HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI : MAVAZI YAJIELEZA


ONEKANA yai viza, 

Au unayependeza,

Mwenyewe yote waweza,

Vile wajitengeneza,

Watu watakutukuza, 

Na hata kukupuuza,

Fanya kile unawaza,

Ndicho kitajitokeza.


Picha zimejieleza,

Zile wamezitangaza,

Wawili wajieneza,

Vile mtu ajiweza,

Mmoja anapendeza,

Nguo amezikoleza,

Mwingine kajichuuza,

Nguo kajibaraguza.


Swali linajitokeza,

Mtu anayeongoza,

Ambaye pia aweza,

Kwa watu akatokeza,

Kichwa acha kuumiza,

Mavazi yajieleza,

Yule anayependeza,

Kura zinatosheleza.


Vipi wataka tokeza,

Kwa watu ukapendeza,

Na moyo wako kusuza,

Kwamba umejiongeza,

Au unajipuuza,

Kama bangi wapuliza?

Jua wajiangamiza,

Nakuambia sikiza.


Kama utajitokeza, 

Mbele za watu pendeza,

Kama unaokoteza,

Nguo za kujiliwaza,

Mwenyewe wajipunguza,

Hadhi unayoiweza,

Na hata unapoteza,

Utu ulotengeneza.


Kwa nguo wajieleza,

Thamani ilokujaza,

Kwa hizo unapoteza,

Heshima unayoweza,

Unakokwenda chunguza,

Uwezavyo tokeleza,

Uwe wanaoongoza,

Kwa jumla kupendeza.


Huwa sare naziwaza,

Jinsi zinavyopendeza,

Hadhi zinatuongeza,

Vile tunavyotokeza,

Hakuna wa kujikweza,

Wala anayejitweza,

Kama zingefululiza,

Zingezidi kututunza.


Nenda tembea pendeza,

Macho ukiyaliwaza,

Asiwepo wa kubeza,

Kwamba unamshangaza,

Kote unakotokeza,

Usionekane giza,

Hayo mavazi nawaza,

Ni vema kuyahimiza.


Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments