HEADER AD

HEADER AD

KUJUANA KWA MICHANGO

HIVI twafahamiana, au tumeshaonana?

Vipi sasa nakuona, unasogea kijana?

Nini kwangu umeona, hata sasa twaitana?

Kujuana kwa michango, mimi sipendi kabisa.

Hivi wewe hasa nani, ndio leo nakuona,

Unajua mimi nani, huko tunaalikana?

Tulishaonana lini, wadai tunajuana?

Kujuana kwa michango, mimi sipendi kabisa.

Na maana waniona, yangu nahangaishana,

Hapo wewe wauchuna, ntajijua unaona,

Huna soni ninaona, kutafuta kupatana,

Kujuana kwa michango, mimi sipendi kabisa.

Sisi ni ndugu naona, japo hatujakutana,

Sura ninayoiona, jamii moja naona,

Ila kwa sasa nanuna, badaye tutaonana,

Kujuana kwa michango, mimi sipendi kabisa.

Ndugu kusaidiana, wala siyo kuchunana,

Ndugu kutembeleana, wala si kuviziana,

Ndugu kufurahiana, wala si kukomoana,

Kujuana kwa michango, mimi sipendi kaba.

Ufanye kutafutana, ili tuweze jengana,

Pamoja tutaungana, tutafanya mengi sana,

Hizi za kutegeana, ndio mwanzo wa fitina,

Kujuana kwa michango, mimi sipendi kabisa.

Tunafanana majina, usoni sijakuona,.

Si usiku si mchana, hatujawahi kutana,

Kulipata langu jina, sasa wataka nivuna,

Kujuana kwa michango, mimi sipendi kabisa.

Kwa hilo ninauchuna, hata tusipoonana,

Wala sina konakona, ndivyo tunavyopashana,

Hayo yako malizana, badaye tujekutana,

Kujuana kwa michango, mimi sipendi kabisa.

Hebu jianze kijana, ukitaka kupatana,

Viraka anza kushona, hadi tutapojuana,

Tuje kutembeleana, hata kusaidiana,

Kujuana kwa michango, mimi sipendi kabisa.

Watu tuache fitina, lawama ziso maana,

Za huku kutafutana, shida zinapotubana,

Shida zao tunanuna, kwao twapenda kuvuna,

Kujuana kwa michango, mimi sipendi kabisa.

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments