VURUGU ZA MWENYE NYUMBA
MWENYE nyumba kichukia, vizuri kwa mpangaji,
Kule ulikolalia, akili inakuchaji,
Uweze kujipatia, kiwanja hata Kimbiji,
Vurugu za mwenye nyumba, muda mwingine baraka.
Kama unajiishia, mwenye nyumba hajihaji,
Unaweza fikiria, hapo umejenga mji,
Hadi kodi kutimia, ndipo walijua jiji,
Vurugu za mwenye nyumba, muda mwingine baraka.
Vile unasumbukia, kulipa bili ya maji,
Mwenye nyumba akwachia, mabomba yavuja maji,
Unaanza fikiria, nawe utafute mji,
Vurugu za mwenye nyumba, muda mwingine baraka.
Vile afuatilia, kwako wageni hawaji,
Choo watamjazia, nakuyamaliza maji,
Afanya unabakia, wewe siyo mwenye mji,
Vurugu za mwenye nyumba, muda mwingine baraka.
Kile unajipikia, na ule wa kwako uji,
Anakufuatilia, hata kukuhojihoji,
Vipi anakuvizia, wako huo uhitaji,
Vurugu za mwenye nyumba, muda mwingine baraka.
Kodi ikikuishia, na dharura mahitaji,
Kesho utampatia, hiyo habari hachuji,
Dhihaka takufanyia, ubaki meloa maji,
Vurugu za mwenye nyumba, muda mwingine baraka.
Mambo anakufanyia, kwako yawe ni mtaji,
Kiwanja kufikiria, kujenga nje ya mji,
Bila fujo kukujia, ngebakia mpangaji,
Vurugu za mwenye nyumba, muda mwingine baraka.
Muziki kusikizia, hilo kwako ndilo taji,
Mwenye ukifungulia, waleta homa ya jiji,
Mara ataingilia, kelele hazihitaji,
Vurugu za mwenye nyumba, muda mwingine baraka.
Si vema kushangilia, utwezwavyo mpangaji,
Ni ujinga nakwambia, wafanyavyo washikaji,
Manyanyaso kufanyia, ndugu zetu wapangaji,
Vurugu za mwenye nyumba, muda mwingine baraka.
Ila ukiangalia, kelele wazihitaji,
Usibaki watulia, bila kutafuta mji,
Pale utaposikia, unaitwa mwenye mji,
Vurugu za mwenye nyumba, muda mwingine baraka.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment