RC PWANI AWAHIMIZA WATUMISHI KUFANYA KAZI KWA BIDII ILI KULETA MATOKEO CHANYA

Na Gustaphu Haule, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amefunga mafunzo ya kikao kazi cha Watumishi wa Manispaa ya Kibaha kwa kuwataka watumishi hao kujenga tabia ya kufanya kazi kwa bidii ili kuleta matokeo chanya.
Kunenge amesema anatamani kuwe na mfumo wa anayezalisha zaidi alipwe zaidi utaratibu ambao utamfanya kila mtumishi kufanya kazi kwa bidii kuleta matokeo chanya kwa jamii.
Kunenge ameyasema hayo Julai 27,2025 alipokuwa akifunga mafunzo kwa watumishi wa Manispaa ya Kibaha yaliyolenga kufanya tathmini ya utendaji wa kazi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya mwaka wa fedha wa 2024/2025 na kuangalia bajeti ya 2025/2026.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Kibaha katika mkutano wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo Cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani."Kigezo sio cheti kazini lakini utendaji kazi wako ndio unaotakiwa kazi yako ikiwa nzuri mwisho utaonyesha kwamba imetokana na cheti ulichonacho na wote tukisimama hivi hakuna kitu kitakachoyumba",amesema.
Amesema watumishi hao kila mmoja kwenye idara yake kuhakikisha atatatua kero za wananchi kabla hazijafika ngazi ya juu huku akisisitiza ushirikiano kwenye maeneo ya kazi kwa kufanya kazi kama timu moja.
Amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha kwa kazi nzuri anayofanya ikiwa pamoja na kuandaa kikao hicho na kwamba mkurugenzi huyo anauwezo mkubwa na anaweza kufanya vizuri katika Manispaa ya Kibaha.
Awali akimkaribisha mkuu wa mkoa, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dk.Rogers Shemwelekwa amesema kuwa watumishi hao katika kikao kazi hicho cha siku mbili watumishi hao wamepewa mafunzo ya aina mbalimbali.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt . Roger's Shemwelekwa akizungumza katika na watumishi wa Manispaa hiyo katika mkutano wa kikao kazi kilichofanyika kwa siku mbili katika Chuo Cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.Ametaja mada zilizofundishwa pamoja katika kikao hicho kuwa ni ushiriki wa utendaji kazi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, mfumo wa mawasiliano katika utumishi wa umma ,usimamizi na uendeshaji wa taarifa za elimu na ushirikishwaji wa wadau.
Mada nyingine ni pamoja na maadili na utawala bora,usalama na usiri katika utumishi wa umma,afya na akili, uongozi wa ufanisi kufanyakazi kwa pamoja na muelekeo wa utendaji kazi wa mwaka 2025/2026.
Shemwelekwa amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2024/2025 Manispaa ya Kibaha imetekeleza miradi mingi na mikubwa yenye maslahi mapana kwa Wananchi ikiwemo ujenzi wa Shule za msingi na Sekondari,vituo vya afya, ujenzi wa miradi ya maji na hata mikopo kwa wajasiriamali.
Watumishi wa Manispaa ya Kibaha wakiwa katika mkutano wa kikao kazi uliofanyika Julai 26 na 27,2025 katika chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.Amesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026 Manispaa ya Kibaha imejipanga kukusanya zaidi ya Tsh. Bilioni 13 za mapato ya ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na kuendesha shughuli za Manispaa.
Amesema malengo ya Manispaa ni kufikia makusanyo ya bilioni 20 za mapato ya ndani lakini kwasasa tayari Manispaa imeweka mipango mbalimbali ya utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo.
Amesema katika kipindi cha mwaka 2025/2026 pamoja na kutekeleza miradi mingi ya maendeleo lakini mipango yao ni kutekeleza miradi mikubwa mitatu ya kimkakati itakayokwenda kuimarisha zaidi mapato ya Halmashauri.
Dkt. Shemwelekwa amesema miradi hiyo ya kimkakati ni pamoja na ujenzi wa kituo cha Sheli ya mafuta, kituo cha biashara na maegesho ya magari na kwamba wanafanya hivyo kuendana na mabadiliko ya kisera pale yatakapotokea.
Watumishi wa Manispaa ya Kibaha wakiwa katika mkutano wa kikao kazi kilichofanyika katika chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani Julai 26 na Julai 27, 2025.Amesema miradi hiyo imetengewa zaidi ya sh.bilioni 2 huku kila kata ikitengewa fedha kwa ajili ya samani za ofisi na fedha za mafuta ya pikipiki zao ili kurahisisha utendaji kazi kwa kuwafikia wananchi kwa urahisi.
Shemwelekwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Kibaha.
Afisa utumishi mkuu wa Manispaa ya Kibaha Mrisho Mlela awali akimkaribisha mkurugenzi wa Manispaa amesema anampongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanya lakini pia amempongeza mkurugenzi wa Manispaa Dkt.Roger's Shemwelekwa kwa kuandaa mkutano huo.
Mlela amesema kuwa kikao hicho kimejumuisha washiriki 600 wakiwemo Maafisa watendaji Kata na Mitaa, Walimu wa shule za Sekondari na Msingi pamoja na wasaidizi wao, Maafisa maendeleo ya Jamii, Maafisa ustawi wa jamii, Maafisa ugani,Maafisa afya , Wakuu wa vitengo na kada nyingine .
Post a Comment