UPUNGUFU WA DAMU KWA WAJAWAZITO MASWA BADO NI TATIZO
Na Samwel Mwanga, Maswa
TATIZO la upungufu wa damu miongoni mwa akinamama wajawazito katika wilaya ya Maswa limetajwa kuwa kubwa, hali inayochangiwa na kutokuzingatia lishe bora inayojumuisha makundi sita ya vyakula muhimu kwa afya ya mama na mtoto.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya katika wilaya hiyo, hali hiyo imeendelea kuwa tishio kwa maisha ya mama na mtoto hasa wakati wa kujifungua, huku baadhi ya wajawazito wakionekana kutoelewa umuhimu wa mlo kamili au kushindwa kumudu gharama za vyakula mchanganyiko kutokana na changamoto za kiuchumi.
Akizungumza Alhamis, Juni 12, 2025 na wananchi wa kijiji cha Mwabagalu wilayani humo,Afisa Lishe wa wilaya ya Maswa, Kelvin Mwiza amesema kuwa asilimia kubwa ya wajawazito wanaofika kliniki hugundulika kuwa na kiwango cha damu kilichoshuka chini ya kiwango kinachohitajika kiafya.
Amesema kuwa upungufu wa damu kwa wakinamama wenye umri wa miaka 15 hadi 45 ni asilimia 37.4, hali ambayo inasababishwa na kutokula chakula chenye makundi sita ya chakula ambayo ni protini, vitamin, wanga, madini mafuta na maji.
“Tunaona mama anafika kliniki akiwa na kiwango cha damu chini ya 11g/d na hali hii huweka maisha yake na ya mtoto aliye tumboni kwenye hatari kubwa. sababu kubwa ni lishe duni na kutozingatia ushauri wa kitabibu,” amesema.
Amesema kuwa kwa sasa vituo vya afya wilayani humo vinaendelea kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wajawazito na kugawa tembe za madini ya chuma ili kusaidia kuongeza damu, lakini ufanisi wake unategemea mwitikio wa jamii kufuata mashauri ya kitaalamu.
Rosaria Laurent mkazi wa kijiji cha Mwabagalu ambaye ni mama wa watoto wawili amesema kuwa alijifungua mtoto wa kwanza akiwa na kiwango cha damu kilichoshuka hadi 7g/dL, hali iliyomlazimu kuongezewa damu haraka.
"Nilikuwa nachoka sana,
kichwa kinauma, na sikuwa najua kama ni upungufu wa damu. Nilipofika kliniki walisema lazima niongezwe damu haraka, la sivyo ningepoteza maisha. Tangu hapo nimejifunza umuhimu wa lishe,” amesema.
Ester Charles mkazi wa kijiji cha Igwata wilayani humo ambaye kwa sasa ni mjamzito wa miezi sita, amesema changamoto kubwa kwake ni uwezo mdogo wa kununua vyakula vya kutosha.
"Hapa kijijini tunakula ugali na maziwa au mboga tu. Samaki au matunda ni nadra sana. Nimeambiwa nile makundi sita ya chakula lakini vingine havipatikani wala sina uwezo wa kuvipata,” amesema.
Kwa mujibu wa mhudumu wa Afya katika kijiji cha Mwabagalu, Milembe Hoja amesema kuwa zaidi ya wajawazito watano kati ya 10 wanaohudhuria kliniki kwenye zahanati ya kijiji hicho hukutwa na dalili za upungufu wa damu.
“Tunawapa vidonge vya madini ya chuma na folic acid, lakini wengi hawamalizi dozi au hawafuati masharti. Wengine wanatumia dawa za kienyeji badala ya kufuata ushauri wa wataalamu,” amesema.
Amesema moja ya changamoto zinazokwamisha mapambano hayo ni pamoja na imani potofu kuhusu lishe na dawa za kliniki,ugumu wa maisha vijijini na ukosefu wa vyakula mchanganyiko na uelewa mdogo kuhusu athari za upungufu wa damu.
Haliye Abubakary ni Afisa kutoka wizara ya Afya,Idara ya kinga,sehemu ya huduma za lishe amesema kuwa serikali imeweka mikakati ya kuhakikiksha inapambana na changamoto hiyo kwa kuhamasisha na kutoa elimu nchi nzima kwa akinamama wajawazito kula vyakula vyenye makundi sita ya vyakula.
Haliye Abubakary ni Afisa kutoka wizara ya Afya,Idara ya kinga,sehemu ya huduma za lishe akielezea jinsi serikali ilivyojipanga kupambana na upungufu wa damu kwa wajawazito hapa nchini.
“Na ndiyo maana leo tupo mkoa wa Simiyu kuhakikisha tunatoa elimu na kuhamasisha wajawazito kula vyakula vyenye makundi sita ya vyakula nah ii ni kampeni nchi nzima kuhakikisha tunaondoa tatizo la lishe na upungufu wa damu kwa wakina mama hao,”amesema.
Katibu tawala wa wilaya ya Maswa, Athuman Kalaghe ameeleza kuwa wilaya hiyo imeweka mikakati maalum ili kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa lishe kwa wajawazito, ikiwa ni pamoja na kampeni za lishe bora kupitia vituo vya afya, shule na mikutano ya kijiji.
Katibu tawala wilaya ya Maswa, Athuman Kalaghe (aliyesimama) akizungumzia mikakati ya wilaya hiyo kupambana na tatizo la upungufu wa damu kwa wajawazito.
“Tunaongeza nguvu kwenye elimu ya afya ya uzazi na lishe, lakini pia tumeagiza viongozi wa vijiji na kata kuhakikisha wajawazito wote wanahudhuria kliniki na kufuata masharti ya lishe wanayopewa sambamba na kila shule ya msingi na sekondari kutoa chakula chenye virutubisho kwa wanafunzi .
“Pia kampeni za kutoa elimu ya lishe zitaimarishwa katika ngazi ya vijiji, na wahudumu wa afya ya jamii wataongeza ufuatiliaji kwa wajawazito hadi majumbani,”amesema.
Amesema kuwa mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali ikiwemo kampuni ya SANKU imekuwa ikishirikiana na serikali katika wilaya hiyo kwa kufunga mashine katika vijiji mbalimbali kwa ajili ya kuongeza virutubishi katika unga wa mahindi unatumiwa mara kwa mara na jamii katika chakula.
Pia amesema kuwa katika baadhi ya maeneo ya vijiji katika wilaya hiyo kumeanzishwa mashamba darasa ya mahindi lishe, viazi lishe na maharagwe lishe na kutoa virutubisho vya damu bure kwa wanawake wajawazito hasa katika maeneo ya vijijini ambako hali ni mbaya zaidi.
Wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa lishe yenye makundi yote sita ya vyakula vya wanga, protini, vitamini, madini, mafuta na maji si ya gharama kubwa ikiwa jamii itatumia vyakula vinavyopatikana katika mazingira yao kama mboga za majani, kunde, nafaka, matunda na samaki.
Eliamani Mmari(kulia)kutoka kampuni ya SANKU akieleza jinsi mashine ya kuchanganya virutubishi na unga wa mahindi katika mashine ya kusaga mahindi kuwa unga kwa ajili ya chakula.
Post a Comment