HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI : SUMU AMENITILIA


DUNIA nasimulia, kule nilikoanzia,

Ninasema ninalia, hapa tulipofikia,

Mtu namfurahia, naye ninajisikia,

Kumbe kutoka kidogo, sumu amenitilia.


Kunywa sikuangalia, mdomo taka kutia,

Paka akanirukia, chombo kuniparuria,

Chini kikaangukia, moto ukainukia,

Kumbe kutoka kidogo, sumu amenitilia.


Wengine kwa kujulia, hata bila kujulia,

Zama tulishachanjia, ulinzi umetulia,

Kitaka tushambulia, fanya kwa kushitukia,

Kumbe kutoka kidogo, sumu amenitilia.


Moto kuuangalia, sakafu inatitia,

Sumu ingeniingia, na mimi ningeishia,

Mbona nikimwangalia, malaika avutia,

Kumbe kutoka  kidogo, sumu amenitilia.


Hasira nilichukia, vipi ananifanyia,

Paka nikamwangalia, kuona afurahia,

Chaka ningeliingia, hatari ingenijia,

Kumbe kutoka kidogo, sumu amenitilia.


Mtesi namwangalia, vipi ananiwangia,

Macho ninamkazia, chini anainamia,

Kama ningemjulia, hali singemjulia,

Kumbe kutoka kidogo, sumu amenitilia.


Mungu amemtumia, paka shari nikingia,

Miye namshangilia, mema ananiwazia,

Wale wananiwangia, wenyewe wataishia,

Kumbe kutoka kidogo, sumu amenitilia.


Ndiyo ilivyo dunia, watu vema angalia,

Wakutabasamulia, hata kukukumbatia,

Moyoni wakuwazia, kwamba ungeangamia,

Kumbe kutoka kidogo, sumu amenitilia.


Ukiwepo watulia, na kukuchangamkia,

Wape kisogo watia, sumu kukumalizia,

Pale ukiparudia, watu wanakununia,

Kumbe kutoka kidogo, sumu amenitilia.


Pale unajiishia, hata kazi kufanyia,

Pesa zinapoingia, amani wajipatia,

Vema sana angalia, sumu isijeingia,

Kumbe kutoka kidogo, sumu amenitilia.


Ni bahati nakwambia, paka kukuvurugia,

Kumbe anasaidia, usijekuangamia,

Kitu cha kujifunzia, wanadamu angalia,

Kumbe kutoka kidogo, sumu amenitilia.


Na wewe nakuambia, haya unayosikia,

Usijeukajitia, wengine kuwawangia,

Wakabaki wanalia, ulivyowaharibia,

Kumbe kutoka kidogo, sumu amenitilia.


Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments