FITINA ZA MAJIRANI

FITINA za majirani, kwako hazitatimia,
Hata wakiwa sitini, watakuja kuzimia,
Ukweli ule sirini, kweupe watasikia,
Akuchomae usiku, aadhirike mchana.
Yale mambo kitabuni, wewe unayajulia,
Na ufanisi kazini, kwako umeshatimia,
Mtu toka kijijini, kwani akuchafulia?
Akuchomae usiku, aadhirike mchana.
Usiumie moyoni, jungu walokupikia,
Japo lagusa kwa ndani, litakuja kuishia,
Washitaki yao soni, mwilini tawaishia,
Akuchomae usiku, aadhirike mchana.
Mungu unaye mwamini, hakuachi ukalia,
Endelea kumwamini, hilo atakushindia,
Mtego wa uvunguni, yeye takutegulia,
Akuchomae usiku, aadhirike mchana.
Jiandae kusaini, ushindi ukitimia,
Watu na zao kwanini, wajute wakisikia,
Ukweli ukibaini, na uongo kufulia,
Akuchomae usiku, aadhirike mchana.
Kuna Neno kitabuni, Mungu alishindilia,
Silaha zao vitani, wao zitawarudia,
Tena watachomwa ndani, chozi gumu watalia,
Akuchomae usiku, aadhirike mchana.
Silaha zako makini, dola zinaangushia,
Zidi kunena rohoni, ubaya utafifia,
Mungu aonaye ndani, ndiye takupigania,
Akuchomae usiku, aadhirike mchana.
Kama Esita zamani, ukisema shindilia,
Hao kwako ni wagoni, ni bora wakaishia,
Wapige ndani ya mboni, wajute kukuchulia,
Akuchomae usiku, aadhirike mchana.
Mungu wetu wa amani, ndiye tunamwangukia,
Tunapokuwa shidani, yeye atusaidia,
Wala yeye si haini, mabaya kufagilia,
Akuchomae usiku, aadhirike mchana.
Mtu si wa kumwamini, hilo ninakumbushia,
Akuchekea usoni, moyoni akukandia,
Hata ndani ya sahani, sumu aweza kutia,
Akuchomae usiku, aadhirike mchana.
Ninyi farijianeni, kwa neno lotuachia,
Hatuachi asilani, Mungu tunayemwishia,
Watu wenye kisirani, Yeye atatupingia,
Akuchomae usiku, aadhirike mchana.
Nakuomba Maanani, kweli hii simamia,
Maneno ya mdomoni, yasijekuwazidia,
Na kuwatia shidani, wanaokutumikia,
Akuchomae usiku, aadhirike mchana.
Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment