TANROADS PWANI YASAINI MKATABA NA KAMPUNI YA DOTT UJENZI WA BARABARA MLANDIZI
>> Barabara ya Mlandizi - kituo cha reli ya Mwendo kasi itagharimu Tsh Bilioni 60.2
Na Gustaphu Haule, Pwani
WAKALA ya Barabara (TANROADS) Mkoa wa Pwani imesaini mkataba na kampuni ya Dott Services Ltd kutoka nchini Uganda kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mlandizi kuelekea kituo cha reli ya Mwendokasi ( SGR) Ruvu Station wenye thamani ya Tsh.Bilioni 60.25.
Mkataba huo umesainiwa leo Mei 2,2025 katika ofisi za TANROADS Mkoa wa Pwani ukishuhudiwa na baadhi ya wafanyakazi wa ofisi hiyo huku upande wa kampuni ukishuhudiwa na mtendaji Mkuu wake Enock Aligawesa.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani Baraka Mwambage,amewaambia Waandishi wa habari kuwa mkataba huo utahusisha ujenzi wa barabara hiyo kwa urefu wa Kilomita 23 kwa kiwango cha lami.
TANROADS Mkoa wa Pwani na kampuni ya Dott Services Ltd wakisaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Mlandizi - Kituo cha SGR Ruvu Station wenye thamani zaidi ya TSh.Bilioni 60.25.
Amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo utaanzia Mlandizi kuelekea katika kituo cha reli ya Mwendokasi (SGR) Ruvu Station ambapo ujenzi wake utahusisha vipande viwili.
Amesema kuwa kipande cha kwanza kitakuwa chenye urefu wa Kilomita 15 ndani ya barabara ya Mkoa ya Mlandizi Maneromango na kipande cha pili kitakuwa na Kilomita 8 ambacho kinaanzia katika makutano ya barabara hiyo kuelekea kituo cha Ruvu Station.
Amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo utachukua siku 900 mpaka kukamilika ambapo upana wa barabara hiyo itakuwa mitaa 11 kulingana na maeneo mbalimbali.
Amesema , maeneo ya njia ya magari haitapungua mitaa 6.5 ambapo mitaa 3.25 kila upande wa magari lakini mabega ni mita 4 ikiwa ni mita 2 kila upande huku maeneo ya Miji na yenye kona upana wa barabara huwa unaongezeka ambao hufikia mita 11.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani Baraka Mwambage kushoto akibadilishana hati ya mkataba na mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Dott Services Ltd Golamudivet Prudhuit Raj mara baada ya kutilia saini ya ujenzi wa barabara ya Mlandizi - SGR Ruvu Station Mei 2,2025
" Mradi huo pia utahusisha uwekezaji wa taa kadri ya uhitaji katika eneo la Mlandizi Mjini unapoelekea kituo cha reli Ruvu Station.
" Mbali na uwekaji wa taa hizo lakini pia ujenzi huo utahusisha madaraja ambayo kwa mtindo wa barabara hiyo na usanifu wake hayatapungua madaraja manne.
Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Golamudivet Prudhuit Raj, amesema kuwa ataanza kazi maramoja na anaimani atakamilisha kazi kwa muda uliopangwa.
Meneja TANROADS Mkoa wa Pwani Baraka Mwambage na mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Dott Services Ltd Golamudivet Prudhuit Raj wakionesha mikataba ya ujenzi wa barabara ya Mlandizi -Ruvu station Mei 2, 2025
Post a Comment