, maagizo kipokea,

Bali mwana mpumbavu, ni mzigo wa mamaye. 

Jicho ukilipokea jinsi anakutolea, 

Yote linaelezea, yatakayokutokea,

Kwa heshima wapokea, uweze kuendelea,

Bali mwana mpumbavu, ni mzigo wa mamaye. 

Wageni mkipokea, na wewe wawachezea,

Mama takuelezea, kwa jicho hatasogea,

Kwako cha kuendelea, ndicho anategemea,

Bali mwana mpumbavu, ni mzigo wa mamaye. 

Adabu ilienea, jicho walivyopokea,

Kama hayakuelea, mama livyotegemea,

Kichapo walipokea, nidhamu kuendelea,

Bali mwana mpumbavu, ni mzigo wa mamaye. 

Mbona jicho lapotea, wapi limeelekea?

Lawama mnapokea, kinamama mwalegea,

Kipi kinaendelea, jicho mwalipotezea?

Bali mwana mpumbavu, ni mzigo wa mamaye. 

Ni simu mnachezea, kiasi zawalemea?

Usasa umeenea, huko mnaegemea?

Nini kinachotokea, malezi yawalemea?

Bali mwana mpumbavu, ni mzigo wa mamaye. 

Hizo nyumba tembelea, watoto tajionea,

Adabu imepotea, wageni wawachezea,

Jicho la kuwakemea, kama limetokomea,

Bali mwana mpumbavu, ni mzigo wa mamaye. 

Jicho lenu twatetea, vile tulilizoea, 

Kwamba lingeendelea, watoto kuwalelea,

Nidhamu ingerejea, sote tukichekelea,

Bali mwana mpumbavu, ni mzigo wa mamaye.

(Mithali 10:1) 

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments