HEADER AD

HEADER AD

MADA ZILIZOWASILISHWA NA WAANDISHI WA HABARI MRPC ZAMKOSHA DC TARIME


> Afurahishwa kuona Waandishi wa Habari wakifundishana

>>Baadhi ya Waandishi wa Habari watunukiwa vyeti , zawadi .

>> Wanachama wampatia zawadi Mwenyekiti MRPC, Jacob Mugini

Na Ada Ouko, Tarime

MKUU wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele amevutiwa na Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Mara, baada ya kuona miongoni mwa wanachama wakiwasilisha mada ya matumizi ya akili mnemba, usalama wa mtandaoni na umakini katika kuripoti habari za uchaguzi.

Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa amefurahi sana kuona baadhi ya waandishi wa habari wana vipaji tofauti tofauti kwa kuwasilisha mada kwa waandishi wenzao pasipo kutegemea kutoa wakufunzi nje ya Klabu hiyo.

Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele akizungumza na Waandishi wa habari mkoa wa Mara ,wakati wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari mkoani humo, kushoto ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Mara , Jacob Mugini, kulia ni Katibu wa Chama hicho, Pendo Mwakembe.

" Nimefurahi sana kuona kuna watu humu wana vipaji tofauti tofauti, kumbe kuna mpaka walimu humu, wataalam wa fani zingine . Hii inatusaidia sisi kwa pamoja " amesema DC Gowele.

Ameongeza kusema " Nimefurahi kuona mnafundishana hiyo AI , Dinna nilikuwa nakuona mdogomdogo kumbe una mambo makubwa hongera sana " amesema DC wakati akimkabidhi Dinna bahasha yenye fedha kama zawadi iliyotolewa na Mwenyekiti MRPC.

Mkuu huyo wa wilaya mbali na mafunzo ya Akili Mnemba, ameushauri uongozi wa Chama hicho kutafuta wataalam ili wawafundishe wanachama Akili Hisia ( Emotional Intelligence ).

Mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele akimkabidhi cheti cha Pongezi Mwandishi wa Habari wa DIMA Online , Dinna Maningo wakati wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari yaliyofanyika Mei, 23, 2025 mkoani Mara.

" Kwasababu mnafanya kazi na jamii, mnajihusisha na jamii itakuwa vizuri mno mkitafuta mtaalam aje awafundishe Emotional Intelligence (Akili Hisia) , lakini mpaka hapa nimefurahi sana" amesema DC .

Amempongeza Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Mara,Jacob Mugini na uongozi wa Chama kwa ujumla kwa kuwatunuku vyeti baadhi ya waandishi wa habari kutokana na mchango wao mkubwa kwa maendeleo ya Klabu.

      Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele akimkabidhi Zawadi Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Mara, Jacob Mugini iliyotolewa na wanachama wakimpongeza kwa kuchapa kazi katika Klabu hiyo.

Pia kuwapa zawadi ya fedha kwa wawasilishaji wa mada waliotoa elimu na wengine kutunukiwa vyeti vya pongezi kwa kujitoa kwa ajili ya maendeleo ya Klabu kama motisha lakini pia wanachama kuonesha upendo kwa Mwenyekiti kwa kumpatia zawadi kutokana na juhudi zake na kujituma katika kukitumikia chama.

Mwenyekiti wa Chama hicho cha Waandishi wa Habari mkoani humo, Jacob Mugini, amesema kwamba yeye na kamati tendaji wameamua kutoa zawadi ili kuwapa motisha waandishi wa habari kutokana na mchango wao katika maendeleo ya chama.

    Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Mara, Jacob Mugini akizungumza wakati waaadhimisho siku ya uhuru wa vyombo vya habari ambapo chama mkoani huo kimeadhimisha , Mei, 23, 2025.

" Hatukutoa wawezeshaji nje ya wanachama kuzungumzia matumizi ya akili mnemba ambayo ni kauli mbiu ya siku ya uhuru wa habari, tumewachukuwa wanachama waliopata mafunzo mbalimbali na wamewasilisha mada zao.  

" Tumethibitisha kuwa Mara Press Club ina watu ambao inaweza kuwatumia kutoa mafunzo kwa wenzao. Dinna kafafanua faida na hasara na jinsi gani mtu anaweza kupotosha taarifa na kuonesha ni jinsi gani anaweza kufahamu kama taarifa hiyo ni ya kweli au ni ya uongo na chanzo ilipotokea.

"  DC siku moja ukitaka watu wa ofisini kwako kufundishwa AI, Dinna anaweza akawaelimisha vizuri kabisa yaani huwezi kuamini aliyetoa mafunzo haya anatokea Tarime.

" Tumetoa zawadi na vyeti kwa baadhi wenye moyo wa kusaidia wengine ambao wana mchango mkubwa kwa maendeleo ya Klabu" amesema Jacob.

Pia amewashukuru wadau mbalimbali waliochanga fedha kufanikisha maadhimisho hayo wakiwamo kampuni ya BARRICK, WARACHA, PKM, STANLEY, MAMA LEAH, CMAG, NBA, KEMANYANKI, aliyewahi kuwa mbunge mstaafu Jimbo la Tarime Nyambari Nyangwine pamoja na Katibu mkuu Wizara ya Katiba na Sheria , Eliakim Maswi. 

Mwandishi wa habari ambaye pia ni mmiliki wa chombo cha habari cha Mtandaoni DIMA Online, Dinna Maningo aliwasilisha mada iliyohusu faida na hasara za matumizi ya akili Mnemba (Artificial Intelligence).

   Mwandishi wa Habari Dinna Maningo, akitoa elimu ya matumizi ya akili Mnemba wakati waandishi wa habari wakiadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari.

" Kupitia matumizi ya akili Mnemba inakuwezesha kufahamu taarifa/ habari, picha za upotoshaji na mahali ilipotokea kupitia Tovuti ya Google Lens, Akili mnemba inakuwezesha wewe kuingiza taarifa za tukio fulani na kukuonesha picha halisi za tukio fulani hata kama haupo eneo la tukio.

" Matumizi ya akili Mnemba yanakuwezesha kutambua taarifa ya zamani ambayo imepotoshwa na kuonekana kuwa ni tukio ambalo limetokea sasa pamoja na mambo mengine " amesema Dinna.

Ameeleza kuwa matumizi ya akili mnemba wakati mwingine yana athari kwani yanasababisha mtu kutokuwa mbunifu na badala yake kila jambo kutegemea msaada wa akili mnemba.

       Mwandishi wa habari wa DIMA Online, Dinna Maningo, akimwelekeza Mwandishi wa habari gazeti la Mwananchi, Beldina Nyakeke ( kushoto) namna ya kugundua  picha bandia .

Ameongeza kuwa akili mnemba inaweza kutengeneza matangazo bandia kwa kutumia nyaraka za serikali au shirika huku akisisitiza umakini zaidi kwa mwandishi wa habari au muhariri atakaetumia akili mnemba kwenye kazi zake .

Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Majira na Dira Makini, Fresha Kinasa amewasisha mada ya usalama mtandaoni (Digital Security), amesema kuwa usalama mtandaoni ni hali ya mwandishi wa habari, vifaa vyake vya kazi na ujumbe anaoutoa kwa jamii vyote kwa pamoja kuwa katika hali ya usalama.


Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Edward Gowere akitoa zawadi kwa Mwandishi wa habari, na Mwanachama Cha Waandishi wa Habari(MRPC) Fresha Kinasa.

" Mwandishi wa habari katika kazi zako taarifa unazotoa kwa umma hakikisha ziko salama kwa maana ya wewe binafsi, vifaa vyako vya kazi kama kamera, simu na kompyuta, endapo kompyuta yako haina usalama ni rahisi mtu kuiba taarifa zako" Amesema Fresha .

Ameeleza kuwa ili mwandishi wa habari na vifaa vyake vya kazi kuwa salama kwanza anapaswa kutopenda kuchangia Nywila hata na mtu anayemfahamu, pia kuacha tabia ya kujihusisha na (Wi-Fi) katika eneo lenye watu wengi wanaomzunguka, kwani ni rahisi taarifa, habari huweza kudukuliwa.

Mwandishi wa Jambo T V, Helena Magabe, ameeleza mafunzo aliyoshiriki yalikuwa yanahusu umakini katika uandishi wa habari za uchuguzi, hasa ikizingatiwa serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi mkuu utakao husisha Madiwani, Wabunge na Rais.

      Mwandishi wa habari Helena Magabe akionesha Jaketi ambalo Mwandishi wa habari anatakiwa kuvaa hasa wakati wa chaguzi kama utambulisho .

Helena amewaeleza wanachama na wasiowanachama wa MRPC katika kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika octoba, 2025, Mwandishi wa habari haruhusiwi kuajiriwa na mgombea vinginevyo anapaswa kuacha kazi ya uandishi wa habari.

"Tumetakiwa kupitia tena sheria zilizopo sambamba na hilo kipindi cha uchaguzi tunapaswa kujali usalama wetu kwa maana ukihisi upotevu wa amani eneo la tukio chukua tahadhari kwa kuondoka haraka eneo hilo" Amesema Helena.

Waandishi wa habari waliopewa vyeti vya pongezi ni Ghati Msamba n Dinna Maningo, na wawezeshaji wa mada waliopewa fedha kama motisha ni Dinna Maningo, Helena Magabe na Fresha Kinasa.

        Mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele akimkabidhi cheti cha pongezi Mwandishi wa habari wa gazeti la uhuru ,Ghati Msamba kilichotolewa na uongozi wa Chama kama kutambua mchango wake ndani ya Klabu hiyo.

Kauli ya Waziri Mkuu

>> Rejea 

Katika Maadhimisho ya vyombo vya habari Duniani, ambayo kitaifa yalifanyika mkoani Arusha, Aprili ,2025 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa wito kwa waandishi wa habari nchini kutumia akili mnemba , kama nyenzo ya kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo na sio kikwazo cha uhuru wao.

Alisema katika Dunia ya sasa , vyombo vya habari vinakutana na changamoto mpya zinazotokana na maendeleo ya teknolojia, ambapo akili mnemba inachukua nafasi kubwa katika uzalishaji na usambazaji wa Habari.

Waziri mkuu aliongeza kuwa serikali inaendelea kuandaa sera maalum ya akili Mnemba ambayo itatoa mwongozo wa matumizi yake katika vyombo vya habari ili kuhakikisha kuwa teknolojia hiyo inaendana na misingi ya uhuru wa vyombo vya habari kwani inatumika katika mfumo wa uchakataji wa habari kuanza, kukusanya, kuchakata na uchapishaji.

Waziri wa Habari, Uatamaduni, Sanaa na Michezo , PROFESA Palamagamba Kaburu akiwa kwenye maadhimisho hayo alisema akili mnemba isiwafanye waandishi wa habari nchini wakafubaa na badala yake wahakikishe wanaitumi vizuri katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kila Mwezi, Mei, 3 ya kila mwaka Dunia uadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari  Duniani ambapo kauli mbinu ya mwaka 2025 inasema ' Athari za akili Bandia kwa uhuru wa vyombo vya habari na Tasnia ya Habari' .

Mwandishi wa Habari wa DIMA Online akitoa elimu ya matumizi ya akili mnemba.




          Mkuu wa wilaya  ya Tarime Meja Edward Gewele akimpongeza  Mwandishi wa habari wa Jambo TV , kulia ni Katibu wa Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Mara, Pendo Mwakembe.

















Picha zote ni waandishi wa habari , wadau wa habari wakiwa katika maadhimisho ya siku ya uhuru Duniani ambapo chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Mara wameadhimisha wilayani Tarime, Me, 23, 2025.

No comments