ELIAKIM MASWI AWAPATIA WAANDISHI WA HABARI LAPTOP ZENYE THAMANI YA MILIONI 11.4
>> Tarakilishi hizo mpakato zimenunuliwa kwa fedha zake za mfukoni
>>Waandishi wa habari wamshukuru Maswi kwa kujali
>> Wasema ni za kisasa zitarahisisha utendaji wa kazi
Na Mwandishi wetu , Musoma
KATIBU mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria nchini Tanzania , Eliakim Maswi amewapa Tarakilishi mpakato kwa jina maarufu kompyuta mpakato (Laptop) baadhi ya waandishi wa habari kutoka wilaya ya Tarime na Musoma wapatao 14 , zenye jumla ya thamani ya Tsh. 11,480,000 ziwasaidie katika majukumu yao ya kazi .
Eliakim Maswi ambaye ni mzaliwa wilayani Tarime mkoani Mara, amesema ametoa Tarakilishi hizo aina ya HP ikiwa ni utekelezaji wa ombi la Waandishi wa habari 14 mkoani Mara waliomuomba awanunulie ili ziwawezeshe kutekeleza vyema majukumu yao ya kazi.
" Waandishi hao wa habari walifika nyumbani kwangu kijijini wakati nikiwa kwenye maandalizi ya harusi ya kijana wangu mwishoni mwa mwezi uliopita. Walikuja ili tufahamiane ,tuzungumze tubadilishane mawazo lakini pia walitaka kufahamu kama nami nitatia nia ya ubunge Jimbo la Tarime vijijini .
" Tulizungumza nikawaambia mimi sijatangaza nia ya kugombea ubunge na kama nikitaka nitasema . Tukiwa katika mazungumzo waliniomba niwanunulie kompyuta ili ziwasaidie katika majukumu yao kwasababu wapo baadhi yao hawana vitendea kazi wanapata changamoto wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao " amesema Eliakim.
Amewaomba kuzitumia vyema ili ziweze kuwasaidia katika kazi zao za uandishi wa habari huku akiwasisitiza kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia maadili hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa ndani ya vyama na uchaguzi mkuu.
Akikabidhi Tarakilishi hizo kwa Waandishi wa habari kwa niaba ya Katibu mkuu Eliakim Maswi , makabidhiano yaliyofanyika mjini Musoma , Mwandishi wa Azam TV mkoa wa Mara, Augustine Mgendi na waandishi wenzake wa habari wamemshukuru kiongozi huyo kwa kuwajali waandishi wa habari.

" Tunamshukuru Katibu mkuu Maswi kwa hiki alichotusaidia sisi waandishi wa habari , ni kitu ambacho tutamkumbuka sana kwenye kazi zetu kwasababu vifaa vya utendaji kazi kwa waandishi wa habari ni changamoto sana.
" Baadhi ya waandishi wa habari tulimuomba atusaidie kompyuta mpakato na yeye akachukua hatua za haraka kutusaidia . Kitendo cha mtu kuweza kukusaidia kitendea kazi ni mtu ambaye anajali maisha yako anakupenda na anakuthamini.
Mgendi amemuomba Maswi msaada huo usiishie hapo aendelee kuwiwa kuwasaidia waandishi wa habari ili kuboresha mazingira yao ya utendaji wa kazi kwani baadhi ya waandishi wa habari wanachangamoto ya vifaa vya kazi katika shughuli zao za uandishi wa habari na hawana uwezo wa kifedha kuwawezesha kununua vifaa vya gharama na vya kisasa.
Mwandishi wa habari Augustine Mgendi akimkabidhi kompyuta mpakato (Laptop) Mwandishi wa habari wa Channel Ten , Mussa Makari miongoni mwa waandishi wa habari waliopewa kifaa hicho, vilivyotolewa na Katibu mkuu wizara ya Katiba na Sheria , Eliakim Maswi.
" Hizi Laptop popote unapoenda tutafanya kazi yako kwa wakati na kwa haraka . Maswi kamfanya mwandishi kuwa wa kisasa zaidi kuliko alivyokuwa anafanya kazi. Tunaendelea kumkaribisha katika maisha yetu ya kikazi aweze kutusaidia.
" Waandishi wa habari mkoani Mara tupo wengi, si rahisi kuwamudu wote kwa wakati mmoja ,tunaomba na waandishi wengine ambao hawakupata fursa hii nao siku nyingine wapate laptop na wadau wengine wajitokeze kusaidia " amesema Mgendi.
Mwandishi wa habari wa DIMA Online , Dinna Maningo amesema Maswi ni mfano wa kuigwa kwani hakuna kiongozi wa juu aliyopo serikalini ambaye ni mzaliwa wa Tarime aliyewahi kuwasaidia vitendea kazi waandishi wa habari licha ya kwamba kuna viongozi wakubwa ndani ya serikali ambao ni wazawa mkoani Mara.
Tarakilishi zilizotolewa na Katibu mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi kwa baadhi ya waandishi wa habari mkoani Mara .
Amesema kwa upande wa viongozi wa kisiasa wilayani Tarime aliyewahi kuwasaidia vifaa vya kazi waandishi wa habari ni Nyambari Nyangwine aliyewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Tarime vijijini mwaka 2010- 2015, aliweza kuwapatia kamera baadhi ya waandishi wa habari wilayani humo.
" Tunamshukuru sana kiongozi wetu wa kiserikali Eliakim Maswi kuwakumbuka waandishi wa habari mkoani Mara. Ni jambo jema kama mtu una uwezo ukakumbuka ulikotoka na kufanya jambo hii inaleta faraja sana.
" Waandishi wa habari tumekuwa tukikumbukwa tu kwenye kazi za kihabari tunaalikwa tunafanya kazi lakini linapofika suala la kuwasaidia waandishi basi watu hukaa kando na kuwaona waandishi hawastaili kuwezeshwa bali kazi yao ni kuandika tu habari. Kumbe sivyo nao ni wananchi kama wengine wanastahili kusaidiwa" amesema Dinna.
Ameongeza kusema " Mara nyingi watu wamekuwa na mitazamo hasi kwamba waandishi wa habari wakisaidiwa wanalichukulia jambo hilo kuwa wamehongwa kwa ajili ya malengo fulani.
" lakini wananchi wengine wakisaidiwa wao wako sawa . Sasa unajiuliza kwani Mwandishi wa habari yeye sio binadamu ama sio mwananchi je yeye hana shida binafsi ? kwanini yeye akisaidiwa watu wanakuwa na hisia tofauti! .
" Mbali na kazi kuna maisha mengine ,na ieleweke kuwa mwandishi wa habari kusaidiwa haifuti dhana ya utendaji wake wa kazi kama ni mwadilifu kazini ni mwadilifu tu hivyo watu waache mitazamo hasi kwamba kumsaidia mwandishi wa habari ni kosa.
" Waandishi wa habari nao ni binadamu wana changamoto kama zilivyo changamoto za watu wengine hasa ikizingatiwa baadhi ya waandishi wa habari vipato vyao ni duni na wana familia , kwahiyo tunamshukuru Maswi si mtiania ni mtumishi wa serikali ameamua kuwezesha waandishi wa habari . " Amesema Dinna.
Mwandishi wa habari wa kujitegemea gazeti la Nipashe, Timothy Itembe amemshukuru Eliakimu Maswi kumwezesha kifaa hicho na kusema kitamsaidia kufanikisha kazi zake na kuongeza kuwa hajawahi kumiliki Kompyuta mpakato kwani amekuwa akifanya kazi zake kwenye kompyuta za watu.
Mwandishi wa habari Augustine Mgendi akimkabidhi kompyuta mpakato (Laptop) Mwandishi wa habari wa kujitegemea gazeti la Nipashe , Timothy Itembe miongoni mwa waandishi wa habari waliopewa kifaa hicho, vilivyotolewa na Katibu mkuu wizara ya katiba na Sheria Eliakim Maswi.
" Nampongeza Maswi na nimtakie afya njema na maisha marefu , mwenyezi Mungu amfungulie madirisha ya kipato pamoja na moyo wa kutoa ili kuendelea kusaidia wengine wenye uhitaji.
" Laptop hii itanisaidia sana maana nilikuwa nahangaika kwenda internet za watu kuchapa habari ama kutumia kompyuta za watu kwakuwa sikuwa na uwezo wa kununua kompyuta jambo ambalo limenitesa kwa miaka mingi.
" Kwa sasa nitaweza kufanya kazi zangu hata nikiwa nyumbani sitahangaika kwenda kuchapa internet, mara umeme ukatike lakini laptop ukiichaji hata umeme ukikatika utaendelea kufanya kazi zako bila kupoteza muda " amesema Itembe.
Amemuomba Katibu mkuu huyo asichoke kuisaidia jamii yakiwemo makundi mbalimbali yenye uhitaji na kusema kwamba Tarakilishi hizo zimeleta furaha kwa waandishi wa habari ambao hawakuwa nazo.
Mwandishi wa habari Augustine Mgendi akimkabidhi kompyuta mpakato (Laptop) Mpiga picha wa Star TV Amos Chitara , miongoni mwa waliopewa kifaa hicho, vilivyotolewa na Katibu mkuu wizara ya katiba na Sheria Eliakim Maswi
Post a Comment