HEADER AD

HEADER AD

RAIS SAMIA ATOA SIKU TANO TPA KUPELEKA HUDUMA ZOTE BANDARI KAVU YA KWALA


Na Gustaphu Haule, Pwani 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan  ametoa siku tano kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha inapeleka huduma zote muhimu katika Bandari Kavu ya Kwala ili kurahisisha huduma kwa watumiaji wa Bandari hiyo.

Rais Samia ameielekeza Wizara ya Uchukuzi kuhakikisha inashirikiana na sekta binafsi kuhamasisha utumiaji wa  miundombinu ya Bandari Kavu ya Kwala ili  kuondoa msongamano wa malori Jijini Dar es Salaam.

Rais Samia ametoa maelekezo hayo Julai 31,2025 wakati akizungumza na Wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kwala Mkoani Pwani mara baada ya kuzindua Bandari Kavu ya Kwala pamoja na kupokea Mabehewa mapya na yaliyokarabatiwa ya MGR.

        Rais Samia Suluhu Hassan akizindua Bandari ya Kavu ya Kwala leo Julai 31, 2025.

Amesema,kupatikana kwa huduma hizo katika Bandari Kavu ya Kwala itawasaidia wale wanaohitaji huduma hizo wanapofika Vigwaza wanaingia moja kwa moja Kwala na hivyo kuwaondolea usumbufu madereva kwenda Dar es Salaam.

"Kutokana na mahitaji muhimu ya Bandari hii ya Kwala na umuhimu wake sasa naagiza TPA kuhakikisha ifikapo Agosti 4,2025 huduma zote zihamishiwe hapa ili kurahisisha huduma katika Bandari hii,"amesema Rais Samia.

Mbali na Rais Samia kutoa maelekezo hayo lakini pia ametaka huduma zote muhimu ziwepo katika Bandari hiyo ikiwemo kituo cha polisi huku akiagiza pia viwango vya ukodishaji vipungue ili kuwavutia wakodishaji.

         Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ( katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala iliyopo Mkoani Pwani hafla hiyo imefanyika leo, Julai 31,2025.

Rais Samia amesema kuwa uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala itachochea uchumi wa Taifa na mtu mmojammoja na kwamba mpaka sasa tayari wateja na wafanyabiashara wakubwa akiwemo GSM wamevutiwa na reli hiyo.

Kuhusu Kongani ya viwanda iliyopo Kwala Rais Samia amesema kuwa, kituo hicho kitatoa fursa kwa wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi huku akiwahita wawekezaji wa kati na wakubwa waje kuwekeza katika eneo hilo.

       Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan akiweka jiwe la msingi katika Kongani ya viwanda iliyopo Kata ya Kwala Halmashauri ya Kibaha Vijijini katika hafla iliyofanyika Julai 31,2025.

Ameagiza TRC kuhakikisha wawekezaji walioonyesha nia ya kuwekeza katika eneo hilo wasikwamishwe kwakuwa anataka kuona siku zijazo mteja yeyote anaagiza mzigo wake kupitia Bandari ya Kavu ya Kwala.

Amesema Serikali inampango wa kuunganisha Bandari  Kavu ya Kwala na Bandari ya Bagamoyo  pamoja na Tanga ambapo kwasasa usanifu unaendelea kwa kuunganisha reli ya Mwendokasi(SGR).

Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa,amesema kuwa sekta ya uchukuzi ni kiungo muhimu katika uendeshaji wa maisha ya kila siku ya Mtanzania.

Profesa Mbarawa amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya uchukuzi ambapo amemshukuru Rais Samia kwa kutoa kipaumbele cha uendelezaji wa reli za kisasa hapa nchini.

    Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan akiwasili katika Kata ya Kwala leo Julai 31,2025 kwa ajili ya kupokea Mabehewa mapya ya mizigo ya reli ya Mwendokasi (SGR) na uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini Mkoani Pwani.

Amesema katika kuimarisha miundombinu ya bandari ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala ni kufuatia sababu mbalimbali ikiwemo sababu ya kiuchumi na sababu ya kijamii na hiyo ilitokana na uwezo mdogo wa bandari Kavu 11 zilizopo nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya hususani katika kuleta maendeleo Mkoa wa Pwani.

Kunenge amesema kuwa Rais Samia alipoingia madarakani mwaka 2021kulikuwa na viwanda 1,387 na sasa Kuna Viwanda 1,681 ambapo vikubwa vilikuwa 59 na sasa vimefika 97 sawa na ongezeko la asilimia 73 huku Viwanda vya kati vikiongezeka 71.

Hata hivyo Kunenge amesema viwanda hivyo vimetoa ajira ya moja kwa moja 21,000 na ajira za muda mfupi 60,000 huku akiongeza kuwa kwasasa Mkoa wa Pwani Kuna viwanda vinazalisha Tv,nondo,vioo,magari, Saruji, Chuma,na dawa za mifugo na binadamu.

No comments