MITARA NI NINI

MITARA ni mila gani, nijuzeni wahisani,
Nami nataka baini, wasiwasi nitoeni,
Majibu nipatieni, yenye vina na mizani,
Mitara ni mila gani nami nataka bayana.
Hili neno siyo geni, linanichoma moyoni,
Asili yake ni nini, ndugu nifahamisheni,
Maana sijabaini, moyo wangu mashakani,
Mitara ni mila gani nami nataka bayana.
Si leo tangu zamani, mitara limeshehini,
Faida yake ni nini, tafadhali nijuzeni,
Nauliza kwa huzuni, msifikiri utani,
Mitara ni mila gani nami nataka bayana.
Imani yangu ni duni, kusema si mshindani,
Majibu nitumieni, andikeni kiundani,
Wajuzi jiridhisheni, mboni zangu fumbueni,
Mitara ni mila gani nami nataka bayana.
Wadau niteteeni, msiniache njiani,
Gizani niondoeni, mwangani nipitisheni,
Nishikeni mkononi, salama nifikisheni,
Mitara ni mila gani nami nataka bayana.
Naelekea mwishoni, rafiki nawathamini,
Kujua ninatamani, fumbo nifumbulieni,
Semeni kwa umakini, kiswahili tumieni,
Mitara ni mila gani nami nataka bayana.
Mtunzi ni Sirdody - Kilimanjaro
0675654955 au 0762396923
Post a Comment