DC MASWA AWAWAKIA MADIWANI WANUNUZI WA PAMBA
Na Samwel Mwanga, Simiyu
KATIKA jitihada za kuhakikisha haki na uwazi katika ununuzi wa zao la pamba wilaya ya Maswa, Mkuu wa wilaya hiyo, Dkt. Vicent Naano Anney, ameonya vikali madiwani wanaojihusisha na ununuzi wa zao hilo, akisisitiza kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watakaokiuka taratibu zilizowekwa.
Akizungumza Mei , 3, 2025 katika kikao cha Baraza la Madiwani, Dkt. Anney amesema kuwa katika ziara aliyoifanya ya kusikiliza kero katika Vijiji na Kata za wilaya hiyo kuna mambo ambayo amejifunza kikiwemo kilimo cha pamba.
Dkt. Anney amehamishiwa hivi karibuni akitokea wilaya ya Bunda mkoa wa mara amesema ya kuwa licha ya kutoka kwenye wilaya inayolima zao hilo lakini kwa wilaya ya Maswa zao hilo ni siasa.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dkt Vicent Naano Anney akizungumza katika kikao cha baraza la Madiwani la halmashauri ya wilaya hiyo.Amesema miongoni mwa mambo aliyojifunza ni pamoja na kampuni zilizo nyingi zinazonunua zao hilo zimekuwa zikiibiwa fedha zao na viongozi wa vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) na kwa musimu huu amemwagiza Afisa ushirika wa wilaya hiyo, kuhakikisha wote waliojihusisha na utapeli wa fedha hizo katika musimu uliopita hawapati nafasi ya kununua pamba msimu huu.
Dkt Anney amesema kuwa wapo madiwani ambao wanajihusisha na ununuzi wa zao hilo jambo ambalo ni sahihi kwani hakuna mgogoro wa kimaslahi kwa wao kufanya hivyo lakini ni lazima wawe wasafi kwa kufuata taratibu zilizowekwa.
“Hakuna mgogoro wa kimaslahi kwa diwani kununua pamba maana hiyo si kazi ya halmashauri bali ni ya bodi ya pamba, lakini mheshimiwa diwani wewe unanunua pamba kwenye eneo la Kata yako au Kata jirani miaka mine mfululizo na AMCOS inapata hasara haipati faida,na watoto wako wako humo kwenye AMCOS ambao ni Katibu na Mhasibu.
“Nimesisitiza muwe wasafi,mimi sitavumilia diwani atakayefanya hujuma kwenye AMCOS na kwenye ununuzi wa pamba nitakuning’iniza, hatutakusamehe.
"Unapokuwa kiongozi wewe ni taswira ya jamii, kila mtu anayekuona ni lazima uwe msafi, lipa kwa wakati fedha za AMCOS,ushuru wa halmashauri na kusiwe na mgogoro,”amesema.
Amesema kuwa kwa taarifa alizonazo ni kuwa baadhi ya madiwani hao ambao ni wanunuzi wa zao hilo wamekuwa wakidaiwa fedha ambazo hawajalipa katika musimu uliopita hivyo akaona ni vyema kuwaeleza ukweli kuwa kwa musimu huu watachukua hatua kali kwa wote wanaokwenda kinyume na taratibu zilizowekwa.
Pia alisisitiza kuwa mizani ya kisasa ya kidigitali inayotumika sasa kununulia zao hilo kwa mkulima ina mfumo unaowezesha ufuatiliaji wa mwenendo wa ununuzi kwa wakati halisi, hivyo ni rahisi kufanya udanganyifu.
Afisa Kilimo wa wilaya ya Maswa, Robert Urassa amesema kuwa ofisi yake imejipanga kuhakikisha msimu huu wa ununuzi wa pamba unakwenda kwa uwazi na haki, kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba Tanzania kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa mizani.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, alieleza kuwa halmashauri hiyo inategemea ushuru wa zao hilo kama chanzo kikuu cha mapato katika halmashauri hiyo kwa ajili ya kuendesha shughuli mbalimbali za miradi ya maendeleo hivyo watahakikisha wanasimamia vizuri ununuzi wa zao hilo katika AMCOS zote.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa.Maisha Mtipa akizungumza katika kikao cha baraza la Madiwani la halmashauri ya wilaya hiyo.Katika kuhakikisha madiwani wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu kilimo bora cha pamba, Halmashauri ya wilaya ya Maswa iliandaa mafunzo maalum kwa waheshimiwa madiwani, ambapo walipatiwa elimu kuhusu masuala ya kisheria na kanuni za kilimo bora cha pamba.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Maswa, Paul Maige akiwa anaongoza kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo.
Post a Comment