WAFUGAJI WATAKA HATI ZA UMILIKI WA MAENEO YA MALISHO
Na Samwel Mwanga, Bariadi
CHAMA cha Wafugaji Tanzania (CCWT) kimeiomba Serikali kuchukua hatua madhubuti za kupanga, kupima na kumilikisha maeneo rasmi ya malisho.
Lengo ni kutokomeza migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa chanzo cha majeruhi, vifo na uharibifu wa mali katika maeneo mbalimbali nchini.
Wito huo umetolewa Juni 15, 2025 na Katibu wa CCWT, Mathayo Daniel, katika kongamano la kitaifa la wafugaji lililofanyika kwenye viwanja vya Nanenane, Nyakabindi wilayani Bariadi, mkoani Simiyu.
Katibu wa CCWT, Mathayo Daniel akitoa taarifa kwenye kongamano la wafugaji kwenye viwanja vya Nyakabindi mkoa wa Simiyu.
Amesema kuwa licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali katika kuboresha sekta ya mifugo, tatizo la uhaba wa maeneo ya malisho na maji limeendelea kuwasukuma wafugaji kuhama kutoka eneo moja hadi jingine, hali inayochochea migogoro na kuathiri ustawi wa sekta hiyo muhimu ya kiuchumi.
"Pamoja na mambo mazuri ambayo serikali yetu imetufanyia, ombi letu la sasa ni maeneo ya malisho yapimwe na yamilikishwe kwa wafugaji,pia tupatiwe maji ya mifugo, bila hivyo, migogoro kati ya wakulima na wafugaji itaendelea," amesema .
Ameongeza kuwa baadhi ya juhudi kama ujenzi wa majosho 750 ya kuogeshea mifugo na uchimbaji wa visima vya maji katika baadhi ya maeneo ni hatua njema, lakini bado hazijakidhi mahitaji ya wafugaji katika maeneo mengi ya nchini.
Mfugaji Maligigwa Maganga kutoka Meatu, mkoa wa Simiyu amesema kuwa umiliki rasmi wa maeneo ya malisho utaongeza tija kwa wafugaji na kuinua uchumi wa mifugo nchini.
"Tukipata maeneo yetu ambayo tutayamiliki, mifugo yetu itapata malisho bora na hivyo tutazalisha maziwa na nyama zenye ubora na ushindani kwenye soko la ndani na hata kimataifa," amesema.
Naye Naila ole Nashaki mfugaji kutoka wilaya ya Ngorongoro mkoa wa Arusha amesema kuwa ni vizuri kwa wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya ardhi kupanga na kutenga maalum ya malisho kama ilivyoelekezwa kwenye Mpango kabambe wa matumizi ya ardhi wa taifa (NLUP).
“Wafugaji tukiwa na maeneo yetu ambayo yamerasimishwa lakini pia tukipata hati miliki itakuwa ni hatua ya kututambua rasmi kisheria na kutuwezesha kupata mikopo kupitia sekta ya kifedha,”amesema.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ashati Kijaji amesema kuwa hatua hii ni muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo yameathiri upatikanaji wa malisho na maji, hivyo kusababisha wafugaji kuhama mara kwa mara.
Waziri wa mifugo na uvuvi,Ashatu Kijaji akizungumza katika kongamano la Wafugaji Kitaifa lililofanyika viwanja vya Nyakabindi mkoa wa Simiyu
Amesema kuwa mara nyingi, migogoro hiyo huzuka wakati wafugaji wanapolazimika kuvamia mashamba ya wakulima wakitafuta malisho au maji kwa ajili ya mifugo yao hali inayosababisha uharibifu wa mazao na kusababisha uhasama mkubwa kati ya jamii hizi mbili.
Mgeni rasmi katika kongamano hilo,Katibu Mkuu wa CCM,Balozi Dkt Emanuel Nchimbi amesema kuwa chama hicho kwa kuona umuhimu wa wafugaji katika ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2025-2030 imeelekeza serikali kutenga na kumilikiwa kwa maeneo ya malisho.
Katibu Mkuu CCM,Dkt Emanuel Nchimbi akizungumza katika kongamano la wafugaji katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.
“Mikakati ya kudhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji,ilani inasisitiza juhudi za serikali za kupunguza migogoro ya ardhi na malisho, ikiwa ni pamoja na utayarishaji wa mipaka ya maeneo ya malisho, uwekezaji katika msingi wa maji, na ununuzi wa mifugo kadiri inavyofaa ,”amesema.
Katika miaka ya hivi karibuni, migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji imezidi kushika kasi hususan katika mikoa ya Simiyu, Tabora, Morogoro na Manyara.
.
Post a Comment