HEADER AD

HEADER AD

SERIKALI, BARRICK NORTH MARA KUENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO ZA AJIRA KWA VIJANA


>>Mafunzo kwa vijana waliopewa leseni ya uchimbaji yazinduliwa 

Na Dinna Maningo, Tarime

SERIKALI ya mkoa wa Mara, imesema kwamba utoaji wa leseni bure kwa vikundi vya vijana wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika vijiji vinavyozunguka mgodi wa Barrick North Mara, ni kuendelea kuwajali vijana.

Serikali imesema kwamba ina ina imani kubwa kupitia utoaji wa leseni kwa vikundi vya vijana wanaozunguka mgodi itamaliza changamoto ya uwepo wa matukio ya uvamizi yaliyokuwa yanafanywa na vijana kutokana na kukosa maeneo ya uchimbaji.

        Vijana kutoka vijiji vinavyozunguka mgodi waliopewa leseni za uchimbaji wa madini ya dhahabu.

Pia Mgodi wa Barrick North Mara, umeahidi kuendelea kuunga mkono vijana katika hatua mbalimbali ili kuhakikisha sekta ya madini inazidi kuwainua vijana hususani vijana wanaouzunguka mgodi huo.

Hayo yameelezwa wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya siku 14 yanayotolewa na serikali kwa vikundi 48 vya vijana waliopewa leseni za uchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu,  mafunzo yaliyodhaminiwa na mgodi wa Barrick North Mara kwa kushirikiana na mfuko wa dhamana  (TRUST FUND).

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, mkuu wa wilaya ya Musoma Juma Chikoka , Juni, 20, 2025 katika viwanja wa Ingwe sekondari - Nyamongo, wilayani Tarime, amesema kwamba utoaji wa leseni kwa vijana ni moja ya hatua ya kuendelea kutatua changamoto za vijana katika ajira.

           Mkuu wa wilaya ya Musoma, Juma Chikoka akifungua mafunzo kwa vikundi vya vijana vya uchimbaji wadogo wa madini ya dhahabu.

" Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwajali wachimbaji wote wadogo hasa vijana na kutoa leseni za uchimbaji kwa vijana katika maeneo yao yanayozunguka mgodi .

" Mwezi Mei, 25, 2025 Waziri wa Madini Mavunde alikuja Nyamongo na kukabidhi leseni za uchimbaji wa madini kwa vikundi 48, kwa lengo la kuwawezesha vijana kunufaika na rasilimali hii muhimu." Amesema DC Juma .

Ameongeza kusema " Serikali ina imani kubwa itamaliza changamoto ya uwepo wa matukio ya uvamizi wa mgodi yaliyokuwa yanafanywa na vijana kutokana na kukosa maeneo ya kuchimba dhahabu.

       Mkuu wa wilaya ya Musoma, Juma Chichoka aliyemwakilisha mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akizindua mafunzo katika mradi wa vikundi vya vijana wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu.

" Serikali ina amini kwamba leseni hizo za uchimbaji zinaenda kuwa suluhisho ya changamoto kwa vijana wetu wale Intruda" amesema Juma.

Serikali ya Mara imeushukuru na kuupongeza mgodi huo wa Barrick North Mara kwa kulidhia na kutoa leseni zao katika mradi huo ili ziweze kunufaisha vijana wa maeneo yanayozunguka mgodi.

" Kwa kutambua umuhimu wa uwekezaji  mkubwa uliofanywa na kutoa leseni bure kwa vikundi vya uchimbaji, Serikali imeona kuna haja na hoja ya kutoa mafunzo ya siku 14 yaliyoanza kutolewa Juni, 21, 2025 na kuhitimishwa Julai, 04, 2025.

" Lengo ni kuwajengea uwezo vijana kuhusu uendeshaji wa vikundi , sheria , taratibu zilizopo katika sekta ya madini " amesema DC Juma Chikoka.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Meneja mkuu wa mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko, Meneja Mahusiano wa mgodi huo, Francis Uhadi, amesema mafunzo hayo kwa vijana ni sehemu za jitihada za mgodi wa Barrick na mfuko wa dhamana wa North Mara (TRUST FUND).

Meneja Mahusiano wa mgodi huo, Francis Uhadi, akiteta jambo na mkuu wa wilaya ya Musoma, Juma Chichoka aliyemwakilisha mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi kwenye uzinduzi wa mafunzo katika mradi wa vikundi vya vijana wachimbaji wa madini ya dhahabu.

" Lengo la mafunzo ni kuhakikisha sekta ya madini inakuwa na tija zaidi ikizingatia usalama endelevu wa mazingira, usimamizi wa biashara, kuheshimu na kufuata taratibu na sheria za nchi na usimamizi wa vikundi pamoja na elimu kuhusu masuala ya fedha na kuepuka migogoro katika uchimbaji hasa kwenye vikundi vya wachimbaji wadogo" amesema Francis.

Amesisitiza kwamba mafanikio ya mradi huo yanahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya wachimbaji , serikali na wadau wengine na kwamba mgodi utaendelea kuunga mkono katika hatua mbalimbali ili kuwainua vijana katika sekta ya madini hususani vijana wanaozunguka mgodi huo.

Amewahimiza wachimbaji kuwa waaminifu, waadilifu, waendelee kujifunza ili kuboresha shughuli zao za uchimbaji na kufanya kazi kwa ushirikiano na mshikamano kuhakikisha mafanikio ya vijana yanadumu na kuleta maendeleo kwa jamii.

Amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu , Waziri Mavunde na mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi ambaye ni mlezi wa vikundi hivyo vya vijana vya wachimbaji wa madini katika kuboresha vijana kupitia madini.

Afisa Madini mkazi mkoa wa Mara, Amini Msuya , amesema mafunzo kwa vikundi vya vijana wachimbaji yatahusisha mada mbalimbali zitakazowajengea uwezo katika uchimbaji wa madini , matumizi ya fedha , sheria ya madini, kuhifadhi wa mazingira na biashara ya madini.

    Mkuu wa wilaya ya Musoma , Juma Chikoka akisalimiana na kiongozi wa Ngoma ya asili, Kushoto ni Afisa madini  mkazi mkoa wa Mara, Amini Msuya.

" Utekelezaji wa mradi huo umepitia katika hatua zifuatazo, kusajili vijana wanaohitaji kuingia kwenye mradi, vijana waliosajiliwa waliunda vikundi, serikali kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali iliandaa maeneo ili kuwapatia leseni vikundi vya vijana vilivyoundwa.

" Vikundi vilipatiwa maeneo na kuvikabidhi leseni na sasa ni hatua ya kuwajengea vijana uwezo waliopo kwenye vikundi kabla hawajaanza shughuli ya uchimbaji. 

"Na baada ya kumaliza mafunzo itaendelea hatua ya kuwaonesha leseni zao na kuwawekea utaratibu wa uchimbaji,  na hatua ya mwisho itakuwa mpango wa utafiti wa maeneo yao kwa kushirikiana nao katika shughuli zao za uchimbaji." amesema Amini .

Amesema kwamba vikundi 48 vyenye vijana 1736 vimepewa leseni za uchimbaji wa madini ya dhahabu ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde kwa vijana hao wanaotoka maeneo yanayozunguka mgodi.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa kamati ya maendeleo (CDC) Diwani wa Kata ya Matongo Godfray Kegoye , Diwani wa Kata ya Nyarokoba, Juma Matiko ameiomba serikali kuongeza juhudi ili vijana waanze uchimbaji.

Ameushukuru mgodi wa Barrick North Mara kwa kujitoa kuhakikisha maeneo yanayozunguka mgodi vijana wananufaika na mradi huo.

" Mgodi umesikia kilio cha wananchi tunaomba tushirikiane kwa pamoja tuhakikishe vijana wetu tunapoanza mwaka 2026 tuone sura hizi zimebadikika kwa kiwango kikubwa ." amesema Diwani.

Diwani wa Kata ya Kemambo, Rashid Bogomba , amewaomba vijana kuzitendea haki leseni huku akimuomba mlezi wa vikundi hivyo ambaye ni mkuu wa mkoa wa Mara, kuwa bega kwa bega na vijana hao ili uchimbaji huo ulete manufaa kwa vijana.

Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo kwa vikundi vya vijana waliopewa leseni za uchimbaji wa madini ya dhahabu, Carren John ameishuku serikali na mgodi kwa kuwapatia leseni na kwamba mafunzo hayo yatawasaidia kuwajenga wanapokuwa katika shughuli za uchimbaji.

Mei, 03, 2025, Waziri wa Madini Anthony Mavunde akiwa Nyamongo, alikabidhi leseni kwa vikundi 48 vya vijana wanaozunguka mgodi wa Barrick North Mara ili kujiinua kiuchumi kama ilivyoripotiwa katika chombo hiki cha habari, Mei, 04, 2025.






















No comments