PAKULALA PAWE SAFI
KWELI maisha popote, hata riziki popote,
Mwingine mwache apite, akuache uzichote,
Kwako huo ni ubwete, hata watu wakukute,
Ndoa na iheshimiwe, pakulala pawe safi.
Kwa mahusiano yote, unapokwenda popote,
Kwenye ndoa watu wote, pakulala ndiyo pete,
Kuvaliana ukute, wawili ni yao pete,
Ndoa na iheshimiwe, pakulala pawe safi.
Hasa wanaume wote, walovalishana pete,
Kwa wenzi wao popote, wataka heshimu pete,
Wafanyiane yoyote, sio kuivunja pete,
Ndoa na iheshimiwe, pakulala pawe safi.
Mtu akivaa pete, ni wa ndoa na apite,
Fanya naye mambo yote, wala usiguse pete,
Waume wengi kwa pete, hawataki itepete,
Ndoa na iheshimiwe, pakulala pawe safi.
Wale wajuao wote, kwamba mtu ana pete,
Wataka wamuokote, kitandani wakapete,
Hao wakutema mate, mbali na wewe wapite,
Ndoa na iheshimiwe, pakulala pawe safi.
Na waliovaa pete, wanusa nusa kokote,
Waje kwako wakukute, kutaka myale mate,
Kwa mbali uwapepete, waende kucheza kete,
Ndoa na iheshimiwe, pakulala pawe safi.
Ukishavalishwa pete, nawe kuvalisha pete,
Wengine wote wafute, wewe ufungwe na pete,
Waache nao wapate, wakufunga nao pete,
Ndoa na iheshimiwe, pakulala pawe safi.
Huyo amevaa pete, shem hiyo usikate,
Vipi wewe yakukute, mwingine wako achote?
Katulie utakate, kwako usipitepite,
Ndoa na iheshimiwe, pakulala pawe safi.
Akuchekea na pete, yaonekana popote,
Cheka na asikuchote, uvunje ahadi pete,
Akikitaka kipute, dimbani asikukute,
Ndoa na iheshimiwe, pakulala pawe safi.
Waliooana wote, ni mwili mmoja wote,
Kula wanakula wote, kulala walala wote,
Wamejifunga kwa pete, hadi kifo kiwakate,
Ndoa na iheshimiwe, pakulala pawe safi.
Mtunzi Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment