HEADER AD

HEADER AD

VIONGOZI WA DINI SIMIYU WAPEWA ELIMU YA URAIA


Na Samwel Mwanga, Bariadi

VIONGOZI wa dini mkoani Simiyu wametakiwa kuwahamasisha waumini wao kujitokeza kwa wingi kushiriki Uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, ikiwa ni sehemu ya kutimiza haki yao ya kikatiba ya kumchagua kiongozi bora.

Wito huo ulitolewa Juni 25, 2025, na Mwezeshaji wa Elimu ya Uraia, Uzima Justin, wakati wa mafunzo ya siku mbili kwa viongozi wa dini wa mkoa huo yaliyofanyika mjini Bariadi.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Uzima amesema uchaguzi ni mchakato unaohusisha kila raia na kwamba umekuwapo tangu enzi za kale, hata katika maandiko ya vitabu vitakatifu.
“Katika mfumo wa demokrasia, ushindani wa sera na mitazamo ni jambo la kawaida. 

     Mwezeshaji wa Elimu ya Uraia, Uzima Justin akitoa moja ya mada katika mafunzo kwa viongozi wa dini mkoa wa Simiyu.

Hakuna uchaguzi usiokuwa na mapungufu, hivyo ni jukumu la wadau wote, wakiwemo viongozi wa dini, kushirikiana kuyaondoa na kuhakikisha kila mmoja anashiriki bila woga,” amesema.

Amesisitiza kuwa viongozi wa dini wako katika nafasi nzuri ya kutoa elimu ya uraia, hususan kuhamasisha amani, utulivu, na ushiriki wa wananchi.

“Ninyi kama viongozi wa dini, mna nafasi kubwa ya kuwaelewesha waumini wenu washiriki uchaguzi mkuu ujao, wachague viongozi watakaowaongoza kwa miaka mitano ijayo. Ni lazima muwe raia makini msiyumbishwe,” amesema.

Mwanasheria Maftaha Ngwebeya amesema viongozi wa dini wana jukumu la kutumia majukwaa yao kufundisha misingi ya katiba, sheria za uchaguzi, na haki ya kila raia kupiga kura.


“Viongozi wa dini ni watu wanaoheshimika sana. Endapo mtatumia nafasi zenu vizuri, mnaweza kupunguza migogoro, taharuki, na upotoshaji unaoweza kujitokeza wakati wa uchaguzi,” amesema.

Shekhe Issa Eliasa, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, amesema viongozi wa dini wana wajibu wa kuwaeleza waumini wao ukweli na hali halisi ya kisiasa nchini, huku akisisitiza kutenda haki.

     Shekhe Issa Eliasa akiwa kwenye mafunzo ya elimu ya uraia mjini Bariadi mkoa wa Simiyu.

“Viongozi wa dini tuna wajibu wa kuwaeleza waumini wetu ukweli kuhusu mwelekeo wa kisiasa hapa nchini, lakini pia tuhakikishe tunatenda haki katika zoezi hili. Ni muhimu tusiiegemee upande wowote ili kila mmoja awe huru kushiriki uchaguzi kwa amani na bila hofu,” amesema.

Mchungaji Winstone Kweka wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) aliyehudhuria mafunzo hayo, amesema elimu hiyo ni muhimu na kwamba viongozi wa dini watakuwa mabalozi wazuri wa mchakato wa uchaguzi.

“Tutahakikisha tunawaelimisha waumini wetu kuhusu umuhimu wa kupiga kura, kuepuka vurugu, na kuheshimu matokeo,tunaamini kwamba kupitia mafunzo haya tutaweza kuchangia uchaguzi wa amani na maendeleo,”amesema.

Mkazi wa Bariadi, Khalima Mohamed amesema ni faraja kuona viongozi wa dini wakihamasishwa kutoa elimu ya uraia.

“Viongozi wa dini wakiwa mstari wa mbele kuhamasisha ushiriki wa wananchi, tutapata uchaguzi ulio huru, wa haki na wenye amani,” amesema.

Mratibu wa Mradi wa Norwegian Church Aid(NCA),Omari Ibrahim amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha viongozi wa dini wanakuwa sehemu ya mchakato wa demokrasia.

“Tunatambua nafasi kubwa ya viongozi wa dini katika jamii yetu. Tumeamua kuwajengea uwezo ili wasaidie kupunguza sintofahamu kuhusu mchakato wa uchaguzi, hususan kipindi hiki tunapoelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025,”amesema.




No comments