MIRUNGI KWETU HARAMU
MIRUNGI hiyo kilevi, siyo vema kutumia,
Wakulima na wavuvi, nyote ninawaambia,
Kutumia sasa hivi, mwataka kuangamia,
Mirungi kwetu haramu, ni madawa ya kulevya.
Alivyosema Sidory, na mimi ninajazia,
Ni kweli siyo stori, mirungi kukatazia,
Tuweze kwenda vizuri, pasi hata kusinzia,
Mirungi kwetu haramu, ni madawa ya kulevya.
Mirungi ishatangazwa, katika yetu dunia,
Mimea inakatazwa, inalevya sikia,
Madhara yakielezwa, mlaji ajipatia,
Mirungi kwetu haramu, ni madawa ya kulevya.
Ukitafuna miraa, gonjwa wajipalilia,
Mwilini waweza kaa, ubaki walialia,
Kutumia we kataa, salama utabakia,
Mirungi kwetu haramu, ni madawa ya kulevya.
Ni vidonda vya tumbo, inakusababishia,
Hilo wazi siyo fumbo, gomba ukilitumia,
Kukataza huu wimbo, vema ukakuingia,
Mirungi kwetu haramu, ni madawa ya kulevya.
Hizo nguvu za kiume, chini zinapukutia,
Hilo vema ulisome, kuilinda familia,
Siyo mke alalame, kukosa mridhishia,
Mirungi kwetu haramu, ni madawa ya kulevya.
Miraa ukitumia, madhara mengi sikia,
Choo unajifungia, taabu inavyoingia,
Shida ya kujitajia, mirungi ukitumia,
Mirungi kwetu haramu, ni madawa ya kulevya.
Ini utendaji kazi, chini unadidimia,
Meno rangi kama gunzi, yavyojibadilikia,
Kupungua usingizi, na huko kutakujia,
Mirungi kwetu haramu, ni madawa ya kulevya.
Hafu mbaya mdomoni, hiyo yaweza kujia,
Hata fizi mdomoni, zinauma waumia,
Utendaji wawa chini, sikia nakuambia,
Mirungi kwetu haramu, ni madawa ya kulevya.
Mama kama watumia, athari zinaingia,
Mtoto kijizalia, maziwa tayakimbia,
Hatataka kutumia, ladha mbaya kubugia,
Mirungi kwetu haramu, ni madawa ya kulevya.
Uraibu wa mirungi, ni mbaya nakwambia,
Jambo bora la msingi, ni kuacha kutumia,
Madhara tajwa ni mengi, wala hayatakujia,
Mirungi kwetu haramu, ni madawa ya kulevya.
Kama wewe watumia, na kujisafirishia,
Ni mkono wa sheria, mara utakufikia,
Wakukutia hatia, lupango utaishia,
Mirungi kwetu haramu, ni madawa ya kulevya.
Mtunzi wa Shairi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment