MPASUKO WA WALIMU MAGOTO SEC. WAZAZI, WAJUMBE WA BODI WAFUNGUKA
>> Mkurugenzi Tarime atuma watu kufanya uchunguzi
Na Dinna Maningo, Tarime
Hivi karibuni chombo hiki cha habari kiliripoti changamoto mbalimbali katika shule ya sekondari Magoto, iliyopo wilaya ya Tarime , mkoani Mara ambazo zisipotatuliwa zinaweza kupelekea kushuka kwa taaluma ya wanafunzi kutokana na kuwepo kwa makundi ya walimu yanayosababisha kutoelewana.
Kama ilivyoripotiwa Aprili 8, 2025 zilielezwa tuhuma mbalimbali zikimuhusisha mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Magoto, Christopher Kinene Mosabi ikiwemo kushindwa kuwaunganisha walimu.
Tuhuma zingine ni pamoja na ushirikishwaji duni wa walimu, kukoseka
na kwa uwazi wa mapato na matumizi ya miradi ya shule, wazazi kuchangishwa fedha kwa ajili ya walimu wa kujitolea wa masomo ya sayansi lakini hakuna walimu, fedha za wanafunzi wa hosteli kutojulikana matumizi yake.
Kuwepo kwa tuhuma hizo Aprili 2, 2025 Mwandishi wa DIMA Online akafunga safari mwendo wa takribani kilomita 25 kutoka Tarime mjini hadi shule ya sekondari Magoto ili kufahamu ukweli wa mambo ikiwa ni pamoja na kuzungumza na uongozi wa shule, wananchi, wazazi, wanafunzi na wajumbe wa bodi ya shule.
Mwandishi wa chombo hiki cha habari alifika ofisi ya mkuu wa shule hiyo ili kupata majibu ya tuhuma zinazoelekezwa kwake lakini alikataa kuzungumza na kwamba ili azungumze mpaka mkurugenzi wa halmashauri ambaye ni mwajiri wake ampe barua ya maandishi ili azungumze na mwandishi wa habari.
"Sio kwamba sitaki kukupa ushirikiano ila kama unavyojua hii ni aasisi ina msemaji wake ambaye ni mkurugenzi wa halmashauri mwajiri wangu ndio msemaji , nitazungumza pale nikipata barua aliyoiandika yeye kuruhusu nizungumze na wewe, hata akinipigia simu bado haitatosha mpaka anipe barua ambayo nitaifaili " anasema mkuu wa shule.
Mwenyekiti wa Bodi ya shule afunguka
Mwandishi akazungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya shule ya sekondari Magoto, Amon Wambura muuguzi mstaafu ili kujua nini anachokifahamu katika shule akiwa kama mzoefu ndani ya bodi kwa miaka kumi.
Mwenyekiti huyo anaanza kwa kusema kuwa amekuwa mjumbe wa bodi ya shule kwa miaka 4 kisha akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa bodi aliyoiongoza kwa miaka minne, akachaguliwa tena nafasi hiyo mwaka 2023 kuongoza kwa miaka mitatu.
Anasema kuwa hafahamu yanayoendelea katika shule likiwemo la walimu kugawanyika makundi na hakuna malalamiko ya walimu yaliyofika kwenye bodi kwakuwa hashirikishwi mambo mengi yanayofanyika shuleni yakiwemo ya nidhamu na taaluma.
"Wanasema kwamba mkuu wa shule amekuwa akinichagua mara kadhaa kuwa kwenye bodi. Mimi sina mwanafunzi kwenye hiyo shule, nimekuwa mjumbe wa bodi miaka minne kabla hata ya huyo mkuu kuletwa hapa shuleni.
"Ulipofika uchaguzi wa mwenyekiti wa bodi huyu mkuu wa shule wa sasa aliniletea barua kwamba nimechaguliwa na wajumbe kuwa Mwenyekiti wa bodi nikaongoza kwa miaka minne .
"Ulipofanyika tena uchaguzi mwingine nikaletewa barua kuwa nimechaguliwa kuwa mwenyekiti wa bodi kwa miaka mitatu itakayoisha mwaka kesho, mimi sijichagui wananichagua wenyewe hata nilipochaguliwa awamu hii nilikataa lakini walisema kwamba wamenichagua mimi , labda wana sababu zao za kunichagua" anasema Amon.
Akizungumza kuhusu vikao vya bodi ya shule anasema "Kiukweli sijui mambo mengi ya shule kwasababu tangu bodi ichaguliwe mwaka 2023, tulishakaa kikao cha bodi mara moja tu ambacho kulikuwa cha kututambulisha.
"Tulikaa kikao kingine kimoja cha dharura basi hatujawahi kuitwa tena, huu ni mwaka wa tatu unaelekea kuisha tangu tuchaguliwe, bodi inatakiwa kukaa kikao mara mbili kwa mwaka na vikao vya dharura ambavyo vinaweza kukaa wakati wowote.
"Pengine labda mkuu haitishi kikao labda hana posho za kulipa wajumbe maana huwezi kuacha kazi zako unakuja kikaoni alafu unaondoka bila kulipwa posho ya kikao ukizingatia wajumbe wengine wanatoka mbali vijiji jirani.
"Mwandishi muulize mkurugenzi wa halmashauri kwanini wajumbe wa bodi wao wakikaa hawawezeshwi nauli maana hata nauli mkuu wa shule anatulipa kwa fedha zake za mfukoni.
Alipoulizwa kama anafahamu chochote kuhusu mpasuko wa walimu na changamoto zingine za shule, anasema kuwa bodi imekuwa haishirikishwi mambo mengi ya shule na hakuna mwalimu ambaye amewahi kupeleka malalamiko kwa bodi ya shule hivyo inakuwa ni vigumu kufahamu yanayoendelea shuleni.
"Bahati mbaya wale walimu hawanishirikishi, kuna mwalimu mmoja alikuwa ni mkuu msaidizi anaitwa Yusuf ndio aliwahi kuja kwangu akimlalamikia mkuu wa shule, yeye alishahamishwa kwenda kuwa mwalimu mkuu wa shule moja ila wengine hao wanaona kama mimi nina urafiki na mkuu wa shule .
"Juzi tu kuna mwalimu alikuja kwangu kulalamika akimlalamikia mkuu wa shule kwamba hafiki shuleni akatulia, anafika tu anaondoka na ukimfuatilia anasema anaenda kikao Nyamwaga kumbe anaenda kwa familia yake huko kwao, kwamba amekuwa akijihusisha na siasa".
"Niliongea na mkuu wa shule akasema yeye akiondoka huwa anaaga akaniambia nimfuatilie nione kama kweli huwa haendi kwenye vikao kwamba anaenda kwa familia.
Anaongeza "Kuna mwalimu mwingine alikuja hapa dukani kwangu kununua dawa nikamuonya nikamwambia wewe ni mmoja wapo unaechafua shule, alijitetea na kulaumu kwamba wanapotoa taarifa idara ya elimu kuhusu mkuu wa shule yote yanamrudia mkuu, akasema Mwenyekiti wewe hujui shida tunayoipata walimu" anasema Amon.
Kuhusu malalamiko kuwa mkuu wa shule ni dikteta hatoi uhuru wa mawazo kwa walimu kutoa hoja zao anasema " Nachokiona mkuu wa shule ana uwezo wa kuongea kujibu hoja hata kwa watu wengi haogopi, ukiita kikao cha wazazi, wazazi watakuja na mawazo mbalimbali anawashinda .
"Hata hao walimu huwa anawashinda, wote wanakuwa na magrupu yao wakikaa kikao cha pamoja mkuu wa shule anawashinda anajibu hoja zao na kuonekana kama hana kosa, sasa sijui ukweli halisi lakini naona makosa ya walimu yapo" anasema.
Mjumbe wa bodi ya shule Ibrahim Nyansiri anasema "Hili la mpasuko wa walimu siwezi kufahamu kama lipo wao wenyewe ndio wanajua maana hawajawahi kuleta lalamiko lolote kwenye bodi ili wajumbe wajadili" anasema.
Utata fedha za hosteli
Inaelezwa kwamba wanafunzi wanaokaa Hosteli wanalipa kwa mwaka Tsh. 600,000 lakini bodi ya shule, walimu hawajui pesa inayoingia wala matumizi yake huku wanafunzi wa hosteli wakitumia sehemu kubwa ya chakula cha wanafunzi wa bweni wa kidato cha tano na sita wanaolishwa na serikali.
Mwenyekiti huyo wa bodi ya shule anasema bodi ya shule haijui ni wanafunzi wangapi waliopo hosteli, uendeshaji wala mahitaji yake.
"Ukikaa na mkuu wa shule anasema pesa inanunua hiki na hiki pindi serikali inapokuwa imewacheleweshea pesa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita, pesa ya hosteli ndio inasaidia.
"Maelezo unaona kama yamejitosheleza lakini sasa kumbe walimu wengine wanahoji tofauti wanapopiga mahesabu wanaona kwamba pesa ni nyingi siyo pesa yote inayotumika" anasema.
Mjumbe wa bodi ya shule Ibrahim Nyansiri anasema "Hosteli ni kwa ajili ya wavulana wa kidato cha kwanza hadi cha nne na kwa kidato cha nne kwa wasichana. Kuhusu chakula huwa kinaunganishwa pamoja cha hawa wanaolipiwa na serikali pamoja na waliopo hosteli.
"Chakula kinapikwa pamoja sio kwamba wanafunzi wa hosteli wanakula chakula cha kidato cha tano na sita kinachogharamiwa na serikali huwa vyakula vinapikwa pamoja." anasema
Anaongeza "Mimi kinachonishangaza kama wanavyosema walimu kwanini mkuu wa shule anapanga mwenyewe mambo yote ya shule inamaana hakuna kamati nyingine inayoshughulikia? hakuna mwalimu wa idara husika?.
"Kwanini walimu wasikae vikao vya walimu waongee ni mvurugano sijui ni nani hawajibiki katika zile idara zao au vitengo vya walimu na sijui mkuu wa shule anakontroo vipi au amefeli!. Watu wanaweza dhani labda yanayoendelea shuleni ni siasa lakini sio siasa " anasema.
Michango ya walimu ya sayansi
Inaelezwa kwamba wazazi wamekuwa wakichanga fedha Tsh. 20,000 kwa ajili ya kuwalipa walimu wa kujitolea wa masomo ya sayansi tangu mwaka 2022 ambapo walimu watatu walipatikana na kuanza kufundisha. Baada ya mwaka mmoja 2023 walimu waliondoka na kubaki mwalimu mmoja anayelipwa mshahara 150,000 kwa mwezi ambaye nae mwezi uliopita ameondoka.
Mwenyekiti wa Bodi ya shule analizungumzia vipi jambo hilo la michango? "Kwenye kile kikao cha siasa kuna mwalimu alisimama akauliza hela mnazochanga ni za nini akasema hizo mnamchangia mtu , wazazi wakapiga makofi wengine wanapiga hadi na ukuta wakishangilia .
"Walimu wa kulipwa na wazazi walikuwa watatu walifundisha mwaka mmoja baadae mmoja aliacha mwaka umepita, mwingine nilisikia ameacha ila sijui aliondoka lini na mwingine ameacha ameondoka mwezi uliopita, malipo yalipungua .
"Wazazi walipouliza pesa wanazochanga zinaenda wapi wakati hakuna walimu, mkuu wa shule hakujibu kitu, wazazi wakasema kwanini pesa ya michango isipungue kwa kuwa mwalimu anayefundisha ni mmoja . Vikao vya shule huwa wazazi wanaitwa isipokuwa sisi kama bodi hatuitwi wala kushirikishwa kwenye vikao vya wazazi .
Mwenyekiti wa bodi anasema wazazi walimchagua mjumbe wa bodi ya shule Ibrahim Nyansiri kuwa mkusanyaji wa michango ya wazazi hivyo aulizwe yeye ndio ana majibu ya kiasi gani kinacholipwa kwa walimu hao wa sayansi na kiasi kinachochangwa .
Ibrahim anasema "Tulikuwa na walimu wa sayansi watano wa kujitolea waliokuwa wanalipwa na wazazi, waliondoka kwa awamu wengine wamepata ajira, wengine wameenda masomoni wakabaki watatu . Mwaka juzi aliondoka mmoja tukaleta mwingine.
"Mwaka jana mmoja alienda shule wakabaki watatu, mwaka jana mwezi wa tano mmoja akaondoka tukabaki na wawili tumefungua nao shule mwaka huu ila mmoja ameondoka tumebaki na mwalimu mmoja.
Anasema sababu ya walimu kuondoka ni muitikio mdogo wa wazazi kuchanga fedha kwa ajili ya walimu wa kujitolea, na kwamba wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne wapo 409 kati ya hao wanafunzi wanaotoa pesa ni kati ya 200 hadi 204 .
"Tulikuwa tunalipa walimu Tsh. 300,000 kwa mwezi baadae tukashindwa kuwalipa. Tukaulizana namna ya kuwalipa walimu wengine wakasema tuwalipe kulingana na viwango vyao vya elimu, mwenye diploma Tsh. 180,000.
"Mwenye digrii analipwa Tsh. 200,000 wengine wakiona ni ndogo wanalalamika wanaondoka tunatafuta wengine. Walimu waliokuwa wanalipwa na wazazi ni walimu wa somo la Biolojia na Kemia.
Anasema mbali na changamoto hiyo ya walimu wa sayansi pia kuna changamoto ya walimu wa somo la kingereza na kiswahili hali inayolazimu mwalimu mmoja kufundisha somo kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.
Bodi haishirikishwi nidhamu ya shule
Inaelezwa kwamba, kumekuwa na utaratibu wa mkuu wa shule kuwasimamisha wanafunzi kwenda kwao hasa wale wa A-level wakiwemo wanaokutwa na simu bila hata bodi ya shule kujua juu ya hatua hizo ambapo wakishatumikia adhabu wazazi wao huitwa shuleni na kuwatoza fedha kati ya Tsh 50,000 hadi 100,000 ili kulipa bili ya imeme na kwamba fedha hiyo huhesabiwa kama adhabu kwa mwanafunzi .
" Hivi karibuni kuna mwanafunzi wa kidato cha sita alikutwa na simu na mkuu huyo wa shule akamsimamisha kwa siku 4 na akaambiwa alipe Tsh. 50,000 kwa ajili ya umeme .
"Kuna wanafunzi watatu kidato cha sita wamerudishwa nyumbani juzi kwa kosa la kutokuwepo shule siku ya jumapili na kulala nje ya shule. Baada ya kurudi wamepewa adhabu ya kulipia umeme kuwaka bure bila kuutumia kiasi cha Tsh. 50,000 kila mmoja na adhabu ya visiki wanayoendelea kuifanya " anasema mwalimu mmoja.
Mwandishi wa DIMA ONLINE akiwa ameketi nje ya ofisi ya mkuu wa shule akisubiri kuingia ndani ili azungumze nae, nawaona baadhi ya wazazi nao wakiwa wanasubiri kuingia ndani kuonana na mkuu .
Nazungumza na mmoja ananieleza kwamba ameitwa na mkuu wa shule kwamba mwanae alitoroka shule siku ya wikendi kwenda nyumbani bila ruhusa .
Mzazi huyo anaonana na mkuu wa shule na kisha anatoka ndani na kuketi nilipokaa. namuuliza alichoelezwa. Anasema mkuu amemwambia asubiri nje kwasababu tayari kamati ya nidhamu imeshafanya maamuzi hivyo anasubiri ili kuambiwa maamuzi yaliyopitishwa na Kamati ya nidhamu.
Hali hiyo inanilazimu kumuuliza Mwenyekiti wa bodi ya shule taratibu zitumikazo pindi mwanafunzi anapofanya makosa ya kinidhamu. Anasema bodi ya shule ina kamati ya nidhamu lakini haishirikishwi .
" Bodi ina kitengo cha nidhamu na taaluma lakini hatushirikishwi, huwa tunasikia tu wanafunzi wamesimamishwa shule bila bodi kushirikishwa. Majuzi kwenye kikao cha kamati ya siasa nilisikia kwamba kuna wakati walimu wakichapa wanafunzi wanaenda kushitaki kwa mkuu wa shule.
" Walimu wanakosa uhuru wa kumwadhibu mwanafunzi . Sio jambo zuri mwanafunzi anaadhibiwa na mwalimu alafu anamzunguka na kwenda kushitaki kwa mkuu haiwezi kuleta amani shuleni. Mkuu anapokeaje hiyo taarifa kuna nini hapo ? hapo unaona kabisa kuna gepu kati ya mkuu na mwalimu anayetoa adhabu " anasema Amon .
Mjumbe wa bodi ya shule Ibrahim anasema bodi haijapewa taarifa ya wanafunzi watovu wa nidhamu na kwamba bodi inashirikishwa endapo mwanafunzi akifanya kosa litakalopelekea afukuzwe shule.
" Makosa ya kusimamishwa shule siku chache mkuu na mwalimu wa nidhamu ndio wanaoshughulikia. Sisi sio walimu wakati mwingine jambo linaweza kufanyika tusijue " anasema Ibrahim.
Miradi ya shule kutojulikana mapato
Inaelezwa kwamba, miradi ya shule kama vile mashine ya kusaga unga, mashamba, duka, saluni ya kunyoa nywele, miti ya shule imekuwa ikiendeshwa bila walimu, bodi ya shule kujua mapato na matumizi yake, hakuna ushirikishwaji wa walimu katika miradi hiyo.
" Kwakweli mimi kama Mwenyekiti wa bodi sijui mapato ya miradi, ukiona mashine ya kusaga inafunguliwa saa tisa au saa kumi jioni , bodi tulishauliza mnapata Tsh ngapi ? ukimuuliza anayesimamia mashine maana wanabadilishana badilishana anakwambia wanapata pesa kidogokidogo ya chai haizidi elfu 8,000 -10,000 .
" Ukimuuliza mkuu wa shule nae anakwambia muulize mhusika wa idara inabidi uwaache usiwabane maana wanasema wanapata pesa ndogondogo isiyozidi elfu kumi kwa siku na inaishia kwenye chai yao. Kwanini wasiajiri mtu wa kusimamia mashine ili ifanye kazi siku nzima! " anasema Amon .
Kuhusu mashamba ya shule kukodishwa kwa watu na kutojulikana mapato huku walimu wakikosa mashamba ya kulima Mwenyekiti huyo wa bodi anasema " Hilo la mashamba ya shule kukodishwa kwa watu mimi hilo ndo nalisikia kwako halijawahi kuletwa kwenye bodi na sijui wanavyogawana huko" anasema.
Uuzaji wa miti ya shule
Inaelezwa kwamba mkuu huyo wa shule amekuwa akikata miti ya shule kwa kushirikiana mwenyekiti wa bodi ya shule, Amon Wambura na Marwa Wambura maarufu Marwa Meneja ambaye ni ndugu wa Mwenyekiti wa bodi, ambapo hupasua mbao ambazo huuzwa kwa watu mbalimbali bila uongozi wa shule kushirikishwa .
Mwenyekiti huyo wa bodi ya shule anafafanua " Jamani kuna watu wanadonoa vitu ambavyo vipo nje , tumewahi kujenga choo cha wasichana, barua ilikuja kwamba wananchi wachangie nguvu kazi , choo kilikuwa kimejaa kinaleta aibu.
" Kwenye mikutano ya Kijiji walisema shule hiyo ni kubwa ina mpaka kidato cha sita ina bajeti yake serikalini hivyo hawawezi kujenga choo. Tulikaa bodi tukasema tutumie kile tulichonacho miti ikaangushwa ikauzwa tukapata fedha shimo likachimbwa kwasababu bajeti tuliyokuwa tumepewa ilikuwa ndogo choo kikajengwa kikakamilika"
" Wanakijiji wanasema miti ya shule imeisha wakati miti inapandwa na wanafunzi kwa ajili ya matumizi ya shule . Safari hii wameangusha miti bodi hatukushirikishwa mkuu wa shule ndio anaweza kuitolea majibu vizuri japo nilisikia kwamba kuni zilileta shida mzabuni anayeleta kuni shuleni alichelewa kuleta kuni ikabidi miti ikatwe" anasema Amon.
Marwa Wambura maarufu Marwa Meneja anayetuhumiwa kuuziwa miti ya shule na mbao anakanusha kuhusika " Nani huyo aliyesema mimi nimeuziwa miti ya shule na mkuu wa shule ? Mungu aliye mbinguni ananisikia ninachokiongea. Mimi sijawahi kununua miti au mbao za shule , mimi sina cheo shuleni nawezaje kujua kuwa kuna miti inauzwa shuleni na niuziwe kama nani.
" Amon Mwenyekiti wa bodi ndiye awaambie ukweli nani alinunua mbao sio mimi uliza watu watakwambia mimi simo humo hata wanapouziana mimi sijui natamani na mimi nivipate lakini siambiwi, Amon ni mchungaji hawezi kusema uongo akikwambia ana kwambia ukweli muulize akwambie ukweli" anasema.
Kauli ya Mwenyekiti wa kijiji
Mwenyekiti wa Kijiji cha Magoto, Zabron Magabe Kimori akizungumzia kuwepo makundi ya walimu shuleni anasema " Kuna changamoto pale shuleni wapo walimu ambao wapo upande wa mkuu wa shule na wapo ambao mkuu wa shule hayuko nao ndio maana lile kundi lingine likaamua kusema changamoto zao kwenye kikao cha kamati ya siasa ya CCM.
" Kuna mwalimu mmoja aliongea mambo mengi ambayo mengi ndio nimeyasikia kwa mara ya kwanza. Alisema kwamba kero zimekuwa nyingi moyoni bora amepata nafasi aziseme nikajiuliza sasa mbona hakuwa ametuambia sisi viongozi wa serikali ya Kijiji?
" Changamoto aliyonayo mkuu wa shule ni ushirikishaji kama mkuu ndio anaenda kununua vifaa vya shule wakati kuna walimu husika wa vitengo ni tatizo. Najiuliza wanafunzi wanalipa michango ya walimu kufundisha masomo ya sayansi alafu walimu hakuna sasa pesa hizo zinaenda wapi? Sisi tulikuwa hatujui kama walimu hawapo nilifahamu siku ya kikao kumbe walimu wanaolipwa pesa na wazazi hawapo" anasema.
Anaongeza kusema " Mwalimu aliyelalamika kikaoni hana mahusiano na walimu , walimu wakuu wanaofika hapo huwa wanamuandikia taarifa mbaya, yeye ndio hana ushirikiano na walimu wenzake .Angekuwa na mahusiano mazuri zile changamoto asingezisema kwenye kikao angezipeleka kwa uongozi wake wa juu.
" Walimu wote wanaofika lazima awe na migogoro nao. Kuhusu changamoto za shule ikiwemo michango, fedha za hosteli sikuwa nafahamu, siku ya kikao mambo mengi yaliibuka ambayo hata mimi sikuwa nayafahamu" anasema Mwenyekiti wa Kijiji .
Wasemavyo wananchi, wazazi
DIMA Online ikiwa Kijiji cha Magoto imezungumza na baadhi ya wananchi, wazazi na wanafunzi kama wanafahamu uwepo wa changamoto hizo na maoni yao. Wengi wao wakaishauri serikali kumwamisha mkuu wa shule kutoka na tuhuma zinazoelekezwa kwake pamoja na walimu waliokaa kwa miaka mingi shuleni.
Joseph Chacha mkazi wa Magoto anasema " Kuna walimu wamekaa kwenye hii shule miaka mingi hadi wamekuwa wenyeji wa shule kupita kiasi , tunaomba serikali ya Rais Samia imhamishe mkuu wa shule na walimu waliokaa muda mrefu .
" Shule ya Magoto sekondari ina historia ya kuchafuka mara kwa mara, kuna mwaka fulani walimu waliwashawishi wanafunzi mpaka wakaandamana mara mbili kwa mguu kwenda kwa mkuu wa wilaya Tarime mjini wakilalamikia changamoto za shule.
" Unafuu ni kuwatawanya walimu wote waje wapya maana unaweza kumwamisha mkuu alafu umewaacha walimu wasumbufu wanaochafua wenzao, walimu watakao kuja nao itakuwa hivyo hivyo maana alishakuja mkuu wa shule wakasema mbaya akahamishwa akaja huyo aliyepo nae wanasema ni mbaya .
" Kuna walimu wawili ndio wanasumbua, amekuja mwalimu mgeni hivi karibuni lakini na yeye ameingia kwenye kundi ambalo linapingana na mkuu, kwahiyo hata mkuu wa shule akiondoka bila kuwaondoa wale walimu wawili kwa majina nawahifadhi vurugu itaendelea ila wanajulikana maana ndio walalamishi kila leo" anasema Joseph.
Mwananchi mwingine Peter Marwa anasema " Mimi kwanza nashangaa hii shule wakati wa mahafali mkuu wa shule analeta wageni rasmi ambao hata hawana uwezo mkubwa wa kielimu . Kwanini mkuu wa shule kwenye mahafali analeta wageni rasmi watu wa chini wakati ni shule kongwe na kubwa wanatuleta mgeni rasmi hadi bodaboda shule yenye kidato cha kwanza hadi cha sita.
" Tulitarajia kwakuwa shule hii ina kidato hadi cha sita tungewaona wageni rasmi viongozi wa serikali kama vile afisa elimu ili hata wanafunzi wanaposoma risala yule mtu wa serikali anaijibu au kama ni kiongozi wa siasa anasikiliza alafu anawasilisha kwenye vikao vya chama kisha serikalini.
" Sasa mkuu wa shule analeta wageni rasmi watu wa kawaida ambao hata elimu yao ni ndogo. Hivi mwendesha pikipiki atatatua vipi changamoto zinazoelezwa kwenye risala ! mkuu wa shule anaogopa nini kualika viongozi wa juu wa serikali kwenye mahafali " anahoji.
Ghati John anasema " Walimu wana haki kueleza changamoto zao , eti kuna viongozi wanalalamika kwamba kwanini walimu walienda kulalamika kwenye kikao cha CCM badala ya kwenda kwa viongozi wao wa serikali. CCM nako ni sehemu sahihi ya kila mtu kulalamika maana ni serikali ya CCM . Chamsingi changamoto zilizoelezwa zitatuliwe.
Mwanafunzi katika shule hiyo jina linahifadhiwa anasema " Kuna mwalimu anatufundisha somo la historia na uraia kidato cha sita, huyu mwalimu haelewani na mkuu wa shule hata ofisi amejitenga anakaa peke yake hata chai hanywi pamoja na wenzake.
" Wanasema kwamba mwalimu huyo aliwahi kupata ajali hivyo kuna wakati ubongo wake huwa unamtaka kusema ukweli yaani uhalisia wa mambo, na akisema jambo ujue ni la kweli. Wanamchukia na kumuona mkorofi kwasababu anasemaga ukweli, jambo analoliona liko tofauti analisema hafichi " anasema.
" Kuhusu adhabu mwanafunzi mmoja anasema " Ukifanya kosa mkuu anakufukuza unaambiwa umesimamishwa shule siku kadhaa ambazo hazizidi wiki na unaporudi unakuja na mzazi wako anaonana na mzazi kisha anaambiwa alipe fedha atakayoona yeye kati ya Tsh. 50,000 hadi 100,000 kama adhabu ya mwanafunzi kurudishwa shule.
" Sijawahi kusikia kwamba amemfukuza mwanafunzi ila anawafukuza siku chache zisizozidi waki moja . Wanasema yeye huwa hafukuzi mwanafunzi hata kama amefanya kosa kubwa kwasababu kuna fedha inayotolewa na serikali akiwafukudha idadi itapungua kwahiyo anakuwa anacheza kwenye adhabu za kusimamishwa kwa siku chache kisha mzazi anakuja anatoa pesa mwanae anaendelea na masomo " anasema.
Mzazi mwingine anasema " Sijajua serikali inapompandisha mwalimu cheo cha ukuu wa shule huwa ni vigezo gani vinavyotumika kama mkuu wa shule anashindwa kuwaunganisha walimu wawe kitu kimoja ni hatari inaweza pelekea kushuka kwa taaluma maana hamu ya ufundishaji itapungua na migogoro itaongezeka kila mara" anasema.
Mkazi wa mjini Tarime jina linahifadhiwa anakiri kwamba miti ya shule ya sekondari Magoto imekuwa ikiuza miti ya shule mjini Tarime " Hapo shule ya sekondari Magoto tumechanapo mbao sana, wameuza mbao sana za mamilioni. Shule imeuza mbao kwa wauza mbao wa Tarime mjini.
" Hukuona visiki vya miti iliyokatwa kwa mashine ? miti ya kuchipua ni rahisi sana kutambua . Mimi nimechana mbao hapo mwaka 2021-2023, sisi kazi yetu ilikua ni kuchana wao wanawauzia mbao wa Tarime mjini. Hao waliowaibia siri kuwa shule inauza miti walisahau kukwambia ukiwa unaingia au kutoka uangalie visiki" anasema.
Kauli ya mkurugenzi
Mwandishi wa DIMA Online akafunga safari hadi ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, Solomon Shati kufahamu nini anachokijua juu ya tuhuma zinazoelekezwa kwa mkuu wa shule ya sekondari Magoto
Mkurugenzi huyo alipoulizwa kama anazifahamu changamoto za shule hiyo kama alivyoelezwa na Mwandishi wa habari zikiwemo tuhuma zinazomhusu mkuu wa shule anasema hana taarifa yanayoendelea shuleni.
" Sifahamu yaliyozungumzwa kwenye kikao cha kamati ya siasa, mtendaji kama alikuwepo ndio alitakiwa aniletee hiyo taarifa ya kikao maana mimi sina taarifa ya hicho kikao kilichojadili changamoto za shule .
" Ishu ya malalamiko ya mwalimu mpaka nijue je afisa elimu aliyekwenda huko anafahamu? je amechukua hatua gani ? . Nipe muda nifuatilie taarifa hizo na hao walioshiriki niwatake waniletee hizo taarifa ili niweze kujiridhisha na lazima mimi niende nikachunguze.
" Kabla ya mimi kwenda nitatuma watu tofauti kabisa kwenda kufanya upelelezi kujua nini shida . Kikao cha WDC bila mimi kupata mhitasari wake ni ngumu na taratibu haziniruhusu " anasema Mkurugenzi.
Anaongeza kusema " Ili niichukue hatua za kikao cha WDC mpaka taarifa ya WDC ije ndio itakuwa imeainisha yote ndio sasa nitaichambua, ila kabla ya taarifa mengine yanaweza kuwa ni umbea na sisi kama viongozi hatufanyii kazi umbea, nitatuma watu wataenda wakawasikilize walimu na wamsikilize mkuu wa shule kujua je kinachosemwa ni sahihi?
"Mfano pale Sirari ilitokea shida kituo cha afya, mimi nikafikiri ni watumishi yakasemwa mengi kufuatilia kumbe ni mtu mmoja, nilipomchomoa saizi Sirari pametulia, nitatuma timu ya maafisa utumishi wakafuatilie huko Magoto.
Kuhusu utaratibu wa wajumbe kulipwa posho ya vikao kama ilivyoulizwa na Mwenyekiti wa bodi kuwa zamani walipokaa kikao cha bodi walikuwa wanalipwa posho za vikao Tsh. 60,000 lakini kwa sasa hakuna posho. Mkurugenzi huyo akasema kwamba hana uzoefu juu ya posho kwa wajumbe wa bodi na akaahidi kufuatilia.
Mwandishi wa chombo hiki cha habari alimuomba mkurugenzi huyo kibali ili akazungumze na mkuu wa shule juu ya tuhuma zinazomkabili , lakini pia azungumze na afisa elimu sekondari halmashauri hiyo juu ya malalamiko kwamba idara ya elimu haitunzi siri za walimu wanapopeleka kero zao kwani yote wakiyasema huwafikia wahusika na hivyo kuwatambia.
Mkurugenzi Solomon akakataa na kusema kuwa yeye ndio msemaji wa Taasisi hivyo haitowezekana kumuhoji mkuu wa shule na afisa elimu sekondari halmashauri ya wilaya hiyo.
Hata hivyo , siku ya ijumaa , Aprili, 4, 2025 timu kutoka ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ikafika shule ya sekondari Magoto na kukutana na watumishi wakiwemo walimu na bodi ya shule na kuweza kusikiliza kero zao.
Post a Comment