MAFANIKIO SAFARI
MAFANIKIO safari, tena huwa mchakato,
Wafanikiwa wakiri, kwamba yanayo mapito,
Bila ya kuwa ngangari, huwezi pata kipato,
Hakuna njia mkato, kupata mafanikio.
Yale unayatamani, upate bila majuto,
Lazima wende kazini, kwenye baridi na joto,
Kuyatia kibindoni, mwili upate fukuto,
Hakuna njia mkato, kupata mafanikio.
Waenda ngazi kwa ngazi, siyo njia za mkato,
Lazima kufanya kazi, jasho pia msoto,
Tena mema maamuzi, kulia au kushoto,
Hakuna njia mkato, kupata mafanikio.
Wenda harakaharaka, mali iwe kama puto,
Vivyo hivyo wanachoka, waudurie msoto,
Vile njia za mashaka, zinazoleta majuto,
Hakuna njia mkato, kupata mafanikio.
Wizi rushwa ujambazi, haramu hicho kipato,
Wapate za matanuzi, wakikamatwa majuto,
Ila kwa mchapakazi, halali chako kipato,
Hakuna njia mkato, kupata mafanikio.
Bidii unayoweka, kwa kazi siyo kwa lotto,
Taratibu tainuka, utimize zako ndoto,
Jinsi ulichokachoka, mara wapata mvuto,
Hakuna njia mkato, kupata mafanikio.
Uvivu hivyo vijiwe, kurusharusha kokoto,
Na mipira ishangiliwe, wanakopata kipato,
Akili ifunguliwe, kama hutaki msoto,
Hakuna njia mkato, kupata mafanikio.
Chimba yake Bakhresa, kilikotoka kipato,
Hiyo ikupe hamasa, usizembee kitoto,
Mkonosio kinasa, tazidi saka mapato,
Hakuna njia mkato, kupata mafanikio.
Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagh@gmail.com 0767223602
Post a Comment