HEADER AD

HEADER AD

MKURUGENZI MKUU TAKUKURU AWATAKA WANASHERIA KUWADHIBITI WAGOMBEA WATAKAOTOA RUSHWA


 Na Gustaphu Haule, Pwani

MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Crispin Chalamila, amewataka wanasheria wa taasisi hiyo kuwadhibiti baadhi ya wagombea watakaobainika kutoa rushwa katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa kufanya uchunguzi wa kina na wenye tija.

Chalamaila ametoa agizo hilo wakati akifungua mafunzo ya kuimarisha weledi wa taaluma ya Sheria kwa wanasheria wa Takukuru 307 kutoka mikoa yote nchini yaliofanyika katika shule ya uongozi ya mwalimu nyerere Mjini Kibaha,mkoani Pwani.

       Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Crispin Chalamila akifungua mafunzo ya kuwajengea uweledi wanasheria wa taasisi hiyo yaliyoanza kufanyika Agosti 25/2025 katika chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani.

Amesema  majukumu makuu ya taasisi hiyo ni kutoa elimu ya rushwa kwa umma, kuzuia rushwa na kufanya uchunguzi na kwamba katika kipindi hichi cha uchaguzi ni wanasheria hao wanajukumu kubwa la kuchunguza vitendo vya rushwa na kudhibiti hatua itakayosaidia upatikanaji wa viongozi bora.

"Sasa tunaelekea katika kipindi cha kampeni ambacho kitachukua miezi miwili, ni wakati wenu kufanyakazi ili kuchunguza vitendo vya rushwa ni dhahiri kwamba viongozi ambao wanaopatikana kwa njia ya rushwa ni ngumu  kutusaidia kusimamia miradi"amesema

Amesema iwapo wanasheria hawata tekeleza jukumu hili vema litasababisha kupatikana kwa viongozi  wa bovu na wasio kuwa na nia njema katika kutumikia jamii ikiwemo kushindwa kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao na kuisababishia serikali hasara.

    Wanasheria wa Takukuru wakishiriki mafunzo ya kujengewa ueledi yanayofanyika chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere Kibaha Mkoani Pwani.

"Tuwe makini haswa viongozi hao ambao ni madiwani na wabunge miradi mingi inatekelezwa kwao na wao wapo karibu kule na tukiangalia sisi ni wachache hivyo watatusaidia kuibua vitendo vya ubadhirifu katika miradi iliyopo kwenye kata zao na majimbo yao"alisema

Mbali na hilo aliwataka kuhakikisha wanafanya uchunguzi nzuri hatua ambayo itasaidia kutengeneza ushahidi mzuri itakaosaidia kushinda kesi mbalimbali za rushwa na kufikia malengo waliojiwekea ikiwemo kutaifisha mali zote zilizopatika kwa rushwa.

Chalamila amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa akipigania taasisi hiyo na kuridhia kufanyika kwa mafunzo hayo kwa wanasheria wake.

Amesema mafunzo hayo mara ya mwisho yalifanyika mara ya mwisho mwaka 2011 kwahiyo anaimani kwasasa mafunzo hayo yataimarisha utendaji kazi wa kila siku.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa taasisi hiyo nchini, George Balasa, amesema wanasheria 307 wamenufaika na mafunzo hayo na kwamba watapata fursa za kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo mbinu mbalimbali za kisheria, ukusanyaji wa ushahidi kwa njia za kielektroniki, mabadiliko yasheria mbalimbali na masuala ya afya.

"Mafunzo haya yatasaidia kuboresha weledi na mbinu mpya katika utendaji kazi katika taasisi yetu kama mnavyojua malengo yetu ni kufikia asilimia 85 ya kesi tunazozipeleka kushinda  na asilimia mia moja ya mali zote zilizopatikana kwa rushwa kurejeshwa serikalini"amesema 

Afisa uchunguzi wa TAKUKURU  nchini, Biswalo Biswalo, amesema  mafunzo hayo yatawasaidia zaidi kujua  mabadiliko ya Sheria mbalimba ikiwemo  mabadiliko ya Sheria ya umma 2023 sambamba na mabadiliko ya teknolojia katika tasnia ya Sheria.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani Domina Mkama amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru kwa kuhakikisha mafunzo hayo yanafanyika Mkoa wa Pwani.

Hata hivyo , Mkama amesema kuwa mafunzo hayo ya siku mbili yanamanufaa makubwa kwao kwakuwa yatawasaidia wanasheria katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

        Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Crispin Chalamila (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanasheria kutoka mikoa mbalimbali nchini mara baada  ya kufungua mafunzo ya siku mbili ya wanasheria hao yaliyofanyika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kibaha Mkoani Pwani.

No comments