HAWA MCHAFU AJIZOLEA KURA 802 UCHAGUZI NAFASI YA UBUNGE VITI MAALUM KURA ZA MAONI
Na Gustaphu Haule, Pwani
ALIYEKUWA mbunge wa Viti maalum kutoka mkoa wa Pwani Hawa Mchafu Chakoma amefanikiwa kutetea nafasi yake baada ya kujizolea kura 802 na kuwaacha mbali washindani wake.
Hawa ameibuka kidedea katika uchaguzi wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT) uliofanyika Julai 30,2025 katika viwanja vya Shule ya uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo katika Manispaa ya Kibaha Mkoani Pwani.
Katika uchaguzi huo Hawa alikuwa akichuana na wenzake Saba lakini hata hivyo amefanikiwa kuwa kinara katika uchaguzi huo na hivyo kufanikiwa kurudi katika ulingo wa siasa kwa nafasi ya ubunge wa Viti maalum.
Hawa Mchafu akiomba kura kwa wajumbe katika uchaguzi wa Wabunge wa Vitimaalum Mkoa wa Pwani uliofanyika Julai 30,2025 katika Shule ya uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kibaha Mkoani Pwani.
Wagombea wengine waliokuwa wakichuana na Hawa Mchafu ni Mariam Abdallah ((645),Nancy Mutalemwa (449),Irene Makongoro (56),Fatuma Uwesu (71),Sifa Mwaruka(44) ,Rehema Issa (26) na Rehema Mssemo(7).
Hata hivyo,katika uchaguzi huo idadi ya wajumbe waliopiga kura ilikuwa 2095 ambapo kura zilizoharibika 5 ,na kura halali ni 2,108.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi Hawa amemshukuru Mungu kumaliza uchaguzi huo salama lakini pia amewashukuru wajumbe kwa kumpigia kura nyingi zilizompa ushindi huku akisema hana cha kuwalipa lakini mwenyezi Mungu atawalipa maradufu.
Amesema kikubwa ni kuendelea kushirikiana kuhakikisha wanamvusha Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu ili kusudi Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Jumuiya zake kiweze kushika dola.
Amesema kuwa ili CCM iweze kusongambele inahitaji ushirikiano na mshikamano huku akisema CCM inahitaji kuwa na mafiga matatu akiwemo Rais, wabunge na madiwani na kinachotakiwa ni kuhakikisha Oktoba CCM inakuwa kinara katika maeneo yote.
"Binafsi nawashukuru sana wajumbe kwa kunichagua maana huo ni utashi wao, kwakuwa tulikuwa wagombea wengi lakini wakaona nafaa na wakanipa kura nyingi zilizonifanya niweze kuongoza katika uchaguzi huu,"amesema .
Hawa amesema pamoja na kuwashukuru wajumbe hao lakini pia shukrani zake anazipeleka kwa viongozi wa chama na Jumuiya kwa kurudisha jina lake kwakuwa waliochukua fomu za kugombea walikuwa wengi lakini yeye alikuwa miongoni mwa wale waliorudishwa.
Post a Comment