HEADER AD

HEADER AD

MKURUGENZI WA TANESCO NCHINI AFARIKI KWA AJALI YA GARI

MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) Mhandisi Gissima Nyamohanga amefariki dunia usiku wa kuamkia Jumapili, Aprili 13, 2025 kufuatia ajali ya gari iliyotokea wilayani Bunda mkoani Mara.

Akizungumza kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara Pius Lutumo amesema tukio hilo limetokea majira kati ya saa nane usiku wa kuamkia leo baada ya dereva kumkwempa mwendesha baiskeli na kugongana na lori uso kwa uso.

Kwa mujibu wa kamanda Lutumo ajali hiyo pia imesababisha kifo cha dereva wake.


"Ni kweli tukio lipo na amefariki dunia yeye na dereva wake baada ya kumkwepa mwendesha baiskeli na kugongana uso kwa uso na Lori" Amesema kamanda wa polis mkoa wa Mara.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali teule ya wilaya ya Bunda huku wakisubiri taarifa zaidi kuhusu taratibu zingine.

TANESCO kupitia mitandao yake ya kijamii wametoa taarifa hiyo wakitangaza masikitiko.

Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inasikitika kutangaza kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamohanga.

Bodi ya Wakurugenzi inatoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, wafanyakazi wa TANESCO, na Watanzania wote kwa msiba huu mkubwa.

Taarifa zaidi kuhusu taratibu za mazishi na shughuli nyingine za maombolezo zitatolewa kadri mipango inavyoendelea kuratibiwa.

No comments