SHAIRI : WAFANYIWE KISHETANI
Ni matendo ya shetani, kutesana duniani,
Hata wewe uwe nani, kutesa ni ushetani,
Uzaliwe rangi gani, utesaji uhaini,
Kama wewe mtesaji, swahiba wako shetani.
Wapo watu duniani, wajiona wa thamani,
Koo zao za nyumbani, na vyeo vyao kazini,
Wajiona kileleni, na wengine wote ni duni,
Kama wewe mtesaji, swahiba wako shetani.
Pengine unayo dini, au hata huna dini,
Wengine wawafitini, kuwaona wako chini,
Kuua huoni soni, hadharani mafichoni,
Kama wewe mtesaji, swahiba wako shetani.
Ulivyofanya zamani, hujatubu hekaluni,
Bado uko kitabuni, mshirika wa shetani,
Iwe ule ukoloni, bado uko kitabuni,
Kama wewe mtesaji, swahiba wako shetani.
Uliua zetu dini, kisema za mashetani,
Kumbe wewe ni haini, umejaa ushetani,
Unatufundisha nini, haki wewe uso dini?
Kama wewe mtesaji, swahiba wako shetani.
Ulitutesa zamani, utesaji u damuni,
Hujenda madhabahuni, kutubu kwa goti chini,
Unabakia shetani, unapopita njiani,
Kama wewe mtesaji, swahiba wako shetani.
Tulivyouzwa sokoni, kuburutwa baharini,
Na shokoa ugenini, kama wanyama mwituni,
Kama siyo ushetani, basi hayuko shetani,
Kama wewe mtesaji, swahiba wako shetani.
Unatamba duniani, sasa uko kileleni,
Wakati yetu madini, wanunua bei chini,
Unatutia vitani, ukivuna migodini,
Kama wewe mtesaji, swahiba wako shetani.
Eti ainuke nani, akitamba duniani?
Msemaji wetu nani, atamke hadharani,
Unamuita mhuni, na tena huyo haini,
Kama wewe mtesaji, swahiba wako shetani.
Malcolm, Luther Martin, Lumumba liwafitini,
Sankara, Samora ndani, nao mlipiga chini,
Na Steve Biko jamani, shujaa wetu kusini,
Kama wewe mtesaji, swahiba wako shetani.
Haya maneno madini, tena faraja moyoni,
Malipo ni hapa chini, tukiwapo duniani,
Walifanya kishetani, wafanyiwe kishetani,
Kama wewe mtesaji, swahiba wako shetani.
Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment