HEADER AD

HEADER AD

WANANCHI NYASHIMBA MASWA WAANZA MCHAKATO UJENZI WA SHULE

Na Samwel Mwanga, Maswa

BAADA  ya kilio cha muda mrefu cha wananchi wa kijiji cha Nyashimba(M) kilichopo Kata ya Ng’higwa wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu cha watoto wao kutembea umbali mrefu kufuata elimu,wameanza kuchangishana kwa hiari na kutumia nguvu kazi kujenga shule ya sekondari.

Hatua hiyo imekuja baada ya malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wazazi na walezi kuhusu wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi kulazimika kusafiri zaidi ya kilomita 20 kwenda shule za sekondari za vijiji jirani, hali inayochangia baadhi yao kutohudhuria masomo kwa wakati na  kuacha shule .

Hayo yameelezwa Julai 21,2025 na Mwenyekiti wa kijiji cha Nyashimba,Balu Jiliya katika mkutano uliofanyika kijijini hapo ambapo amesema kuwa wameamua kwa pamoja kuanzisha mchakato huo baada ya kuona mateso wanayopitia watoto wao kila siku ya masomo kutembea umbali mrefu kwenda shule ya sekondari Sukuma iliyoko kijiji cha Mwadila.

           Mwenyekiti wa kijiji cha Nyashimba(M)Ballu Jilya (aliye kati)akiongoza mkutano wa kijiji hicho.

 “Tumeamua kwa moyo mmoja kujenga shule yetu ya sekondari ili kuwaondolea watoto wetu mateso ya kusafiri umbali mrefu,tayari tumepata eneo la ujenzi na kila mwananchi anachangia na kila kaya Sh 10,500/- na tayari tuna matofali 6,000, mchanga na kokoto,”amesema.

Happines Sayayi ni mkazi wa kijiji hicho amesema kuwa hatua hiyo ni ya faraja kwa wazazi ambao walikuwa wakihaha kutafuta fedha za usafiri au kupanga nyumba za watoto kwenye vijiji vya mbali.


     Happiness Sayayi mkazi wa kijiji cha Nyashimba(M)akielezea hali ya umbali mrefu wa watoto wao kwenda shule ya kijiji jirani cha Mwadila wilaya ya Maswa.

“Tulikuwa tunahangaika sana, wengine tulikuwa tunalazimika kuwapeleka kwa ndugu ili waishi karibu na shule,hii shule itapunguza gharama na kuweka mazingira bora ya kujifunzia kwa watoto wetu,”amesema.

Naye Sayi Mipawa ni mkazi wa kijiji hicho amesema kuwa wanatambua umuhimu wa elimu kwa watoto wao hivyo hawawezi kusubiri hadi serikali iwajengee shule ya sekondari.

      Sehemu ya matofali 6,000 yalinunuliwa na wananchi wa kijiji cha Nyashimba (M)kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya kijiji hicho.

“Tunatambua kuwa elimu ni ufunguo wa maisha, hatuwezi kuendelea kuwa nyuma kwa sababu ya kutegemea kila kitu kutoka serikalini,tumeamua kuanza sisi, tukiwa na matumaini kuwa serikali itatuunga mkono baadaye,”amesema.

 Afisa Elimu Kata ya Ng’hwigwa,Jane Kidoto amesema kuwa upatikanaji wa shule hiyo utakuwa mkombozi mkubwa kwa jamii ya Nyashimba, hasa kwa watoto wa kike ambao mara nyingi hulazimika kukatisha masomo yao kutokana na kushawishika na vishawishi mbalimbali wanapokuwa safarini.

       Afisa Elimu Kata ya Ng’hwigwa, Jane Kidoto akizungumza na wananchi wa kijiji hicho juu ya ujenzi wa shule ya sekondari.

“Hii ni hatua ya kishujaa,kupatikana kwa shule ya sekondari ya kijiji cha Nyashimba,kutapunguza mimba za utotoni, kuwapa wasichana nafasi sawa ya kupata elimu, na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla,” amesema.

Naye Afisa Mtendaji wa Kata hiyo,Yohana Simba amesema kuwa hadi sasa, wananchi wanaendelea na kuchanga fedha na kusomba mawe kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vya awali huku akitoa wito kwa wadau wa maendeleo, taasisi binafsi na serikali kuunga mkono juhudi hizo.

     Afisa Mtendaji wa Kata ya Ng'hwigwa, Yohana Simba akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nyashimba(M)juu ya ujenzi wa shule ya sekondari ya kijiji hicho.

Mpango huu wa ujenzi wa shule ya sekondari Nyashimba unaakisi dhamira ya jamii kuchukua jukumu katika kuboresha huduma za elimu, sambamba na juhudi za serikali kupeleka elimu karibu na wananchi.

No comments