WAJUMBE WAPITISHENI WENYE SIFA
WAJUMBE nawahusia, tupeni anayefaa
Sisi twawategemea, sije pesa kuthamini,
Pitisheni mgombea, mwenye uwezo jamani,
Wajumbe wapitisheni wagombea wenye sifa.
Wajumbe wapitisheni, wagombea wenye nia,
Watutoe na tabuni, maisha kufurahia,
Wachujeni kwa makini, msiwachuje kwa ria,
Wajumbe wapitisheni wagombea wenye sifa.
Na rushwa iepukeni, kwa haki wateueni,
Msije kuwa kundini, kuwapitisha wahuni,
Misingi zingatieni, twawataka wa thamani,
Wajumbe wapitisheni, wagombea wenye sifa.
Urafiki epukeni, wananchi tulindeni,
Nawaonya kwa yakini, haki pia itendeni,
Bahasha ziepukeni, pitisheni kwa imani,
Wajumbe wapitisheni wagombea wenye sifa.
Jukumu simamieni, pitisheni wanofaa,
Sisi tumewaamini, mtafanya kwa hatua,
Ingawa hatujuani, wapitisheni kwa nia,
Wajumbe wapitisheni, wagombea wenye sifa.
Kwa haki wachambueni, wachujeni kwa hatua,
Majina angalieni, tupeni anayefaa,
Kwa hakika yatendeni, na epukeni rupia,
Wajumbe wapitisheni wagombea wenye sifa.
Tamati nimefikia, ujumbe nimeutoa,
Kwa shairi kupitia, wajumbe kuwahusia,
Mengi nimeelezea, nikiwa ni mwenye nia,
Wajumbe wapitisheni wagombea wenye sifa
Mtunzi ni SirDody- Kilimanjaro
0762396923
Post a Comment