SHAIRI: MPE NAFASI MJINGA

NAFASI mpe mjinga, mwerevu anaondoka,
Nyumba siyo ya kupanga, asije kuadhirika,
Mbele huyo anasonga, huko kitaeleweka,
Kesho wewe utalia, maji yakishamwagika.
Huyo ajigongagonga, akikuona acheka,
Tena mwerevu kulonga, akili zako kuteka,
Ona ameshakufunga, kwake umeshaanguka,
Kesho wewe utalia, maji yakishamwagika.
Mawazo yanakugonga, mtu unayemtaka,
Mengine yanakupinga, kwingine yanakuteka,
Badala mema kuunga, wewe waingia chaka,
Kesho wewe utalia, maji yakishamwagika.
Pale unapojipanga, nani wa kuchagulika,
Ni kuomba na kufunga, kumlilia Rabuka,
Hiyo haina kuvunga, pema uweze padaka,
Kesho wewe utalia, maji yakishamwagika.
Ni vema muda kutenga, vyeo vipate chambuka,
Mchele safi na chenga, viweze kugawanyika,
Jiwe lisijekugonga, na meno yakameguka,
Kesho wewe utalia, maji yakishamwagika.
Hivi ndivyo nakupanga, uchaguzi ukifika,
Safu yako vema panga, ile inaeleweka,
Acha wajingawajinga, popote hautafika,
Kesho wewe utalia, maji yakishamwagika.
Werevu siyo wajinga, wa kufanya takataka,
Kama moto ni kijinga, kikipikwa chaivika,
Wanaelewa kujenga, kufanya ukainuka,
Kesho wewe utalia, maji yakishamwagika.
Ukichagua wajinga, pakubwa ukawaweka,
Umeshapigwa panga, kidonda cha kugangika,
Jinsi watagongagonga, vyote vitavurugika,
Kesho wewe utalia, maji yakishamwagika.
Ndio wachonga mzinga, nyuki waweze fugika,
Pazuri unautenga, ili waweze vutika,
Uvunguni waupanga, huko vipi watafika?
Kesho wewe utalia, maji yakishamwagika.
Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment