WANAOKOPESHA BILA KUSAJILIWA BoT KUSAKWA
>> DC Maswa aagiza msako ufanyike
Na Samwel Mwanga, Maswa
SERIKALI ya Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu, imetangaza oparesheni maalum ya kuwakamata wafanyabiashara wote wanaotoa mikopo kwa wananchi bila kusajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) huku wakituhumiwa kuwaumiza wananchi kwa riba kubwa na mikataba ya ujanja.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Vicent Naano, ametoa tamko hilo Ijumaa, Mei 13, 2025, mjini Maswa wakati akikabidhi mikopo ya Tsh. Milioni 133.6 kwa vikundi vya uzalishaji mali vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dkt Vicent Naano akizungumza wakati wa utoaji wa mikopo kwa makundi maalum katika halmashauri ya wilaya ya Maswa.“Wafanyabiashara hawa siyo tu wanatoza riba kubwa, bali wanatengeneza mikataba ya kijanja kwa nia ya kuwadhulumu wananchi iwapo kesi itafika mahakamani.
" Oparesheni ya kuwakamata inaanza mara moja. Tunawafahamu na tutawapeleka kwenye vyombo vya sheria,” amesema Dkt. Naano kwa msisitizo.
Ameeleza kuwa mikopo inayotolewa na Halmashauri kupitia mapato ya ndani haina riba na ni heshima ya serikali kwa wananchi wake, akisisitiza umuhimu wa kurejesha fedha kwa wakati ili kuwanufaisha wengine.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dkt Vicent Naano(kuahoto)akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya TSh Milioni 133.6 kwa vikundi vya makundi maalum katika halmashauri ya wilaya ya Maswa.Miongoni mwa walionufaika ni Lushinge Salinja, mlemavu kutoka kijiji cha Sola, aliyepokea mkopo wa Bajaji na kusema: “Ninaishukuru Serikali kwa kutukumbuka watu wa makundi maalum. Nitaitumia Bajaji kujipatia kipato.”amesema.

Elizabeth Paul kutoka kijiji cha Mwamitumai, amesema: “Mkopo huu utanisaidia kuongeza mtaji. Nitaachana kabisa na mikopo ya mitaani maarufu kama ‘Kausha damu’.”amesema.
Vijana nao hawakubaki nyuma. Marco Paul wa kijiji cha Sengwa amesema mkopo huo utawasaidia kuanzisha shughuli mbalimbali za uzalishaji mali
Lushinge Salinja mwenye ulemavu wa viungo kutoka kijiji cha Sola, aliyenunua Bajaji kwa mkopo wa halmashauri ya wilaya ya Maswa.Mwenyekiti wa Halmashauri ya Maswa, Paul Maige, amewataka wanufaika kutumia fedha hizo kama kichocheo cha maendeleo kwao na kwa wilaya kwa ujumla.
Akitoa taarifa ya ugawaji mikopo hiyo, Afisa Maendeleo ya Jamii, Lucia Misinzo, amesema kuwa ni awamu ya pili kwa makundi maalum. Vikundi tisa vya wanawake vilipata Sh milioni 78, vijana vikundi vinne TSh Milioni 36 na vikundi vitatu vya watu wenye ulemavu TSh Milioni 19.
Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya wilaya ya Maswa, Lucia Misinzo akisoma taarifa ya vikundi vitakavyopatiwa mikopo katika wilaya hiyo.Hata hivyo, amesema changamoto zimebaki ikiwemo uchache wa fedha kulinganisha na mahitaji pamoja na uelewa mdogo wa baadhi ya wanakikundi kuhusu matumizi ya mfumo wa mikopo ya asilimia 10.
Post a Comment