SHAIRI : KUUA NDEGE WAWILI
KUUA ndege wawili, jiwe moja mtihani,
Wote wakienda chali, moja takuwa kifoni,
Mwingine zile dalili, hajafa ni taabani,
Kuua ndege wawili, jiwe moja mtihani,
Narusha kwa nguvu zote, liwafikie mtini,
Naona dalili zote, litawapata shingoni,
Sasa walete walete, waanguke hapa chini,
Kuua ndege wawili, jiwe moja mtihani.
Vile nawakimbilia, miye niko furahani,
Pale nikiwafikia, niwatie mkononi,
Mboga nitajifanyia, nile waende tumboni,
Kuua ndege wawili, jiwe moja mtihani.
Naanza wakimbilia, kunguru aruka chini,
Vile ninawarukia, mmoja yu mdomoni,
Si yule alozimia, bali alo mautini,
Kuua ndege wawili, jiwe moja mtihani.
Nina hasira mkizi, zake hazioni ndani,
Iweje nafanya kazi, ndege ale kilaini?
Nitatengeneza tanzi, anaswe huko angani,
Kuua ndege wawili, jiwe moja mtihani.
Hii shule naitaka, na biashara sokoni,
Nilidhani bila shaka, nitabakia makini,
Nisome bila mpaka, pesa zije kibindoni,
Kuua ndege wawili, jiwe moja mtihani.
Kwa ule mwezi wa kwanza, nikabaki taabani,
Kufwata bidhaa Mwanza, nikakosa mitihani,
Nasoma mbele machenza, kibaka katia ndani,
Kuua ndege wawili, jiwe moja mtihani.
Sawa kula na kumeza, si pamoja asilani,
Kimoja wakimaliza, kingine chaja njiani,
Hata kijibaraguza, viwili haviendani,
Kuua ndege wawili, jiwe moja mtihani.
Japo maisha ya sasa, figa moja sisaini,
Kwa mapishi ya kisasa, taingia mtaroni,
Nitaongeza kabisa, mawili chungu mekoni,
Kuua ndege wawili, jiwe moja mtihani.
Kufanya huku na huko, kunaongeza thamani,
Wapata huku na huko, unaviweka ghalani,
Kumoja kama hakuko, kwingine ni kivulini,
Kuua ndege wawili, jiwe moja mtihani.
Ofisi na biashara, vivyo nenda mzigoni,
Hata kidogo hasara, usipate kisirani,
Ndivyo waongeza kura, na chakula cha mezani,
Kuua ndege wawili, jiwe moja mtihani.
Ili maisha yaende, bora tujitahidini,
Tusitake tujilinde, kuikwepa mitihani,
Makunguru tuwaponde, tuchakarike kazini,
Kuua ndege wawili, jiwe moja mtihani.
Maisha ni mitihani, na sisi twende kazini,
Twende tuchume juani, tukalie kivulini,
Mashindano duniani, maisha yasiwe duni,
Kuua ndege wawili, jiwe moja mtihani.
Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment