HEADER AD

HEADER AD

TAKUKURU KAGERA YAWATAKA WANANCHI KUTOJIHUSISHA NA VITENDO VYA RUSHWA

Na Alodia Dominick, Karagwe

WANANCHI hapa nchini wameaswa kuwa waadilifu na kutotoa wala  kupokea rushwa wakati wa kuelekea  kuchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Wito huo umetolewa na Ofisa wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) Wilaya ya Karagwe Miriam Kirangi alipokuwa mgeni rasmi katika mahafari ya 28 ya  chuo cha Perfect Education and Training Insitute (PETI) kilichopo wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.

       Mgeni rasmi katika Mahafari ya 28 Chuo cha PETI kutoka Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Karagwe Miriam Kirangi akizumgumza na wananchi pamoja na wanachuo.

"Tunapoelekea katika kipindi cha uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu nitumie nafasi hii kuhimiza wananchi, kutojihusisha na vitendo vya rushwa tusitoe wala kupokea rushwa nyinyi wanajamii na wagombea" amesema Kirangi.

Ameongeza kuwa, rushwa ni adui wa haki siyo sawa mgombea ambaye hana sifa anatumia fedha zake kusawishi wananchi wampigie kura, hivyo akawasihi wananchi kutojihusisha na kupokea rushwa kwani kufanya hivyo watakuwa wamekosa uadilifu na wanaweza kumpata kiongozi asiyefaa.

Kirangi amewaasa wahitimu kuwa,  elimu waliyoipata isiishie hapo wakaitumie huko wanakokwenda kwani walipokuwa chuoni wamejifunza mambo mengi ikiwemo nidhamu, maadili na namna ya kuishi vizuri katika jamii.

"Huko mnakokwenda katika vituo vyenu vya kazi nafurahi kwamba chuo chenu mkimaliza uongozi wa chuo hauwaachi  unahakikisha mnapata maeneo ya  kufanyia mafunzo kwa vitendo (field) niwasihi mnapokuwa huko kuweni waadilifu kwani ndiyo nguzo kuu ya utumishi, mtakapokosa maadili huko mnakokwenda hamtaweza kufanikiwa"

"Maadili, heshima, uwajibikaji ni msingi mzuri katika maisha na katika eneo la kazi kwa nyinyi mliopata nafasi ya kusoma itumie vizuri kuna wengine wanaihitaji lakini hawaipati, itumie kwa uadilifu na heshima kwa kufuata sheria za nchi.

Akijibia changamoto zilizopo chuoni hapo amesema, kuwa watajadili na Mkurugenzi wa chuo hicho namna ya kuzitatua na Mkurugenzi atatoa mrejesho.

           Mkurugenzi wa chuo cha PETI Mbeki mbeki akizungumza.

Mkurugenzi wa Chuo cha Perfect education and Training Institute(PETI) Mbeki Mbeki ametaja changamoti zilizopo Chuoni hapo na kusema kwamba, Chuo kina upungufu wa kompyuta sita, meza na viti 70, vyumba vya madarasa vitatu na mifuko 70 ya saruji.

Mbeki ameiomba Serikali kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya kati kutokana na baadhi ya wazazi kushindwa kumudu gharama za kuwalipia watoto wao.

Amesema chuo hicho kinatoza karo milioni 1.3 kwa miaka miwili huku akiomba serikali kuwalipia fedha laki 7 na mzazi alipe laki 6.

"Serikali iangalie namna ya kutoa mkopo kwa vijana wa vyuo vya kati maana baadhi ya familia zinashindwa kumudu gharama za chuo na hivyo kusababisha baadhi ya vijana kuacha masomo na wengine kutokwenda kabisa" amesema Mbeki .

Ameeleza kuwa wanachuo waliohitimu wako watano wa kike wanne na mmoja wa kiume katika kozi za uandishi wa habari na utangazaji, Hoteli pamoja na maswala ya Utalii, walianza wakiwa 10 wa kike nane na kiume wawili watano waliachwa njiani.

Amesema tangu chuo kilipoanza mwaka 2014 hadi sasa wameishahitimu wanachuo zaidi ya 580 na waliopo kazini ni zaidi ya 540.

" Kuna wanafunzi kutoka chuoni hapo wamesomea utalii wako nchini China  na watoto 40 ambao hawakusomea chuoni hapo wamesaidiwa kupata sehemu ya kusoma kwa vitendo (field). Naiomba Serikali ikiwezekana iondoe kodi katika vyuo na shule za binafsi" amesema.

Risala ya wahitimu iliyosomwa na Julieth Joas mhitimu kozi ya utangazaji na uandishi wa habari amemwomba mgeni rasmi kuwasaidia kutafuta ufadhiri kwa ajili ya kutatua changamoto mbali mbali zilizopo chuoni hapo.

Hata hivyo chuo cha PETI kinayo klabu ya wapinga rushwa  ambapo Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imekuwa ikitoa elimu ya maadili jinsi ya kupambana na rushwa nchini.

         Katika ni Ofisa wa TKUKURU Wilaya ya Karagwe Miriam Kirangi akipokea zawadi kushoto kwake ni mkurugenzi wa Chuo cha PETI Mbeki Mbeki na Kulia kwake ni mkuu wa chuo hicho.


          Wahitimu wakikata keki na mgeni rasmi.

No comments