HEADER AD

HEADER AD

TUKIWAPENDA WATOTO ...

MIMI napenda watoto, wewe ndugu yangu vipi?

Ninapenda wapate joto, siwaze walale wapi,

Yabaki kwangu mapito, wao wabakie hapi,

Tukiwapenda watoto, tunajipenda wenyewe.

Siku hii ya mtoto, hapa kwetu Afrika,

Kumbukumbu yake nzito, ya kusini mwa Afrika,

Waliuliwa watoto, mateso yakasikika,

Tukiwapenda watoto, tunajipenda wenyewe.

Bila watoto ni ndoto, kuendeleza kizazi,

Tutakwenda kama mto, kukauka kiangazi,

Sawa kushika mfuto, kukimaliza kizazi,

Tukiwapenda watoto, tunajipenda wenyewe.

Waende shule watoto, hata sisi tujinyime,

Tusikilizie wito, kutaka wao wasome,

Tusiwakawize watoto, kwa pendo tuwatazame,

Tukiwapenda watoto, tunajipenda wenyewe.

Wakigonjeka watoto, peleka zahanatini,

Kama linazidi joto, nenda hosipitalini,

Wapate tiba watoto, washamiri duniani,

Tukiwapenda watoto, tunajipenda wenyewe.

Mahitaji ya watoto, ni mengi tunayaweza,

Wape furaha watoto, bila ya kuwapoteza,

Mzazi kuwa mvuto, wao ukiwapendeza,

Tukiwapenda watoto, tunajipenda wenyewe.

Kuharibika watoto, wazazi tunachangia,

Utukututu wa watoto, walezi tunachangia,

Bila malezi watoto, shimo tunawachimbia,

Tukiwapenda watoto,tunajipenda wenyewe.

Unyanyasaji watoto, tuache si jambo zuri,

Kutelekeza watoto, sawa sawa na sifuri,

Sote tufanye watoto, wasipate yote zari,

Tukiwapenda watoto, tunajipenda wenyewe.

Kuwaharibu watoto, kwa sababu sio wako,

Ujipatie kipato, na faida iwe yako,

Ninasema kwa mkato, iache tabia yako,

Tukiwapenda watoto, tunajipenda wenyewe.

Sote tulee watoto, kama twazaa wenyewe,

Wasiwekwe kwenye moto, twajimaliza wenyewe,

Tuwajenge kwa kipato, watatufaa wenyewe,

Tukiwapenda watoto, tunajipenda wenyewe.

Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments